Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Maisha Ya Kanisa Afrika

Askofu mkuu Marek Solczyński, awasilisha hati za utambulisho Tanzania

Askofu mkuu Marek Solcynski, Balozi wa Vatican nchini Tanzania, amewasilisha hati zake za utambulisho kwa Rais John Pombe Magufuli wa Tanzania, tarehe 1 Agosti 2017. - AFP

07/08/2017 14:00

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli  tarehe 01 Agosti, 2017 amepokea hati za utambulisho wa Mabalozi watano walioteuliwa kuziwakilisha nchi zao Tanzania. Kati yao ni Askofu mkuu Marek Solcynski–Balozi wa Vatican nchini Tanzania. Itakumbukwa kwamba, Baba Mtakatifu Francisko alimteua, mwezi Aprili, 2017 Askofu mkuu Marek Solczyński kuwa Balozi mpya wa Vatican nchini Tanzania, baada ya Askofu mkuu Francisco Padilla kuhamishiwa nchini Kuwait pamoja na kuwa ni Mwakilishi wa Kitume wa Visiwa vya Kiarabu.

Kabla ya uteuzi huu, Askofu mkuu Marek Solczyński alikuwa ni Balozi wa Vatican nchini Georgia, Armenia na Azerbaijan. Askofu mkuu Marek Solczyński alizaliwa tarehe 7 Aprili 1961 huko Stawiszyn, nchini Poland. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 28 Mei 1987 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Baada ya kufanya utume wake katika masuala ya kidiplomasia ya Vatican sehemu mbali mbali za dunia na tarehe 26 Novemba 2011, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu na kumwekwa wakfu tarehe 6 Januari 2012. Askofu mkuu Marek Solczyński ameshiriki kikamilifu katika maandalizi ya hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Georgia, Armenia na Azerbaijan aliyoitekeleza kunako mwaka 2016.

Mabalozi wengine waliowasilisha hati zao za utambulisho ni;

Mhe. Nguyen Kim Doahn – Balozi wa Vietnam

Mhe. Prof. Ratlan Pardede – Balozi wa Indonesia

Mhe. Dkt. Detlef Wachter – Balozi wa Ujerumani

Mhe. Richard Tumisiime Kabonero – Balozi wa Uganda.

Akizungumza na Mabalozi hao Rais Magufuli amewapongeza kwa kuteuliwa kuziwakilisha nchi zao Tanzania na amewahakikishia kuwa Serikali ya Awamu ya Tano itaendeleza na kuimarisha zaidi uhusiano na ushirikiano wake na nchi hizo ambazo ni marafiki wa muda mrefu na washirika wa maendeleo wa Tanzania. Mhe. Rais Magufuli amewaomba Mabalozi hao kutilia mkazo diplomasia ya uchumi kwa kuongeza juhudi za kuhamasisha wafanyabiashara na wadau wengine wa maendeleo wa nchi hizo kushirikiana na Tanzania katika biashara na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ujenzi wa viwanda, kilimo na huduma za kijamii.

Kwa upande wao Mabalozi waliowasilisha hati zao za utambulisho wamemshukuru Mhe. Rais Magufuli kwa kuwapokea na wameahidi kuhakikisha uhusiano wa nchi zao na Tanzania unaendelezwa na kuimarishwa zaidi.

Wakati huo huo, Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Benedict Martin Mashiba kuwa Balozi wa Tanzania nchini Malawi. Mhe. Benedict Martin Mashiba anachukua nafasi ya Mhe. Victoria Richard Mwakasege ambaye amestaafu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

07/08/2017 14:00