2017-08-03 16:21:00

Vijana wawasha moto wa Injili Barani Asia!


Maadhimisho ya Siku ya Saba ya Vijana Barani Asia kwa Mwaka 2017 yanaongozwa na kauli mbiu “Furaha ya vijana wa Bara la Asia: Kuishi Injili katika wingi wa makabila ya Bara la Asia”. Maadhimisho haya yamefunguliwa rasmi, Jumapili tarehe 30 Julai 2017 na yatafungwa kwa kishindo tarehe 6 Agosti 2017, wakati Mama Kanisa atakapokuwa anaadhimisha Sherehe ya Kung’ara kwa Bwana, inayopania kuwaimarisha mitume, ili kuweza kukabiliana na Kashfa ya Fumbo la Msalaba!

Tarehe 2 - 6 Agosti 2017 vijana wote wamekusanyika Jimboni Yogyakarta kwa uzinduzi rasmi  ili hatimaye, kuendelea na Katekesi, Sala, Liturujia na Ibada ya Misa Takatifu.  Hili ni tukio linalowajumuisha vijana 2, 140 kutoka katika mataifa 22 yaliyoko Barani Asia bila kusahau idadi kubwa ya wakleri na watawa wanaosindikizana na vijana hawa katika maadhimisho haya! Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya ufunguzi, imeadhimishwa na Kardinali Patrick Rosario, Mwenyekiti wa Tume ya Vijana, Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia.  Vijana wamekumbushwa kwamba wao ni jeuri na matumaini ya Kanisa kwa sasa na kwa siku zijazo! Vijana wanapaswa kujengewa utamaduni unaoheshimu na kudumisha Injili ya uhai dhidi utamaduni wa kifo; Injili ya imani, matumaini na mapendo; dhidi ya hali ya kukata na kujikatia tamaa inayopelekea vijana wengi kukumbwa na ugonjwa wa sonona. Vijana lazima waendelee kujikita katika shule ya malezi ya imani na tunu msingi za maisha bora zinazosimikwa katika utu na heshima ya binadamu.

Vijana wamekuwa ni mashuhuda na vyombo vya haki, amani na maridhiano kati ya watu, changamoto kwa watu kuendelea kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kusimama kidete kulinda na kutetea utu na heshima ya binadamu. Vijana wanaendelea kushuhudia furaha inayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake anasema Askofu Robertus Rubyatamoko, mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya maadhimisho haya. Vijana wanaendelea kuadhimisha na kushuhudia furaha ya Injili kwa amani na utulivu, jambo ambalo limenogesha mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene nchini Indonesia, mahali ambapo kuna idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam. Serikali pia imekuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa kuchangia kwa hali na mali ili kufanikisha tukio hili la kihistoria.

Askofu Ignatius Suharyo, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Indonesia anasema, kimsingi Indonesia ni nchi ya amani, lakini misimamo mikali ya kidini na kiimani inatishia misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Vijana wengi wamepatiwa hifadhi kwenye familia mbali mbali, kielelezo cha upendo na ukarimu wa watu wa Mungu nchini Indonesia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.