2017-08-05 17:17:00

Majadiliano ya kidini ni shule ya utu na ni chombo cha umoja na amani


Waamini wa dini mbali mbali duniani wanapaswa kukita maisha yao katika sala na majadiliano ya kidini yanayosimikwa katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja; kwa kushikamana katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kama njia sahihi ya kujibu kilio na mahangaiko ya watu wa nyakati hizi. Ni wajibu wa waamini kujizatiti kupambana kufa na kupona dhidi ya vitendo vya kigaidi na misimamo mikali ya kiimani na kidini; ili kujenga na kudumisha utamaduni wa haki, amani na maridhiano kati ya watu!

Hii ni changamoto ambayo imetolewa na Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini, tarehe 3 Agosti 2017 wakati wa uzinduzi wa kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 30 tangu waamini wa dini mbali mbali nchini Japan, walipokusanyika kwenye Mlima wa Hiei, Kyoto, nchini Japan kwa ajili ya kusali ili kuombea amani duniani. Maadhimisho haya yamezinduliwa na Kardinali John Tong Hon, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Hong Kong ndiye aliyesoma na hatimaye, kuwasilisha Barua ya Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya, aliyekazia kwa namna ya pekee kuhusu: Uhusiano wa upendo, haki na mshikamano wa kidugu; mambo msingi katika Barua aliyomwandikia Mheshimiwa Koei Morikawa, Kuhani mkuu wa Madhehebu ya Kibudha.

Ujumbe wa Vatican katika maadhimisho haya unawajumuisha Askofu mkuu Joseph Chennot na Monsinyo Janakaratne Kodithuwakku Kankanamalarge, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini. Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot anasema, majadiliano ya kidini ni hitaji muhimu sana kwa wakati huu ili kuweza kujizatiti katika kupambana na vitendo vya kigaidi,misimamo mikali ya kidini na kiimani, ili hatimaye, kujenga na kudumisha haki, amani na maridhiano kati ya watu. Kila dini duniani ina tunu msingi za maisha zinazopawa kukuzwa na kudumisha na wengi: Tunu hizi ni: haki, amani, udugu, ustawi na maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili.

Tunu hizi msingi zinaboreshwa kwa njia ya urafiki na mshikamano wa kidugu; ili kusimama kidete, kulinda, kutetea na kudumisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Majadiliano ya kidini ni muhimu sana ili kukabiliana na mambo yote yanayotishia amani, usalama na mafungamano ya kijamii duniani. Ikumbukwe kwamba, vita na ghasia ni mambo ambayo ni kinyume kabisa cha tunu msingi za maisha ya kiroho sanjari na kanuni maadili. Ni dhamana na jukumu la viongozi wa kidini kushuhudia tunu hizi katika maisha na vipaumbele vyao, kwani amani ni dhamana inayowawajibisha watu wote wenye mapenzi mema sehemu mbali mbali za dunia. Kumbe, majadiliano ya kidini ni muhimu katika mchakato wa maboresho ya tunu msingi za maisha ya kiroho anasema  Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot.

Ni wajibu wa viongozi wa kidini kupembua kwa kina na mapana sababu zinazopelekea vita, ghasia na mipasuko ya kidini, ili kuwafundisha waamini wao pamoja na watu wote wenye mapenzi mema umuhimu wa kulinda na kudumisha amani duniani kama kikolezo cha maendeleo endelevu. Waamini wasimame kidete kupambana na maovu pamoja na ubaya wa dhambi, kwa toba na wongofu wa ndani; kwa kupenda na kusamehe; kwa kuishi kwa amani na mshikamano. Lakini, ikumbukwe kwamba, haki na amani ni sawa na “uji kwa mgonjwa”.

Kumbe, haki, amani, msamaha na upatanisho wa kweli ni mambo msingi katika kudumisha utulivu na mafungamano ya kijami. Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kufahamiana, kuheshimiana na kuthaminiana licha ya tofauti zao msingi. Majadiliano ya kidini ni shule hai y autu, ni chombo cha umoja na mshikamano wa kidugu na ni msingi wa jamii inayosimikwa katika heshima na urafiki. Viongozi wa kidini hawana silaha, lakini wamebahatika kuwa ni watu wa sala na vyombo vya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha. Waamini wanapaswa kuendeleza majadiliano ya kidini kwa njia ya sala ili kukuza na kudumisha ”Moyo wa Assisi” chachu muhimu sana katika ujenzi wa amani duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.