2017-08-04 15:44:00

Vijana ni jeuri na matumaini ya Kanisa na Jamii katika ujumla wake!


Maadhimisho ya Siku ya Saba ya Vijana Barani Asia kwa Mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “Furaha ya vijana wa Bara la Asia: Kuishi Injili katika wingi wa makabila ya Bara la Asia”. Hiki kimekuwa ni kipindi cha kutafakari kuhusu umoja na mshikamano wa vijana Barani Asia kutoka katika makabila mbali mbali. Wameadhimisha kwa kutambua na kuthamini tofauti zao ambao ni utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa miongoni mwa familia ya Mungu Barani Asia.

Vijana wa kizazi kipya, wanatambua kwamba, wao ni wamoja katika utofauti zao wa mambo msingi ya maisha; lakini maadhimisho ya Siku ya Saba ya Vijana Barani Asia ni fursa ya kusherehekea umoja wao; kwa kuishi na kushirikishana ile furaha ya Injili, kama anavyokaza kusema Baba Mtakatifu Francisko! Haya ndiyo mambo msingi ambayo yamekuwa yakichambuliwa kwa kina na mapana wakati wa katekesi, ibada na liturujia mbali mbali huko mjini Yogyakarta, nchini Indonesia. Maadhimisho haya yamejikita zaidi katika Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, ili kuwapatia vijana nafasi ya kuzungumzana na Kristo Yesu kutokana katika undani wa maisha yao! Hata katika wingi wao huo, lakini bado kumekuwepo na ukimya, sala na tafakari ya kina!

Vijana wanaendelea kushirikishana furaha, matumaini, changamoto na wasi wasi za maisha ya ujana wao. Ni kipindi cha kujenga na kuimarisha urafiki kati ya wajumbe kutoka sehemu mbali mbali Barani Asia. Maadhimisho haya  yamekuwa ni nafasi kubwa kwa vijana kutoka Barani Asia, kujisikia nyumbani na kusaidiana na vijana wenzao kutoka Indonesia, ambao, wengi wao ni waamini wa dini ya Kiislam. Wamegundua umuhimu wa kushirikiana na kushikamana kama ndugu, licha ya tofauti zao za kidini, mambo msingi katika mchakato wa majadiliano ya kidini. Vijana hawa wamekuwa wakitembelea maeneo mbali mbali mjini humo ili kushuhudia furaha ya Injili, imani na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Hii kimsingi ndiyo “Furaha ya vijana wa Bara la Asia: Kuishi Injili katika wingi wa makabila ya Bara la Asia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.