2017-08-03 15:54:00

Kardinali Parolin: Kiteni maisha yenu katika toba na wongofu wa ndani


Mama Kanisa anayo dhamana na utume wa kuhakikisha kwamba anawasaidia watu wote kuweza kupata furaha na maisha ya uzima wa milele! Hii ni njia mbayo iko wazi kwa maskini, wanaoteseka na kusukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ni mwaliko kwa waamini kujitahidi kuipitia ile njia nyembamba inayowapeleka kwenye Ufalme wa mbinguni. Ni njia inayohitaji, toba na wongofu wa ndani. Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican tarehe 2 Agosti 2017 wakati wa maadhimisho ya Siku ya Msamaha wa Assisi, iliyoadhimishwa kama sehemu ya kufunga rasmi kumbu kumbu endelevu ya Mwaka wa Jubilei ya miaka 800, tangu ilipoanzishwa.

Itakumbukwa kwamba, mwaka huu ulizinduliwa rasmi na Kardinali Gualtiero Bassetti ambaye sasa ni Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na Baba Mtakatifu Francisko kushiriki katika maadhimisho haya hapo tarehe 4 Agosti 2016. Kardinali Parolin, amewasilisha salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa mahujaji na waamini waliokuwa wamefurika katika maadhimisho haya. Maisha na utume wa Mtakatifu Francis wa Assisi bado yanaendelea kuwa ni changamoto pevu kwa kila mwamini ili kuishi kadiri ya tunu msingi za Kiinjili.

Kardinali Parolin anasema, ilikuwa ni tarehe 2 Agosti 1216, Siku ambayoMtakatifu Francis wa Assisi alikuwa amepata ruhusa ya rehema kamili kutoka kwa Papa Honorius III kwa ajili ya mahujaji wote ambao wangefanikiwa kufanya hija ya maisha ya kiroho kwenye Kanisa kuu la “Santa Maria degli Angeli”! Mtakatifu Francis wa Assisi alisherehekea tukio hili mpwitompwito, akitamani kuwapeleka watu wote mbinguni, ili waweze kufurahia maisha ya uzima wa milele, ushuhuda wa upendo thabiti ambao Mtakatifu Francis alikuwa nao mbele ya Mwenyezi Mungu kupitia kwa Kristo Yesu.

Huu ni upendo na huruma inayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu iliyomwilishwa katika maisha ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu daima anatembea bega kwa bega na waja wake, na kweli anapenda kuwashirikisha wote furaha na maisha ya uzima wa milele. Ili kufanikisha azma hii, Mwenyezi Mungu anapenda kutumia fadhila ya unyenyekevu; kwa kuchagua mahali na alama muafaka kwa ajili ya ujumbe wake. Kwa namna ya pekee, Mwenyezi Mungu amependa kujidhihirisha kati ya maskini pamoja na maskini, ili kuweza kuwanyanyua maskini waweze kupata furaha na maisha ya uzima wa milele.

Kwa njia ya unyenyekevu, Mwenyezi Mungu amemrahisishia binadamu mchakato wa kuweza kukutana na kuzungumza naye ana kwa ana! Kardinali Parolin anakazia zaidi fadhila ya unyenyekevu na kiasi, kuwa ni njia ya kuweza kushuhudia Uso wake wenye huruma na mapendo kwa wote; Mwenyezi Mungu anayejitaabisha kumganga na kumtibu mwanadamu kwa mafuta ya faraja na divai ya matumaini. Anawanyanyua wanyonge na kuwapandisha juu kama “mlingoti wa bendera” na kuwatweza wenye kiburi kama “soli ya kiatu”. Huu ni utajiri unaofumbatwa katika unyenyekevu unaomwezesha mwamini kuutambua Uso wa huruma ya Mungu ambaye amejinyenyekesha, akatwaa mwili na kuwa mwanadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi. Ni Mungu anayejinyenyesha ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Kardinali Parolin anakaza kusema, Mtakatifu Francis wa Assisi alikuwa na furaha mpwitompwito kutokana na upendo wa Mungu uliokuwa ni faraja kwa wadhambi waliokuwa wanatubu na kumwongokea na hivyo kuweza kukirimiwa rehema kamili inayotolewa na Mama Kanisa. Ikumbukwe kwamba, rehema ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu wa adhabu ya muda kwa ajili ya dhambi ambazo kosa lao limekwishafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiandaa vyema huupata; kwa kutekeleza masharti yaliyowekwa na Mama Kanisa. Rehema inaweza kuwa ni ya muda au rehema kamili.

Kimsingi kila mwamini anaweza kupata rehema kwa ajili yake mwenyewe au kwa ajili ya marehemu! Ndiyo maana Mtakatifu Francis wa Assisi alikita maisha yake katika sala na matendo ya huruma kwa maskini kwa kuacha fahari na anasa za dunia, daima akijitahidi kusoma alama za nyakati. Hiki kilikuwa ni kipindi kigumu kwa maisha ya maskini kutokana na magonjwa ya milipuko, umaskini na hali ngumu ya maisha. Mtakatifu Francis wa Assisi akaamua kujisadaka kwa ajili ya maskini, wagonjwa na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwaonjesha huruma, upendo na furaha ya maisha ya uzima wa milele. Huruma na msamaha wa Mungu ilikuwa ni chachu ya mageuzi na upyaisho wa maisha ya kiroho. Tafakari ya Neno la Mungu na maisha ya Kisakramenti, vikapewa msukumo wa pekee, kama chemchemi ya furaha na maisha ya uzima wa milele.

Kardinali Pietro Parolin anawataka waamini kwa mfano wa maisha ya Mtakatifu Francis wa Assisi kuwa na mwelekeo mpya wa uhalisia wa maisha, kwa kumwendea zaidi Kristo Yesu kwa njia ya Bikira Maria ili kuweza kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha, daima wakikaza macho kama gumegume kuelekea kwenye maisha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.