2017-08-04 16:03:00

Waamini mnaitwa kuwa mashuhuda wa utukufu na ukuu wa Mungu!


Leo kanisa latualika kusherehekea sherehe ya kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo. Kwanza ya yote twaweza kujiuliza tendo hili lilikuwa na maana gani kwa wale wafuasi watatu walioshuhudia? Inaonekana kuwa mpaka wakati wa tukio hilo walikuwa wamemwona Yesu katika hali ya nje, mtu ambaye ni sawa na wao, na walimfahamu fika kwa vile waliishi naye. Sasa wanapata kumfahamu Yesu mwingine, Yesu halisi, ambaye haonekani kwa macho ya kila siku ya mwanadamu au katika mwanga wa kawaida wa jua ila katika hali ya ufunuo, ya mbadiliko, ya zawadi.

Tunaona kuwa ili hali hii itokee, kama kwa wale mitume mlimani Tabor, ni lazima maisha yetu yaguswe na kubadilika. Padre Cantalamessa anatumia mfano wa watu wawili waliopendana, mwanamke na mwanamme. Mmoja ambaye kabla alikuwa kati ya wengi au pengine hakujulikana, mara moja anapata kitu kipya. Vitu vingine vyote vinapoteza thamani isipokuwa huyo aliyependwa. Hakuna tena kingine chenye thamani zaidi ya huyo mpendwa mpya. Hapa hutokea mng’aro mpya wa sura, yaani kitu kipya kinaonekana kwa namna ya pekee hata kama kilikuwepo kati au katika mazingira ya kila siku. Anayependwa anaonekana katika mwanga mpya na kila kitu kinaonekana kizuri, kipya na kasoro hazionekani. Mapendo ya kweli huzalisha uvumilivu. Kwa kifupi kama asemavyo mwanamashairi Ovid “kila mmoja anavutwa na mvuto wenyewe”. Kwa hakika upendo wa kweli unabadilisha maisha ya mtu kabisa. Mtu aweza kusema urafiki kati ya watu ni kitu kinachoshikika, kuonekana. Ila kwa Yesu yahitajika jicho lingine,  la kimoyo, la kiimani zaidi. Angalia ule ushuhuda wa ufufuko – amefufuka kweli, ni mzima.

Ndugu zangu, twaona kuwa katika injili sababu ya Yesu kwenda mlimani ni kwenda kusali. Hapa tunaona nguvu ya sala. Katika hali yake ya kibinadamu anasali akimuomba Baba yake. Hii sala ya Yesu inatufikirisha sana katika fumbo lake kama mtu. Yesu anaposali anamwita Mungu Baba, Abba, yaani Baba Mpendwa na hii inaonesha uhusiano wa karibu aliokuwa nao na Baba.  Hii sala ya Yesu iko wazi katika Mt. 11:26-27 – Ndivyo, Baba, ilivyokupendeza. Nimekabidhiwa yote na Baba yangu, hakuna amjuaye Mwana, ila Baba. Wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana na ye yote ambaye Mwana apenda kumfunulia.

Sala hii huonesha wazi kuwa kati ya Baba na Mwana kuna uhusiano mkubwa sana. Yeye ni mwaminifu sana kwa Baba. Ni tofauti kabisa na mfano wa shamba la mizabibu na wakulima – ile habari ya wakulima wasio waaminifu – Mk. 12:1-10. Wale wakulima hawakuwa waaminifu. Uhusiano wa Yesu na Baba ni tofauti kabisa.

Tunaona pia katika maisha yake, Yesu hakujiita Mwana wa Mungu bali Mwana wa Mtu. Kwa nini? Na pia hakujiita Masiya. Kwa nini? Alithibitisha tu kuwa masiya mbele ya kuhani mkuu alipokuwa akijibu swali lake – je wewe ni masiya? Tunaona hili katika Mk. 14:61. Yesu alikataa vyeo hivi. Watu walifahamu vizuri maana ya sifa hizi. Wengi waliitwa wafalme, watu wakubwa n.k na walimfahamu masiya kama mkombozi lakini mpiganaji atakayepigana dhidi ya adui wa Israeli. Yesu alitambua mawazo yao na ndiyo maana hakupenda sifa hizi au vyeo hivi. Hata wafuasi wake hawakuelewa hili na ndiyo maana walikuwa bado na wazo la ufalme wa utukufu na nguvu. Mwisho wa maisha yake hapa duniani tunamwona Yesu akiteseka na kufa. Lakini pia akifufuka na tunaona kuwa mitume na wafuasi walielewa vizuri maana ya uwepo na mafundisho yake baada ya ufufuko. Angalia ule ushuhuda wa ufufuko – amefufuka kweli, ni mzima.

Hata hivyo kung’ara sura kunabaki fumbo kwetu. Mtume Paulo anasema, Bwana Yesu aling’arisha miili yetu na kuifananisha na mwili wake. Mlima Tabor unasimama kama dirisha wazi na kwamba miili yetu ya giza itang’ara siku moja katika mwanga. Kwa hivyo kwa tendo hili twaona kwamba pamoja na hali duni ya miili yetu bado Mwenyezi Mungu anatupatia nafasi ya kubadilika. Na hapa Roho Mtakatifu anapata nafasi kubwa ya kututakatifuza sisi wanadamu.

Kadiri ya Biblia, mwili ni sehemu muhimu kwa mwanadamu. Mtu ni mwili pia. Mwili uliumbwa na Mungu, ukamwilishwa na kutakatifuzwa na Roho Mtakatifu katika ubatizo. Mtu wa biblia ametawazwa na utukufu huu wa kimwili. Katika Zab. 139:13 ..  tunasoma haya; maana wewe umeuumba mtima wangu, umeniunga tumboni mwa mama yangu. Ninakusifu kwa kuwa nimefanywa kwa namna ya ajabu ya kutisha. Mwili na roho vitakuwa na utukufu sawa. Mtu mmoja Charles Pequy anasema, siku ya mwisho, mwili na roho; au itakuwa mikono miwili iliyofungwa pamoja katika utukufu au viganja viwili vilivyofungwa pamoja utumwani.

Ndugu zangu, ukristo au niseme kuwa kanisa katoliki linafundisha wokovu wa mwili na si wokovu toka mwili kama walivyofundisha wafuasi wa mafundisho potofu kama Manicheans na Gnostics au baadhi ya dini nyingine au hata baadhi ya madhehebu ya wakati wetu huu. Wao huongea tu kuhusu roho na kudharau mwili. Sisi tunatafuta wokovu wa mwili na roho na si wokovu wa roho tu. Na kung’ara sura Yesu ni dhihirisho wazi la hilo. Thamani ya tendo hili ni kwamba miili yetu iliyoharibika itang’arishwa katika utukufu wake Bwana. Hii ndiyo maana na heshima kubwa ya sherehe hii ya leo. Mwenyezi Mungu anampatia daima mwanadamu nafasi ya kumwona vizuri zaidi. Na katika kumwona Mungu, mwanadamu anapata uzima mpya. Mt. Ireneo anasema, uzima wa kweli wa mtu uu katika kumwona Mungu. Sherehe ya Kung’ara sura Bwana inathibitisha hilo. Nawatakia sherehe njema.

Tumsifu Yesu Kristo,

Pd. Reginald Mrosso, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.