2017-08-04 08:49:00

Utukufu, ukuu na uweza wa Mungu unang'ara katika Fumbo la Msalaba


Kanisa linaadhimisha Siku kuu ya kung’ara sura Bwana wetu Yesu Kristo. Hii ni Sikukuu ambayo huadhimishwa kila mwaka ifikapo terehe 06 Agosti. Mwaka huu terehe hiyo imeangukia siku ya Dominika ya 18 ya Mwaka A na hivyo kuipeleka tafakari yetu katika Utukufu wa Mungu ambao ndiyo ukamilifu tunao uchuchumilia katika maisha yetu ya kila siku katika imani. Mungu wetu ni Mtakatifu. Utukufu ni sifa yake mahsusi kwa kuwa humfanya kuwa mweupe kabisa bila doa lolote na ni Yeye pekee ndiye mwenye kung’aa na mwenye utakatifu wa kweli.

Kristo Bwana wetu, Mwanaye wa pekee anatufunulia utukufu huo. Ni utukufu ambao anao tangu asili ingawa aliuficha kwa ajili ya tendo lake la upendo la kutukomboa sisi wanadamu (Rej Fil 2:6 – 8). Lakini zaidi kwa kuungana na ubinadamu wetu anatufunulia kwamba hata sisi nasi tunapaswa kung’aa hivyo hivyo kwani tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Anatukumbusha kwamba Mwanadamu katika asili yake ameumbwa kwa mfano wa Mungu na katika hali ya utakatifu. Hivyo utakatifu ni wito wetu wa asili.

Neno la Mungu hasa Injili ya Dominika hii inatusimulia tukio hilo. Sehemu hii ya Injili inatanguliwa na matukio mawili ambayo ni muhimu kuyatupia macho ili kupata maana pana ya adhimisho la leo.  Baada ya Kristo kuwatahadharisha mitume wake kuwa makini na chachu ya Mafarisayo na Masadukayo aliithibitisha haiba yake kuwa Yeye ni Kristo Mwana wa Mungu aliye hai. Uthibitisho huo ambao tunauona katika kiri imani ya Mtume Petro kwa niaba ya wengine wote iliunganishwa na kinachoambatana na hadhi yake hiyo yaani njia ya mateso au kwamba Yeye ni Masiha, Mwana wa Mungu ambaye atakataliwa kwa sababu ya ukweli lakini katika ukweli huo ndipo atausimika ufalme wa Mungu na katika ukweli huo ndipo atang’aa.

Hapa ndipo linafuatia tukio la leo ambalo kwalo Mitume wanasikia sauti inayosikika kutoka mbinguni kwamba: “Huyu ni Mwanangu, mpendwa wangu, ninayependezwa naye; msikieni yeye” inakuwa ni uthibitisho wa unasaba wa Kristo kwamba ni Mwana wa Mungu na hivyo kuipa nguvu hoja yake na njia yake anayoipendekeza kufikia wokovu wetu sisi wanadamu. Asili ya Kristo inawekwa wazi mbele yetu kwamba ni Mwana wa Mungu. Lakini Kristo Mwana wa Mungu ameungana na ubinadamu wetu na kujitambulisha katika asili mbili zinazoungana kwa njia ya fumbo. Umungu na ubinadamu unaungana katika namna ya ajabu nasi daima tunakiri kuwa ni Mungu kweli na ni mtu kweli.

Tukienda hatua moja zaidi tunamwona Kristo mzima ambaye anaonekana katika hali ya utukufu. Yeye ambaye yu katika asili ya kimungu na kibinadamu kwelikweli ndiye anang’aa sura na mavazi yake kuwa meupe pe kuliko hata theluji. Katika fumbo la Kristo hatuzioni hali hizi zikitenganishwa. Kuunganishwa kwa umunugu na ubinadamu katika nafsi yake imekuwa ni daraja la kutuunganisha tena na Mungu. Huu ni uthibitisho wa utajiri ambao ubinadamu wetu unarudishiwa kwa fumbo la Kristo, utajiri ambao tuliupoteza kwa sababu ya dhambi. Mwanadamu katika hali ya utakatifu anang’aa kama Kristo. Hivyo katika Kristo yaani katika uhalisia wake mwanadamu anabaki kuwa katika hali ya utukufu mithili ya Kristo mlimani Tabor.

Tukiyatafakari matukio machache pale juu mlimani tunajifunza kitu cha kufanyia kazi tunapoadhimisha sikukuu hii. Tujumuishe yote katika hamu ya Mtume Petro kutaka kubaki katika hali ile daima na katazo la Kristo la kutowaambia wengine hadi baada ya ufufuko wake. Mshangao wa Petro unadhihirisha kwamba hali iliyokuwepo pale juu mlimani ilikuwa ni nzuri ajabu. Hapa anatamani kuendelea kuishuhudia hali hiyo na kutokurudi chini ndiyo maana akamwambia Bwana “ni vizuri sisi kuwapo hapa; nitafanya vibanda vitatu, kimoja chako wewe, na kimoja cha Musa, na kimoja cha Eliya”. Pengine Petro alibakia katika kuushangilia utukufu wa mwingine na kutaka kubakia hivyo bila kujijali mwenyewe au aliifurahia hali hiyo ambayo amefikishwa bila kutarajia.

Utukufu si suala la kupelekwa na kujikuta tayari umefika bali unapaswa kuhangaikiwa. Ndiyo maana baada ya kuonesha hamu yake hiyo sauti itokayo katika wingu ilielekeza kumsikiliza Kristo: “msikieni Yeye”. Ni kweli hali hiyo ni nzuri na inapendeza lakini ili kuifikia hali hiyo si kwa kubebwa tu bali ni kwa kulisikiliza Neno la Kristo. Huyu ambaye ni mwanangu mpendwa ninayependezwa naye atawaonesha njia ya kuufikia utukufu huu. Zaidi kitendo cha Kristo kushuka nao toka mlimani na kuwarudisha katika maisha ya kawaida kiliwaelekeza mazingira ambayo walipaswa kumsikiliza Kristo, kutimiza neno lake na hivyo kuingia katika utakatifu ni katika maisha ya ulimwengu huu, ni katika ushuhuda wa maisha.

Utukufu ni ushindi baada ya kupita katika ulimwengu huu. Si suala la kubaki tu juu mlimani katika utukufu bali kuutafuta utukufu huo katika maisha ya kila siku. Baada ya kuuonja utukufu huo, yaani kuuelewa shuka katika jamii, uthibitishe utukufu huo. Huu ni wito wa kimisionari ambao unatudai kushirikishana utukufu wa Mungu. Maisha yetu ya uaminifu katika neno la Kristo yatatufikisha hadi mwisho tukiwa tumebaki katika utukufu huo.  Njia ambayo Kristo anatuelekeza ni njia ya msalaba. Yeye aliipitia njia hiyo, akabaki mwaminifu katika neno la Mungu na hatimaye “Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina… na kila ulimi ukiri ya kuwa Yesu Kristo ni Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba” (Fil 2:9,11).

Ni vema basi kutafakari kwa ufupi ni kwa namna gani katika msalaba kuna utukufu. Utukufu wa Mungu unapatikana katika kumfanya Yeye atamalaki na hivyo katika kuyatimiza mapenzi ya Mungu ndipo tunapomtamalakisha na utukufu wake kung’aa kwetu. Fumbo la msalaba wa Kristo ni namna ya juu kabisa tunayofundishwa na Kristo katika kuyatimiza mapenzi ya Mungu. Ni fumbo ambalo linatuonesha kuwa tangu mwanzo wa maisha yake Kristo ameungana na Mungu na hivyo matendo yake yote yanarandana na mapenzi yake Mungu. Hivyo kwetu sisi tunapaswa kuipitia njia hiyo kwani kwake Yeye ndipo tunapata asili yetu na kwake Yeye ndipo tunaelekea.

Kutimiza mapenzi ya Mungu kunaunganishwa na msalaba sababu ya ukinzani wa hali yetu ya kimwili ambayo inarahisisha na kuweka uovu wote kuwa kama kitu kitamu au kizuri na cha kuvutia. Tunapewa fumbo la msalaba kama kielelezo ili kuthibitisha utayari wa kuziacha hali hizo zinazotuvutia dhambini hata kama tutapitia katika mateso hadi kufa. Na hapa tuanaambiwa kuwa kifo chetu hicho ni cha mwili tu lakini roho zetu zitaendelea kuwa hai na tutang’aa mbele ya Mungu. Mtume Petro anatuambia katika somo la pili kwamba Neno hilo la Mungu linatujia kama neno la unabii ambao daima lilikumbusha kuifuata njia ya Mungu. Tuiombe neema ya Mungu kusudi nasi tuuchuchumilie utukufu huo kwa kujilinganisha maisha yetu na Kristo aliye kichwa chetu. Yeye ametupatia njia ambayo ni njia ya msalaba. Tuipitie njia hiyo kusudi kuyatimiza mapenzi ya Mungu ili mwishoni tung’ae katika utukufu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.