Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Sala ya Malaika wa Bwana

Papa Francisko akemea na kulaani mashambulizi kwenye nyumba za ibada

Papa Francisko wakati wa Katekesi yake Jumatano, tarehe 9 Agosti 2017 amewakumbuka na kuwaombea wananchi wa Nigeria na Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati ambao wanaishi katika vita, ghasia na kinzani za kijamii. - REUTERS

10/08/2017 11:39

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 9 Agosti 2017, kuhusu matumaini ya Kikristo amesema kwamba, Kanisa linaundwa na wadhambi ambao daima wanapaswa kuchuchumilia huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao, ili waweze kupata matumaini ya maisha mapya. Amewataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo kwa waja wake. Utume na dhamana ya kwanza ya Mama Kanisa ni kuendelea kuwa ni hospitali katika uwanja wa mapambano; mahali pa kuganga na kutibu majeraha ya mwanadamu: kiroho na kimwili: kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini.

Kanisa halina budi kuwa ni mahali pa huruma na msamaha; chemchemi ya matumaini kwa wale waliokata tamaa; wagonjwa na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Waamini kwa kuonja huruma na msamaha kutoka kwa Mwenyezi Mungu, wageuke na kuwa ni vyombo na mashuhuda wa huruma kwa jirani zao! Baba Mtakatifu anakaza kusema, kila aina ya chuki na uhasama; vita na ghasia ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na shambulizi lililofanywa huko nchini Nigeria kwenye Kanisa la Mtakatifu Filipo, huko Ozubulu, Kusini mwa Nigeria, Jumapili tarehe 6 Agosti 2017, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Siku kuu ya Kung’ara Bwana na kupelekea watu 11 kufariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa vibaya. Ni matumaini yake kwamba, vitendo vya kihalifu namna hii havitajirudia tena kwenye nyumba za Ibada, mahali ambapo waamini wanakusanyika kwa ajili ya sala na ibada. Kwa namna ya pekee, Baba Mtakatifu amewakumbuka wananchi wa Nigeria na wale walioko Jamhuri ya Watu wa Afrika ya kati; akaunganika na mahujaji ili kuwaombea ulinzi na tunza ya Bikira Maria, faraja na kimbilio la Wakristo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

10/08/2017 11:39