Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Baba Mtakatifu Francisko \ Katekesi siku ya Jumatano

Ubatizo ni mlango wa matumaini ya Kikristo!

Papa Francisko: Ubatizo ni mlango wa matumaini ya Kikristo. - REUTERS

02/08/2017 14:03

Kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo na imani katika Kristo Yesu, waamini wanakuwa ni wana wa Mungu kwa maana wale wote waliobatizwa katika Kristo Yesu, wamemvaa Kristo na hivyo kuvunjilia mbali utengano kati ya Wayunani na Wayahudi; watumwa au watu huru; wanaume au wanawake, kwani wote wamekuwa wamoja katika Kristo! Sakramenti ya Ubatizo ni mlango wa matumaini! Hii ndiyo kauli mbiu ambayo imeongoza katekesi ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumatano, tarehe 2 Agosti, 2017 baada ya mapumziko ya Kipindi cha Kiangazi. Huu ni mwendelezo wa katekesi kuhusu matumaini ya Kikristo!

Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini kutambua alama na ufafanuzi unaotolewa na Mama Kanisa katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa kwani alama hizi zinabeba utajiri mkubwa katika maisha, imani na matumaini ya watu. Mashariki ni mahali ambapo jua linazama na upande wa Magharibi ni mahali ambapo jua linachomoza. Ni kwa njia ya rehema za Mwenyezi Mungu, mwangaza utokao juu umewafikia watu wake. Yesu ni jua la haki linalowapambazukia wale wote wanaomwamini na kumfuasa kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo.

Katika Ibada ya Ubatizo kwenye Mapokeo ya zamani, wakatekumeni walikuwa wanakiri na kuungama imani wakiwa wameangalia upande wa Mashariki kwa kujibu maswali yanayoonesha kumkataa shetani na mambo yake yote pamoja na fahari zake zote kwa kuungama Imani katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, Ibada ya Ubatizo kwa wakati huu imepoteza lugha ya picha na kubakiza kanuni na ungamo la imani linalojihidhirishwa kwa maswali wakati wa ubatizo. Umuhimu wake unabaki kama ulivyo na wala hakuna mabadiliko anasema Baba Mtakatifu. Kuwa Mkristo maana yake ni kuangalia Jua la haki na kuendelea kuungama Imani katika mwanga hata pale ambapo giza linaonekana kutaka kuitawala dunia.

Wakristo wakumbuke kwamba, daima wanagubikwa na giza la ndani na nje ya maisha yao, kwani wanaishi ulimwenguni, lakini mwanga walioupokea wakati wa Ubatizo unawaelekeza katika mwelekeo mpya wa mwanga wa maisha, wenye matumaini ya mapambazuko; watu wasiokubali kumezwa na giza la kifo, bali wanapambana ili kufufuka na kutembea katika mwanga wa Kristo Mfufuka; ni watu ambao hawakubali kupigishwa magoti na ubaya wa dhambi, kwani wanatumaini kwamba, wema daima utashinda ubaya!

Wakristo ni watu wanaoamini kwamba, Mwenyezi Mungu ni Baba, ambaye kimsingi ni mwanga. Wanaamini na kukiri kwamba, Kristo Yesu ameshuka kutoka mbinguni na yuko kati yao; ametembea katika hija ya maisha yao akiwaonesha kuwa kweli ni mwandani wa maisha, hasa kwa maskini na wanyonge zaidi. Kristo ndiye mwanga wa mataifa! Wakristo wanaamini na  kusadiki kwamba, Roho Mtakatifu anaendelea kutenda kazi zake bila kusimama kwa ajili ya ustawi, wema na maendeleo ya binadamu na ulimwengu wote katika ujumla wake, kiasi kwamba, hata machungu makubwa kiasi gani katika historia ya maisha ya binadamu yataweza kutoweka na kwamba, haya ndiyo matumaini wanayokirimiwa Wakristo kila kunapopambazuka. Wakristo wana amini kwamba, kila wema, urafiki, nia njema, upendo wa dhati kiasi hata cha yale mambo madogo madogo kabisa, siku moja yatapata utimilifu wake mbele ya Mwenyezi Mungu. Hii ndiyo nguvu inayowasukuma Wakristo kukumbatia maisha yao ya kila siku.

Liturujia ya Ubatizo, inawakumbusha waamini umuhimu wa alama ya mwanga katika maisha yao! Huu ni mwanga ambao wazazi na wasimamizi wa Ubatizo au Wakristo wenyewe wanapewa baada ya kuwashwa kwenye Mshumaa wa Pasaka, uliowashwa wakati wa Mkesha wa Pasaka, ili kufukuzia mbali giza na nguvu za shetani kwa kuonesha Fumbo la Ufufuko wa Kristo. Waamini wote wanawasha mishumaa yao kutoka kwenye Mshumaa wa Pasaka, alama ya kwamba, mwanga wa Kristo Mfufuka unaingia na kupenyeza pole pole katika maisha ya Wakristo. Maisha ya Kanisa ni mwanga unaomwilishwa miongoni mwa watu.

Wakristo kwa njia ya Sakramenti ya Ubatizo, wamezaliwa mara mbili: mara ya kwanza ni kwa njia ya asili na mara ya pili wanazaliwa kwa njia ya neema inayobubujika kutoka kwa Kristo katika Kisima cha Ubatizo. Kwa njia ya Ubatizo, wakristo wanaifia dhambi na kufufuka pamoja na Kristo, changamoto ya kushuhudia ile harufu safi ya mafuta ya Krisma ya Ubatizo. Katika maisha ya Wakristo kuna Roho wa Kristo Yesu anayeishi na kutenda kazi ndani mwao, Mwana mzaliwa wa kwanza kutoka kwa wafu na ndugu yake wale wote wanaopambana dhidi ya nguvu za giza na ubaya wa dhambi.

Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha Wakristo kwamba, kwa njia ya neema ya Ubatizo wanakuwa kweli ni “Christophoro”, yaani “Wabeba Kristo” duniani hasa zaidi kwa wale; wenye huzuni, waliokata tamaa; wanaotembea katika giza la mauti, chuki na uhasama. Mwanga ambao Wakristo wanauhifadhi katika mboni ya macho yao unazama hadi undani wa maisha ya watu, kwa kuonesha kwamba, wanawapenda na kuwatakia mema, wale waliokata tamaa ya maisha.

Wakristo waandike historia ya maisha na utume wao katika ushuhuda wa matumaini na kwamba, wanachangamotishwa na Mama Kanisa kuwa waaminifu kwa imani yao katika Sakramenti ya Ubatizo; waendelee kujizatiti katika kutawanya mwanga wa matumaini ya Mungu, ili kuwatangazia na kuwarithisha vijana wa kizazi kipya maana ya maisha! Kwa ufupi kabisa, Sakramenti ya Ubatizo ni Fumbo la Matumaini thabiti yasiyoweza kumdanga mtu awaye yote, kwani yanawawezesha waamini kuingia na kuzama katika upendo na huruma ya Mungu na hivyo kuwa Altare ya Roho Mtakatifu; watoto wa Ufalme wa Mungu na viungo hai vya Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Wakristo wanahamasishwa kukumbuka siku yao ya Ubatizo na kuisherehea mpwitompwito! Kwani hii ndiyo siku yao ya kuzaliwa upya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

02/08/2017 14:03