2017-08-05 06:43:00

Utukufu na ukuu wa Mungu unaofumbatwa kwenye Fumbo la Msalaba!


Ndugu msikilizaji wa Radio Vatican ninakukaribisha katika tafakari ya Neno la Mungu Dominika hii ya kumi na nane ya Mwaka A. Masomo Matakatifu tutakayoyasikia leo hii yanatudhihirishia juu ya umungu wa Bwana wetu Yesu Kristu. Tunaalikwa sote tumfuate yeye nyuma yake ili atuongoze katika njia ya uzima wa milele, tupate nasi kuvishwa utukufu wake. Tafakari yetu inaongozwa na masomo matatu toka katika maandiko matakatifu. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha nabii Danieli Sura ya 7, aya ya 9 hadi ya 10 na aya ya 13 hadi ya 14. Somo la pili linatoka katika Waraka wa pili wa Mtume Petro kwa watu wote, Sura ya 1, aya ya 16 hadi ya 19 wakati somo la Injili linatoka katika Injili ya Mtakatifu Mathayo sura ya 17 aya ya 1 hadi ya 9. Kukuletea tafakari hii ni mimi Padre Walter Milandu wa Shirika la Wamissionari wa Damu Takatifu ya Yesu.

Mtakatifu Yohana katika Injili yake sura ya kwanza aya ya 11 anasema kwamba, Yesu alikuja kwa ajili ya walio wake wala walio wake hawakumpokea. Waisraeli walimsubiri Masia na Mkombozi kwa miaka mingi. Hata alipokuja kati yao, Masiha huyu hawakumtambua kwa sababu alikuja kwa staili ambayo hawakuitegemea kabisa. Yesu hakukidhi kabisa vigezo vya masiha waliyemtarajia. Walimtarajia Masiha anayekuja katika utukufu na nguvu, mtawala wa kisiasa na jemedari mwenye kuwaokoa Waisraeli kwa mkono wenye nguvu huku akiwashinda na kuwatiisha maadui wake.

Hakika Yesu mnyenyekevu na mpole, Yesu mwenye kuuchukua Msalaba na kukubali mateso na kisha kufa Msalabani hakuwaingia kabisa akili mwao kwamba yeye ndiye Masiha aliyetumwa kwao na Mungu. Hata wale ambao walikuwa karibu na Yesu kwa namna ya pekee, walisita kidogo kumtambua mara moja endapo yeye ndiye yule Masiha waliokuwa wakimsubiri. Kwa mfano, Yohane Mbatizaji akiwa gerezani aliwatuma wafuasi wake ili wamuulize Yesu kama kweli yeye ndiye Masiha au yawapasa wamsubiri mwingine. Ijapokuwa mitume wake walimtambua na kumpokea kama Masiha yule waliyekuwa wakimsubiri kila mara alipowaambia juu ya ukweli kwamba imempasa ateswe na kufa msalabani, walipata mashaka, hawakuwa tayari kukubali ukweli huu.

Agano la Kale na manabii linatupatia picha ya huyu Masiha kwamba atakuwa ni uzao wa Mwanamke, atatoka katika kabila la Yuda na ukoo wa Daudi, atazaliwa na Bikira na ataitwa Mwana wa Mungu. Masiha huyu atazaliwa Bethlehemu na atafanya utume wake Galilaya, atakuwa nabii Mkubwa mithili ya Musa, atakuwa mwanga wa mataifa yote, atatenda miujiza na atawachunga watu wa Mungu. Tunaelezwa zaidi kuwa huyu Masiha ni mpole na mnyenyekevu na ataingia Yerusalemu akiwa amepanda punda, anakataliwa na waashi lakini lakini yeye ndiye jiwe kuu la pembeni, atasalitiwa na rafiki yake, atatolewa sadaka kwa ajili ya dhambi za watu, atapigwa na kutemewa mate, atachomwa ubavuni kwa mkuki lakini hakuna mfupa wake hata mmoja utakaovunjwa. Kubwa zaidi ya yote atafufuka toka wafu, atapaa mbinguni na kukaa kuume kwa Mungu.

Ndugu mpendwa tukifuatilia kwa karibu zaidi maisha ya Yesu, maneno na matendo yake, hatutakuwa na sababu ya kuwa na mashaka kwamba Yesu ndiye yule Masiha aliyeahidiwa na Mungu na kutabiriwa na manabii. Huyu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu na Mkombozi wa Ulimwengu mzima. Yesu hakupenda kabisa kujifunua nafsi yake kwa nguvu na kwa miujiza. Hata alipotenda miujiza hakufanya kwa ajili yake binafsi bali kwa wale aliowahudumia. Alipenda watu wamtambue kutokana na mafundisho yake na matendo yake mema. Hata hivyo, Yesu alitambua ugumu wa watu kumtambua na kumkubali kuwa yeye ndiye Masiha mwana wa Mungu. Kwa faida ya mitume wake ambao hakutaka watetereke katika imani yao juu yake, aliamua kujifunua kwao. Anawachagua wachache tu ambao ni Petro, Yohana na Yakobo.

Mitume hawa watatu ndiyo ambao walimshuhudia siku chache zilizopita alipomfufua yule binti Yairo. Na ndiyo haohao ambao baada ya kuwaimarisha katika imani aliwateua waweze kuingia naye Getsemani, katika bustani ile ya mateso. Akiwa juu ya mlima Tabor pamoja na mitume hawa, Yesu akadhihirisha utukufu wake mbele yao, akageuka sura yake, mavaz yake yakawa meupe kama nuru. Hapa tuona jinsi utabiri wa nabii Danieli tuliousikia katika somo la kwanza jinsi ulivyokamilika, mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji na nywele za kichwa chake kama sufu safi. Mitume wanamuona Bwana wao akiongea na Musa na Elia kuonyesha ni jinsi gani ujio wa Yesu duniani unakamilisha yale yaliyoandikwa katika Agano la Kale na yale yote yaliyotabiriwa na manabii. Zaidi sana sauti ya Mungu mwenyewe inamdhihirisha Yesu ikisema, Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye. Sauti ya Mungu inamaliza kwa kusema, Msikilizeni yeye. Hii lilikuwa ni mara ya pili ambapo Mungu anamtambulisha Mwanaye wa pekee kwa watu. Mara ya kwanza ni wakati alipokuwa akibatizwa mtoni Yordani.

Ndugu mpendwa, tukio hili lina maana sana kwetu. Kwanza kabisa tunaimarishwa katika imani yetu na Mungu Baba mwenyewe anayetudhihilishia kwamba huyu tunayemfuata ndiye Mwana wake na Mkombozi wetu. Tusaidiwa zaidi kuamini hili kutokana na ushuhuda wa wenzetu, mitume waliokuwa mashahidi wakisikia na kuuona utukufu wa Mungu ndani ya Yesu Kristo. Hawa ndiyo mashahidi ambao kwa ajili yetu, Yesu aliwaimarisha katika imani yao ili wasitetereke. Tunamsikia leo Mtume Petro katika somo la pili akishuhudia ukweli huu akisema, Maana hatukufuata hadithi zilizotungwa kwa werevu, tulipowajulisha ninyi nguvu zake Bwana wetu Yesu Kristu na kuja kwake, bali tulikuwa tumeuona wenyewe ukuu wake. Bwana wetu Yesu Kristo anapogeuka sura na kung’aa kwa utukufu, anatukumbusha juu ya lengo la maisha yetu la kuufikia utukufu huko mbinguni. Ili kufanya hivyo lazima tukubali kugeuza maisha na miendendo yetu isiyofaa ili tumfuate yeye anayetufundisha namna ya kutimiza mapenzi ya Mungu. Siku za nyuma tuliona kwamba wajibu wa mfuasi pamoja na mambo mengine ni kumsikiliza mwalimu wake. Mienendo na maisha yetu haviwezi kubadilika endapo hatutakuwa tayari kumsikiliza Yesu kama ambavyo Mungu anatualika sote kufanya.

Yesu kwa kupitia mitume wake anatukumbusha suala moja muhimu sana kwamba, hakuna njia rahisi ya kuufikia utukufu bali kukubali kuichukua misalaba yetu. Mara kadhaa Bwana wetu anatuambia kuwa hatuwezi kuwa wafuasi wake endapo hatuko tayari kuichukua misalaba yetu na kumfuata kila siku. Mungu atujalie neema ili tukumbuke daima kuwa nyuma ya Msalaba kuna utukufu na hivyo tuwe tayari kuingia katika utukufu kwa kutimiza yale ambayo Mungu anataka tuyatende hata kama itabidi kutoa maisha yetu.

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.