2017-08-05 16:56:00

Tanzia: Kardinali Dionigi Tettamanzi amefariki dunia


Kardinali Dionigi Tettamanzi, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Milano, Italia, amefariki dunia, Jumamosi, tarehe 5 Agosti 2017 akiwa na umri wa miaka 83. Kwa sasa Baraza la Makardinali limebaki na jumla ya Makardinali 223 kati yao 121 wana haki ya kupiga na kupigiwa kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro na wengine 102 waliobaki hawana tena haki ya kupiga wala kupigiwa kura. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Dionigi Tettamanzi alizaliwa tarehe 14 Machi 1934, Jimbo kuu la Milano. Baada ya masomo na majiundo yake  ya Kipadre akapewa Daraja Takatifu ya Upadre hapo 28 Juni 1957.

Baadaye alipelekwa kujiendeleza kwenye Chuo kikuu cha Kipapa cha Gregorian na kujipatia Shahada ya uzamivu katika taalimungu. Kwa muda wa miaka 20 alifundisha taalimungu maadili sehemu mbali mbali za Italia. Katika kipindi hiki akajipambanua kuwa mwandishi mahiri sana wa vitabu kuhusu masuala Injili ya uhai, familia, kanuni maadili na utu wema. Ni kiongozi aliyechangia sana katika mchakato wa shughuli za kichungaji ndani na nje ya Italia.Alikuwa ni kiungo muhimu sana kati ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na Vatican kuhusu masuala ya Injili ya familia.

Tarehe 1 Julai 1989 akateuliwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Ancona-Osimo na kuwekwa wakfu kuwa Askofu mkuu tarehe 23 Septemba 1989. Aliwahi pia kuwa Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Tarehe 20 Aprili 1995 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu Genova. Alibahatika pia kuwa Makamu wa Rais, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia. Ameshiriki katika maadhimisho mbali mbali ya Sinodi za Maaskofu hapa mjini Roma. Alibahatika kuwa kiongozi mkuu wa Jimbo kuu la Milano kuanzia tarehe 11 Julai 2002 hadi tarehe 28 Juni 2011 alipong’atuka kutoka madarakani. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Kardinali tarehe 21 Februari 1998.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.