2017-08-10 12:30:00

Watawa Afrika Mashariki na Kati, kujizatiti katika Uinjilishaji!


Shirikisho la Mashirika ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki na Kati, ACWECA, kuanzia tarehe 26 Agosti hadi tarehe 2 Septemba 2017, linafanya mkutano wake wa 17 unaoongozwa na kauli mbiu “Kuimarisha umoja wetu katika uinjilishaji wa kina mintarafu mazingira changamani ya nyakati hizi”. Mkutano huu utafunguliwa kwa Ibada ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Kardinali João Braz de Aviz, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mashirika ya Kitawa na Kazi za kitume na itafanyika kwenye Makao makuu ya Sekretarieti ya Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, Kurasini, Jijini, Dar Es Salaam.

Sr. Prisca Matenga, Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki na Kati anasema, kauli mbiu hii ni changamoto kubwa kwa Mashirika wanachama kuimarisha umoja kati yao, kwani umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu. Watawa wanataka kuimarisha umoja, ili kuadhimisha kwa pamoja umoja na ushirikiano wao wa kidugu. Watawa wanaishi katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, unaoufanya ulimwengu kuwa kama “kijiji”. Kuna mambo yanayobadilika haraka sana na hili ni jambo muhimu kwa watawa kulivalia njuga kwa kupyaisha maisha yao ya kijumuiya, ili kuweza kuangalia mambo kwa kutumia “miwani ya Kristo Yesu”, ili hatimaye, kuimarisha umoja na mshikamano kwa ajili ya uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu: kiroho na kimwili.

Watawa Afrika Mashariki na Kati anasema Sr. Prisca Matenga, wanataka kujizatiti kuimarisha umoja na mshikamano wao, ili Injili ya huruma na huduma ya mapendo, iweze kuzaa matunda yanayokusudiwa, yaani, ustawi, maendeleo na mafao ya watu wengi wa Afrika Mashariki na Kati! Kwa upande wake, Sr. Eneless Chimbali, Katibu mkuu wa ACWECA anakaza kusema, dira ya Shirikisho hili ni kukuza na kudumisha ari na moyo wa ushirikiano wa rasilimali na tunu za maisha ya kiroho; kiuchumi na kiutu, ili kuendeleza mchakato wa malezi na majiundo ya watawa; kuwajengea watawa nguvu na uwezo wa kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina.

Mashirika ya kitawa Afrika Mashariki na Kati yanatofautiana kwa utajiri na rasilimali watu, vitu na fedha. Kumbe, kwa njia ya umoja, upendo na mshikamano wa dhati, watawa wataweza kupata mafanikio makubwa, ikilinganishwa na mafanikio ambayo yangeweza kupatikana, ikiwa kama kila Shirika lingetenda “kivyake vyake”. Kwa upande wake, Sr. Mary Abut, mjumbe wa ACWECA, anakaza kusema, dhamira ya mkutano huu ni matunda ya tafakari na safari ndefu iliyofanywa na watawa hawa. Hili ni jukwaa kwa wajumbe kuweza kupembua kwa kina mafanikio, changamoto na matatizo yaliyojitokeza katika utekelezaji wa maamuzi yaliyokuwa yamefikiwa kwenye Mkutano mkuu wa 16.

Uongozi imara, malezi ya awali na endelevu; nguvu ya kiuchumi ili kujitegemea na kutegemeza miradi yao ni mambo ambayo yatajadiliwa kwa kina na mapana. Shirikisho la Mashirika ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki na Kati linaanza kutekeleza mpango mkakati wa uongozi na malezi kwa Mwaka 2017 hadi mwaka 2022. Malezi ya awali na endelevu ni muhimu sana katika maisha na wito wa watawa hususan katika ulimwengu mamboleo. Watawa wanapaswa kuandaliwa vyema, ili kujisadaka bila ya kujibakiza kwa Mungu na jirani zao, kwa kumwilisha ndani mwao nadhiri na maisha ya kijumuiya ili kutekeleza vyema utume wao kati ya watu wa Mungu wanaowahudumia kila siku. Shirikisho la Mashirika ya Watawa wa Kike Afrika Mashariki na Kati, ACWECA, linaundwa na Mashirika ya kitawa kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati yaani: Ethiopia, Kenya, Uganda, Tanzania, Malawi na Zambia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.