Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maendeleo

Tanzania: Kanisa ni mdau mkuu wa maendeleo na wala si mfanya biashara

Askofu mkuu Damiani D. Dallu: Kanisa ni mdau mkuu wa maendeleo na wala si mfanyabiashara! - EPA

09/08/2017 12:16

Mama Kanisa tangu mwanzo wa utume wake amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba, anaendeleza kazi ya ukombozi wa mtu mzima: kiroho na kimwili; kazi iliyofanywa na Kristo Yesu: kwa kuwaondolea watu dhambi zao; kwa kuwaponya magonjwa na shida zao za kimwili na hatimaye, kuwapatia mahitaji yao msingi. Aliguswa na mahangaiko ya watu: kiroho na kimwili; akatoa upendeleo wa pekee kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kwani maskini kwa kawaida ndio walengwa wa Habari Njema ya Wokovu.

Kanisa nchini Tanzania linaadhimisha Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji wa Tanzania Bara, yaani kuanzia mwaka 1868  na kilele cha maadhimisho haya ni Mwaka 2018. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji: furaha ya Injili”. Hiki ni kipindi cha kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa kazi kubwa iliyofanywa na wamisionari waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa kujikita katika uinjilishaji wa kina, uliogusa mahitaji msingi ya binadamu katika elimu, afya, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu!

Wamisionari hawakuja kama wafanyabiashara au wawekezaji, bali wadau wa maendeleo ya binadamu: kiroho na kimwili na ndiyo maana huduma hizi zilielekezwa zaidi kwa watu waliokuwa wanaishi vijijini. Huduma hizi zikatolewa kwa familia ya Mungu bila ubaguzi, dhamana inayoendelezwa na Mama Kanisa nchini Tanzania hata katika mapambazuko ya Millenia ya tatu ya Ukristo! Mwalimu Julius Kambarage Nyerere kwa kutaka kujenga na kuimarisha umoja na mshikamano wa watanzania wote, alitaifisha shule na hospitali zilizokuwa zinamilikiwa na Kanisa.

Viongozi wa Kanisa wakatambua nia njema aliyokuwa nayo Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya watanzania wote! Wakaaa kimya na wala hawakupiga makelele! Serikali ya Awamu ya Pili ilirejesha baadhi ya shule na hospitali zilizokuwa zimetaifishwa na Serikali mikononi mwa Kanisa na baadaye kuingia mkataba, ili wamisionari wasaidie mchakato wa maboresho ya huduma hizi msingi na serikali kutoa ruzuku katika maboresho haya kwani kimsingi mchakato wa huduma ni dhamana na wajibu wa serikali.

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa hivi karibuni na Askofu mkuu Damian D. Dallu wa Jimbo kuu la Songea, wakati wa kutoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Shemasi Jerome Mponzi, katika Parokia ya Nyakipambo, Jimbo Katoliki la Iringa. Anasikitika kusema kwamba, baada ya miaka 50 ya huduma, sadaka na majitoleo kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watanzania wote, mmisionari anafuatwa na kudaiwa kibali cha kufanya kazi nchini Tanzania na kutakiwa kulipa kodi na kusisitiza kua huku ni kumfanya mmisionari kuwa ni mfanyabishara, jambo ambalo si sahihi! Kanisa halina chama cha kisiasa, ingawa waamini wake ni wanachama wa vyama mbali mbali vya kisiasa nchini Tanzania. Kanisa anasema Askofu mkuu Dallu halihitaji upendeleo wa mtu, bali linachotakiwa ni kuhakikisha kwamba, sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa zinafuatwa. Kanisa limesajiliwa chini ya Wizara inayohusika, linafuata Katiba na Sheria.

Askofu mkuu Dallu amekumbushia kwamba, kunako tarehe 15 Mei 1891, Papa Leo XIII alichapisha Waraka wa Kitume, “Rerum Novarum” yaani “Mambo mapya”; msingi wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, unaokazia uhuru, ukweli, utii, hadhi na heshima ya binadamu mambo msingi katika mahusiano na mafungamano ya kijamii kuliko ukatili na jeuri! Askofu Mkuu Dallu anakaza kusema, kuna haja kwa Serikali ya Tanzania kuwekeza katika mfumo wa elimu makini unaojenga dhamiri nyofu, maadili na utu wema, ili kukuza na kudumisha: nidhamu, weledi, uadilifu na uwajibikaji.

Askofu mkuu Damian Dallu amevitaka vyama vya kitume nchini Tanzania na waamini katika ujumla wao, kuhakikisha kwamba, wanatumia karama na mapaji waliyokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na kamwe wasizibinafshe karama hizi kwani si mali yao! Matokeo yake ni kumweka Kristo Yesu pembeni na dharau kwa viongozi wa kiroho. Amewataka kuwa ni mashuhuda na vyombo vya kumtangaza Kristo Yesu: Kuhani, Mwalimu na Nabii. Watumie karama zao vyema ili kuwaponya wenye shida na mahangaiko mbali mbali na kamwe wasiligeuze Kanisa kuwa ni mahali pa biashara! Matokeo yake ni kuligeuza Kanisa kuwa ni la wagonjwa, mahali pa kuombewa tu, hali inayowafanya wagonjwa hawa kuwa ni watumwa wa mwombeaji au yule mwenye karama! Karama zisaidie kuimarisha imani kwa Kristo na Kanisa lake, na wala si kujitafutia umaarufu usiokuwa na tija!

Imehaririwa na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

09/08/2017 12:16