Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Vatican \ Hotuba

Kardinali Parolin anatembelea Russia kuanzia tarehe 20-24 Agosti 2017

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 20-24 Agosti ili kuimarisha uhusiano wa kidplomasia na Russia pamoja na kuendeleza majadiliano ya kiekumene. - AFP

10/08/2017 11:19

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake anapenda kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Injili ya amani, haki, upendo na mshikamano kati ya watu wa Mataifa. Leo hii kutokana na kinzani mbali mbali, mustakabali wa amani duniani uko mashakani! Kutokana na changamoto hii, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kuanzia tarehe 20 - 24 Agosti, 2017 anafanya ziara ya kichungaji nchini Russia. Akiwa nchini humo, Kardinali Parolin anatarajiwa kukutana na kuzungumza na Rais Vladimir Putin wa Russia na kwamba, tangu sasa anapenda kujiaminisha chini ya ulinzi, tunza na maongozi ya Roho Mtakatifu, ili kuendeleza uhusiano wa dhati uliopo kati ya Russia na Vatican sanjari na kuendeleza majadiliano ya kiekumene kati ya Kanisa Katoliki la Kanisa la Kiorthodox. Kumbe, atakutana pia na Patriaki Cyril wa Moscow na Russia nzima.

Itakuwa ni nafasi ya kuweza kujadiliana ana kwa ana na Rais Putin kuhusu mustakabali wa wananchi walioko huko Mashariki ya kati; mateso na mahangaiko ya wananchi wa Siria na Ukraine, nchi ambazo Russia ina mkono wake huko!  Vatican inatambua na kuthamini utajiri mkubwa unaofumbatwa katika: Imani, mapokeo, tamaduni na maisha ya wananchi wa Ulaya ya Mashariki. Wananchi hawa wakishirikishwa kikamilifu, wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kudumisha umoja na mshikamano wa dhati. Baada ya mapambano ya “Vita Baridi Duniani”, kuna haja sasa ya kufungua ukurasa mpya wa majadiliano na ushirikianano ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.

Huu ndio mwelekeo wa sera na mbinu mkakati wa diplomasia ya Vatican ili kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajenga madaraja ya kuwakutanisha watu wa Mataifa. Haya yamesemwa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Bwana Gian Guido Vecchi, wandishi wa habari wa Gazeti la “Corriere della Serra” linalo chapishwa kila siku nchini Italia. Anaendelea kufafanua kwamba, ziara hii ya kikazi ilikwisha kuandaliwa na kupangwa mapema, lakini matukio ya kinzani za kimataifa yaliyojitokeza hivi karibuni yanatoa uzito wa pekee wa ziara hii huko nchini Russia. Huu ni mwendelezo wa diplomasia ya Vatican huko: Caucaso, Bielorussia na Ukraine. Kumbe, lengo la pili la ziara hii ya kichungaji ni kutaka kushuhudia uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko kwa familia ya Mungu katika nchi hizi.

Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, Kanisa linaendelea kufanya majadiliano ya kina na viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa, ili kuwakumbusha dhamana na wajibu wao katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi sanjari na kuhakikisha kwamba, haki msingi za binadamu zinasimamiliwa na kutekelezwa barabara. Utekelezaji wa masilahi ya kitaifa yasivuruge umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa au kupindisha Sheria za Kimataifa. Jambo la msingi linalopaswa kukaziwa ni nguvu ya haki, amani, utulivu sanjari na majadiliano katika ukweli na uwazi. Ni matumaini ya Vatican kwamba, majadiliano ya kina na viongozi mbali mbali wa Jumuiya ya Kimataifa yatasaidia kuleta ufumbuzi wa kina katika migogoro inayotishia amani, usalama na mafungamano ya kimataifa.

Lengo la majadiliano ni kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kuokoa damu ya watu wasiokuwa na hatia isimwagike bure. Hadi sasa kuna watu wanaoteseka kutokana na vita, ghasia na kinzani za kijamii na kisiasa huko Siria, Mashariki ya Kati pamoja na Ukraine. Kardinali Parolin anakaza kusema, Kanisa linaguswa na mateso na mahangaiko ya watu sehemu mbali mbali za dunia, ndiyo maana Baba Mtakatifu katika utume wake, daima anayagusia maeneo haya. Tema ya amani ni kati ya mambo msingi kwenye mazungumzo na viongozi mbali mbali nchini Russia.

Kardinali Parolin ana matumaini kwamba, mgogoro wa kisiasa kati ya Russia na Serikali ya Marekani, utaweza kupatiwa ufumbuzi wa kudumu kwa pande zote mbili kuwajibika barabara kwa maamuzi yake. Serikali ziwe na ujasiri wa kukiri makosa  yaliyotendwa na wafanyakazi wake, na hivyo kuwa tayari kuanza mchakato wa maboresho ya mahusiano haya.

Kardinali Parolin anakaza kusema, katika mkutano wake na Patriaki Cyril wa Moscow na Russia nzima atawasilisha salam na mapenzi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayekazia uekumene wa sala na maisha ya kiroho; ushuhuda wa damu na huduma. Utakuwa ni wakati muafaka wa kuweza kujadili mchango wa Kanisa katika masuala mbali mbali ya kimataifa kwa wakati huu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo. Mshikamano wa Makanisa ni muhimu sana katika medani za kimataifa. Ziara hii pamoja na mambo mengine inaangalia uwezekano wa Khalifa wa Mtakatifu Petro, hatimaye, kwa msaada wa Mwenyezi Mungu kuweza kutembelea nchini Russia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

10/08/2017 11:19