Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa \ Kanisa Ulimwenguni

Vijana wamesimama imara kutangaza Injili na kupambana na changamoto!

Vijana Barani Asia wanasema wamejipanga vyema kutangaza na kushuhudia Injili sanjari na kupambana na changamoto za maisha ya ujana. - ANSA

09/08/2017 12:44

Maadhimisho ya Siku ya Saba ya Vijana Barani Asia kwa Mwaka 2017 yaliyoongozwa na kauli mbiu “Furaha ya vijana wa Bara la Asia: Kuishi Injili katika wingi wa makabila ya Bara la Asia” yaliyofunguliwa rasmi tarehe 31 Julai, 2017 yamefungwa kwa kishindo tarehe 6 Agosti 2017, wakati wa Sherehe ya Kung’ara kwa Bwana, changamoto na mwaliko kwa waamini kuhakikisha kwamba, mioyo na macho yao yanang’ara utukufu, ukuu na uweza wa Mungu, ili kweli wakristo kwa nafasi zao mbali mbali waweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya matumaini kwa wale waliokata tamaa!

Waamini wawe na ujasiri wa kushuka kutoka mlimani, ili kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na mshikamano inayomwilishwa katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake, aliwataka vijana Barani Asia kujifunza kwa bidii kutoka katika shule ya Bikira Maria, kwa kusikiliza kwa makini na kujiaminisha katika ulinzi na tunza yake ya kimama. Wawe tayari kumfuasa Kristo Yesu kama alivyofanya Bikira Maria katika maisha yake, ili waweze kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maboresho ya maisha ya watu, ili hatimaye, dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi.

Vijana katika tamko lao mara baada ya kuhitimisha maadhimisho ya Siku ya Saba ya Vijana Barani Asia kwa Mwaka 2017 wanasema,  wanakumbana na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali katika maisha yao ya Kikristo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Kumekuwepo na ongezeko kubwa la ulaji hasa kutokana na mabadiliko makubwa ya sayansi na teknolojia, kiasi cha kuwatumbukiza vijana katika tabia ya ulaji usiokuwa na kiasi. Vijana wengi wanakabiliwa na changamoto ya kukosa fursa za ajira na matokeo yake wanakata tamaa na kuanza kujiingiza katika vitendo ambavyo vinakwenda kinyume cha imani, kanuni maadili na utu wema!

Baadhi yao wamejikuta wakiwa ni “mateja” wa biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, mambo ambayo ni hatari sana katika ulimwengu wa vijana kwani yanachochea kasi ya kusambaa kwa mifumo ya utumwa mamboleo. Kutokana na utandawazi na mwingiliano mkubwa wa tamaduni, vijana wengi wamejikuta wakikosa utambulisho makini na matokeo yake wameanza kuwa ni watu wa kufuata mkumbuko wa tamaduni na maisha ya watu wengine hata kama hayana tija wala mashiko kwa ustawi na maendeleo endelevu ya vijana Barani Asia. Kutokana na umaskini na hali ngumu ya maisha, vijana wengi wamejikuta wakitumiwa na wanasiasa na baadhi ya viongozi wenye misimamo mikali ya kiimani na kidini kuchochea ghasia na mipasuko ya kijamii.

Vijana katika tamko lao wanakaza kusema, pamoja na mafanikio makubwa yanayoendelea kupatikana katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia, vijana wanataka kujikita katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Wanataka kuwa ni vyombo na mashuhuda wa haki, amani, maridhiano na huduma makini kwa jirani zao. Wanataka kuhakikisha kwamba, sauti yao kama vijana kutoka Barani Asia inasikika katika jamii, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Kanisa mahalia kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Wanataka kuwa ni waenezaji wa Injili ya Kristo Barani Asia kwa kutambua utajiri mkubwa wa tamaduni zilizoko humo. Dhamana hii inawezekana kabisa kwani wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu: karama na mapaji mbali mbali wanayoweza kuyatumia katika kukabiliana na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo.

Vijana wanasema, wanahamasika kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa majadiliano ya kidini na waamini wa dini mbali mbali kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi Barani Asia. Wanamshukuru Mwenyezi Mungu aliyewawezesha kushirikiana kwa karibu na vijana zaidi 100 kutoka katika dini ya Kiislam kwa ajili ya maadhimisho haya, hali inayoonesha kwamba, waamini wa dini mbali mbali wanaweza kuishi kwa amani, upendo na mshikamano, licha ya tofauti zao msingi za kiimani. Roho Mtakatifu amewawezesha vijana kuangalia imani yao kwa mwanga mpya zaidi.

Vijana wanahamasishana kushirikiana na kusaidiana katika maisha; wanawasihi viongozi wao wa kidini, wawe ni mifano bora ya kuigwa, ili kuweza kuwafunda katika tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni. Wanamwomba Roho Mtakatifu anawajalie imani, matumaini na mapendo thabiti; ili waweze kujizatiti katika kumpenda Mwenyezi Mungu pamoja na jirani zao, daima wakiendelea kujikita katika utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote! Changamoto zinazotolewa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote” zinapaswa kuvaliwa njuga na vijana wawe kweli ni mfano bora wa kuigwa!

Vijana wanatambua kwamba, wao ni jeuri ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake! Wanataka kuwa ni madaraja yanayowaunganisha vijana kutoka katika tamaduni mbali mbali Barani Asia; wanataka kuwa ni mashuhuda na vyombo vya umoja, amani, upendo, udugu na mshikamano; kwa kuheshimiana na kuthaminia! Wanatambua kwamba, tofauti zao msingi ni utajiri mkubwa katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vijana wanataka kutumia maendeleo ya sayansi na teknolojia katika mawasiliano ya jamii kwa kuwajibika zaidi, huku wakiwa na mwelekeo chanya unaotambua umuhimu na madhara ya matumizi vya vyombo vya mawasiliano ya jamii katika ulimwengu wa vijana! Njia hizi ziwasaidie vijana kushirikishana utamu na utajiri wa Maandiko Matakatifu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

09/08/2017 12:44