Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Tafakari \ Makala

Mapambano dhidi ya saratani ya rushwa na ufisadi duniani!

Kikundi cha Washauri wa Kimataifa kuhusu Haki kwenye Baraza la Kipapa la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu kinapania kuanzisha kampeni dhidi ya rushwa na ufisadi sehemu mbali mbali za dunia. - REUTERS

03/08/2017 15:31

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu hivi karibuni lilifanya kongamano la kimataifa kuhusu rushwa na malengo ya kongamano hili kutoka kwa washauri wa kimataifa mintarafu haki msingi za binadamu, rushwa na magenge ya kihalifu kimataifa yamechapishwa kama changamoto kwa waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kukataa kishawishi cha kuandamwa na hatimaye, kumezwa na rushwa pamoja na ufisadi. Nia ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwezi Februari 2018 ni kutaka kuwaombea waamini kushinda kishawishi cha rushwa na kama sehemu ya kumbu kumbu endelevu tangu alipouwawa kikatili Mwenyeheri Padre Giuseppe Puglisi.

Kuanzia Mwezi Septemba, 2017 Kikundi cha Washauri wa Kimataifa kuhusu haki katika Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu litaanza kupembua kwa kina na mapana kuhusu kongamano la kimataifa kuhusu rushwa na mifumo yake mbali mbali inayofumbatwa pia katika magenge ya kihalifu. Rushwa ni hali kabla ya kumwilishwa na kuwa ni tendo. Kumbe, inahitaji utamaduni; elimu na malezi; utekelezaji makini unaofanywa na taasisi pamoja na ushiriki wa wananchi katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi.

Kikundi hiki kitajitahidi kutoa maana mbali mbali za rushwa ili kuwajengea watu uwezo wa kupambana na saratani ya rushwa pamoja na kuunda mtandao wa kimataifa, chini ya mwamvuli wa Kanisa. Lengo kuu la mtandao huu, ni kuwajengea watu ujasiri kwa kuwapatia mapendekezo; kuwaonesha umuhimu wa kuzingatia ukweli na uwazi; kujenga na kudumisha ari, moyo, ushirikiano kwa kukazia kipaji cha ubunifu. Kwa watu wanaotaka kupata upendeleo na mafanikio kwa njia ya mkato ni hatari na matokeo yake ni kwenda kinyume cha sheria za nchi na kanuni maadili. Ni hatari kwa viongozi kutumia madaraka na nafasi zao za kazi kwa ajili ya kujitajirisha kwani mambo haya yanakwenda kinyume cha tunu msingi na uaminifu kazini.

Kikundi cha Washauri wa Kimataifa kitajikita katika kutoa elimu na malezi makini ili kuwawezesha watu kujenga dhana ya uhuru na haki, daima wakitafuta mafao, ustawi na maendeleo ya wengi. Ikumbukwe kwamba, rushwa ni kitendo kinachovunja sheria za nchi lakini kwa bahati mbaya, kwa sasa rushwa imekuwa kama sehemu ya maisha ya wananchi wa kawaida. Kikundi hiki kitaendelea kushirikiana kwa karibu sana na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili kuweza kuangalia uwezekano wa wale wote wanaojihusisha na rushwa kutengwa na Kanisa! Hili si jambo rahisi na kwamba, linahitaji majadiliano ya kina katika ukweli na uwazi; ili kudumisha haki na wema.

Kikundi hiki kitajitahidi kugaribisha mwelekeo sahihi wa masuala ya kisiasa kwa kukazia demokrasia na utawala bora ili kuhakikisha kwamba, Mikataba na Itifaki za Kimataifa zinatekelezwa kwa dhati kama njia makini ya kupambana na uhalifu wa kimataifa na uvunjaji wa sheria ndani na nje ya mipaka ya nchi. Mikataba ya Kimataifa ya Palermo na Merida ni kati ya mikataba inayopembuliwa kwa kina ili kuangalia utekelezaji wake. Vatican kwa upande wake, itaendelea kujizatiti katika utekelezaji wa haki na amani kwa kutambua kwamba, rushwa na ufisadi ni mambo yanayohatarisha amani na mafungamano ya kijamii.

Kanuni maadili na utu wema ni muhimu zaidi ili kuhakikisha kwamba, sheria inafuata mkondo wake. Kuna haja kuwajengea watu dhamiri nyofu kwa njia ya elimu, utamaduni pamoja na uraia. Watu hawana budi kujengewa kwa ujasiri ili kupambana na saratani ya rushwa na ufisadi duniani! Kikundi cha Washauri wa Kimataifa kinalenga pamoja na mambo mengine: kutoa tafsiri ya kina kuhusu maana ya rushwa mintarafu haki, utu na misingi ya kitamaduni. Kugaribisha madhara ya rushwa katika maisha ya watu, ustawi na maendeleo yao, ili kujenga utamaduni wa haki.

Kikundi hiki kinapania kuorodhesha madhara ya rushwa na ufisadi; kiuchuni, kijamii, kisiasa na katika maisha ya kiroho. Kumbe, kuna haja ya kuendelea kuimarisha mafungamano ya kijamii kati ya watu na taasisi ili kupambana na mifumo yote ya rushwa na ufisadi, kwa kuzingatia pia sheria za kitaifa na kimataifa; kwa kuweka hatua mbali mbali za kufuatwa katika utekelezaji wa sera na sheria. Ili kupambana vyema na rushwa pamoja na ufisadi kuna haja ya kufahamu historia yake na kuisambaza kwenye vyombo mbali mbali vya habari na mawasiliano ya jamii. Hapa kuna umuhimu wa kuimarisha dhana ya haki jamii dhidi ya rushwa na ufisadi pamoja na kuhakikisha kwamba, waathirika wa rushwa wanapewa sauti ili kusimulia athari zake na hatimaye, kukazia umuhimu wa: historia, wema, Sanaa na haki, mambo ambayo yanapaswa kuendelezwa na kudumishwa na wengi.

Kikundi cha Washauri wa Kimataifa kitaweka kwa muhtasari ushauri katika masuala ya elimu na habari katika ujumla wake; kitatoa mwono wa kisiasa, mambo msingi katika demokrasia; haki jamii na umuhimu wa kukuza na kudumisha mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili. Kuwashirikisha wadau mbali mbali ili kuchangia uzoefu, mang’amuzi na ushuhuda wao katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. Ushirikiano na wadau mbali mbali ni muhimu sana ili kuweza kufikisha mbinu za kupambana na rushwa na ufisadi duniani. Mapambano haya yanaweza pia kuhusishwa kwa kuungana na Mabaraza ya Maaskofu, Makanisa Mahalia na taasisi mbali mbali katika kuwashughulikia watuhimiwa wa kashfa ya rushwa, na pale inapowezekana kutengwa na Kanisa!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

03/08/2017 15:31