2017-08-04 15:00:00

Dini zina wajibu wa kudumisha amani, udugu na mshikamano kati ya watu


Waamini wa dini mbali mbali hawana budi kusali kwa ajili ya kuombea amani na kushirikiana kwa karibu zaidi kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Leo hii kuna vita, kinzani na mipasuko ya kijamii sehemu mbali mbali za dunia inayosababishwa hata na vitendo vya kigaidi vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu! Uhusiano wa upendo, haki na mshikamano wa kidugu ndiyo mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha kwanza na Baba Mtakatifu Francisko katika Barua aliyomwandikia Mheshimiwa Koei Morikawa, Kuhani mkuu wa Madhehebu ya Kibudha, kama sehemu ya kumbu kumbu ya maadhimisho ya Miaka 30 tangu waamini wa dini mbali mbali nchini Japan, walipokusanyika kwenye Mlima wa Hiei, Kyoto, nchini Japan kwa ajili ya kusali ili kuombea amani duniani.

Maadhimisho haya yamezinduliwa tarehe 3 Agosti 2017 na Kardinali John Tong Hon, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Hong Kong ndiye aliyesoma na hatimaye, kuwasilisha Barua ya Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho haya! Ujumbe wa Vatican katika maadhimisho haya unawajumuisha Askofu mkuu Joseph Chennot, Balozi wa Vatican nchini Japan, Askofu Miguel Angel Ayuso, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini pamoja na Monsinyo Janakaratne Kodithuwakku Kankanamalarge, Katibu mkuu msaidizi wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini.

Katika barua hii, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuwahakikishia viongozi wa dini ya Kibudha uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na maisha ya kiroho, wanaposhirikiana kusali kwa ajili ya kuombea amani, usalama na maridhiano kati ya watu wa Mataifa, hususan maeneo ambayo yamekumbwa na vita pamoja na mipasuko ya kijamii. Tukio hili la kidini linalofanyika kila mwaka linasaidia kwa kiasi kikubwa ujenzi wa ari na moyo wa majadiliano ya kidini miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali ili kushirikiana na kushikamana katika kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya amani na utulivu kwa ajili ya familia ya binadamu.

Baba Mtakatifu anasema, sala ni nguvu kuu inayoenzi mchakato mzima wa amani, kwa kuheshimiana na kuthaminiana; mambo yanayo imarisha kifungo cha upendo na kuendelea kuwahamasisha waamini wa dini hiziĀ  kujenga na kudumisha mafungamano ya haki na mshikamano wa kidugu. Ulimwengu mamboleo umesambaratika kutokana na makovu ya vita, ghasia, vitendo vya kigaidi pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayotishia mazingira, nyumba ya wote. Ushuhuda wa sala ya pamoja na mshikamano wa upendo ni ujumbe makini kwa familia ya Mungu duniani.

Kama waamini, anasema Baba Mtakatifu, wanatambua fika kwamba, kuna uwezekano wa kuwa na amani ya kudumu, kwani hakuna jambo lolote lisolowezekana mbele ya Mwenyezi Mungu. Hii ni dhana ambayo Baba Mtakatifu Francisko alikuwa ameifafanua kunako tarehe 20 Septemba 2016 wakati viongozi wakuu wa dini walipokutana tena mjini Assisi kwa ajili ya kuombea amani duniani. Itakumbukwa kwamba, dhana ya kuwa na Siku ya Kuombea Amani Duniani, ilianzishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 27 Oktoba 1986. Huo ukawa ni mwanzo kwa waamini wa dini ya Kibudha kutoka Japan kuanzisha Siku ya Kuombea Amani nchini Japan, inayofanyika kwenye Mlima Mtakatifu wa Mabudha Hiei, nchini Japan.

Mheshimiwa Etai Yamada, Kiongozi wa dini ya Kibudha nchini Japan, mwenye umri wa miaka 80 anasema, alishangazwa sana na mambo yaliyojiri wakati wa maadhimisho ya Siku ya Kuombea Amani Duniani. Tarehe 6 Agosti ya kila mwaka, ni kumbu kumbu muhimu sana nchini Japan, wanapokumbuka, siku ile Mji wa Hiroshima uliposhambuliwa kwa mabomu ya nyuklia, madhara ambayo yanaendelea kujitokeza hata wakati huu. Baba Mtakatifu Francisko anahitimisha Barua yake kwa kusema kwamba, ataendelea kushikamana pamoja nao katika sala kwa ajili ya kuombea amani duniani pamoja na baraka na neema kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ili ziweze kuwashukia na kukaa pamoja nao daima!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.