2017-08-02 15:28:00

Vijana jengeni jamii isiyopekenyuliwa na rushwa pamoja na ufisadi!


Vijana wanahamasishwa kusimama kidete kupambana kufa na kupona na saratani ya rushwa inayopekenyua jamii nyingi duniani, ili hatimaye, kujenga jamii inayosimikwa katika misingi ya haki! Ni changamoto na mwaliko kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko alioutoa kwa vijana nchini Brazil, waliokuwa wanaaadhimisha Siku ya Vijana Kitaifa, kuanzia tarehe 29 - 30 Julai 2017 kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Aparecida. Hii ni sehemu ya kumbu kumbu ya miaka 300 tangu Sanamu ya Bikira Maria wa Apareida ilipokotwa mtoni!

Baba Mtakatifu anafanya rejea kwenye ujumbe wake katika maadhimisho ya Siku ya XXXII Vijana Duniani, akimwonesha Bikira Maria kuwa ni mfano bora wa kuigwa kwa vijana wanaothubutu kufanya hija makini katika maisha yao ya kiroho. Anawataka vijana kuendelea kutafakari kuhusu maisha na utume wa Bikira Maria katika historia nzima ya ukombozi. Tafakari hii imekuwa ni msaada mkubwa kwake binafsi, alipotembelea kwenye madhabahu haya kunako mwaka 2007 wakati wa mkutano wa Shirikisho la Mabaraza ya maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na alipotembelea tena eneo hili kunako mwaka 2013 kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, huko Rio de Janeiro, nchini Brazil.

Hapa ni mahali ambapo vijana wanaweza kutafakari na hatimaye kugundua uso wa Bikira Maria, Mama mwenye huruma, chemchemi ya matumaini  kwa watu wa kawaida nchini Brazil, inayowawezesha kukabiliana na changamoto za maisha kwa imani na ujasiri mkubwa, kila siku ya maisha yao. Ni uso wa Bikira Maria mwenye nguvu anayeweza kuwakirimia wale wote wanaokimbilia msaada, maombezi na tunza yake ya kimama, nguvu ya kuweza kufanya mageuzi makubwa katika maisha, kwa kutoka katika ubinafsi na kuanza kujikita katika ari na mwamko wa kimissionari, kama ambavyo vijana hawa waliweza kutekeleza wakati wa maadhimisho ya Juma la Kimissionari nchini Brazil, ambalo limehitimishwa hivi karibuni.

Baba Mtakatifu Francisko anachukua fursa hii kuwashukuru na kuwapongeza kwa moyo na bidii na ushuhuda wao wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika shida na mahangaiko ya kila siku na  kuendelea kushamiri kwa ukosefu wa haki msingi za binadamu, vijana wawe na uhakika kwamba, wanaye Mama Bikira Maria, kielelezo cha matumaini, ambaye kwa maombezi na tunza yake ya kimama, anawajalia mwamko na ari kuu ya maisha na utume wa kimissionari, kwani anatambua kwa kina na mapana, changamoto ambazo vijana wa kizazi kipya nchini Brazil wanakabiliana nazo kila siku ya maisha. Bikira Maria kwa tunza yake ya kimama atawawezesha kutambua kwamba, katika hija ya maisha, wanaye mwandani anayeweza kuwashangaza katika maisha, kama alivyofanya kwa wale wavuvi miaka 300 iliyopita, kwa kuwakirimia wananchi wa Brazil umoja wa kitaifa.

Hii ndiyo Brazil iliyokuwa imegawanyika kati ya watawala na watumwa; kwa muujiza huu Brazil ikaunganishwa tena kwa njia ya imani thabiti kwa Kristo na Kanisa lake. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika vijana wa kizazi kipya nchini Brazil, kumwachia nafasi Bikira Maria wa Aperecida kuwaletea mageuzi katika maisha, kwa kuwatengenezea nyavu zinazoweza kuunda mtandao wa maisha na urafiki; mtandao wa kijamii, mambo ya kidunia na fadhili. Haya ni mambo ambayo yanaweza kumwilisha katika jamii ya watu; jumuiya yenye ari na mwamko wa kimissionari inayotoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Jumuiya  ziwe ni mwanga na chachu ya ujenzi wa jamii inayomsikwa katika haki na udugu!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, huu ndio mchakato unaopania kuipyaisha tena Brazil, bila wasi wasi wala mashaka ya kujizatiti katika ujenzi wa jamii mpya inayosimikwa katika tunu msingi za maisha ya Kiinjili. Lengo ni kuweza kuchachua maisha ya kijamii, kisiasa na katika mazingira ya taasisi za elimu ya juu na vyuo vikuu kwa tunu msingi za Kiinjili. Baba Mtakatifu anawataka vijana kuonesha ujasiri kwa kupambana na rushwa pamoja na ufisadi na kamwe wasikubali kuambukizwa na saratani ya rushwa katika maisha yao.

Vijana wajiaminishe kwa Mwenyezi Mungu kwa kukimbilia tunza ya Bikira Maria, ili hatimaye, waweze kugundua ndani mwao kile kipaji cha ubunifu na nguvu inayowapatia jeuri ya kuwa ni wadau wakuu katika utamaduni wa mshikamano ili hatimaye, waweze kuunda miundo mipya ya uongozi, ili kutoa dira na mwelekeo mpya nchini Brazil. Mwishoni, Baba Mtakatifu Francisko anawaombea vijana, ili kwa maongozi na maombezi ya Bikira Maria wa Aparecida, awasaidie kupyaisha tena matumaini; ari na mwamko wa kimissionari, kwa kutambua kwamba, vijana ni matumaini ya Brazil na ulimwengu katika ujumla wake. Vijana wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa waja wake na kwamba, Bikira Maria, aweze ni kiongozi wao wa daima.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.