2017-08-07 14:53:00

Papa Francisko asikitishwa na shambulizi dhidi ya Wakristo Kanisani!


Baba Mtakatifu Francisko amesikitishwa sana na mauaji yaliyofanywa kwenye Kanisa la Mtakatifu Filipo, huko Ozubulu, Kusini mwa Nigeria, Jumapili tarehe 6 Agosti 2017, Kanisa lilipokuwa linaadhimisha Siku kuu ya Kung’ara Bwana na kupelekea watu 11 kufariki dunia na wengine 18 kujeruhiwa vibaya. Katika salam zake za rambi rambi zilizoandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu Hilary Paul Odili Okeke wa Jimbo Katoliki la Nnewi, anasema, anapenda kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliofariki dunia kutokana na shambulizi hilo ili waweze kupata raha ya milele na mwanga wa milele uweze kuwaangazia ili wapuzimke kwa amani.

Baba Mtakatifu anawaombea majeruhi ili waweze kupona haraka na kurejea tena kwenye shughuli zao! Kwa namna ya pekee, anazikumbuka familia zote zilizoguswa na kutikishwa na shambulizi hili na anawaombea wote faraja, amani na utulivu kutoka mbinguni! Itakumbukwa kwamba, tangu kikundi cha kigaidi cha Boko Haram kilipoanza mashambuli nchini Nigeria, kunako mwaka 2009, zaidi ya watu 20, 000 wamepoteza maisha na wengi wengi kujeruhiwa vibaya sana bila kusahau uharibifu mkubwa wa miundo mbinu na nyumba za ibada.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.