2017-08-02 14:55:00

Siku ya Utalii Duniani 2017: Utalii endelevu ni chombo cha maendeleo


Sekta ya utalii inaweza kuwa ni chombo muhimu sana katika mchakato wa kukuza uchumi sanjari na kupambana na baa la umaskini duniani. Hivi ndivyo anavyobainisha Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu katika ujumbe wake kwa ajili ya maadhimisho ya Siku ya Utalii Duniani yatakayofikia kilele chake hapo tarehe 27 Septemba 2017, kwa kuongozwa na kauli mbiu “Utalii endelevu ni chombo cha maendeleo”. Mama Kanisa anapenda kuungana na Jumuiya ya Kimataifa kuadhimisha Siku hii kwa kutambua kwamba, kazi msingi na halali hazina budi kupata nafasi katika moyo wa mfuasi wa Kristo!

Kwa mara ya kwanza, ujumbe huu unatolewa na Baraza hili jipya la Kipapa ili kuungana na Umoja wa Mataifa uliotangaza Mwaka 2017 kuwa ni Mwaka wa Kimataifa wa Utalii endelevu na maendeleo. Ni ujumbe ambao umetolewa kwa wakati muafaka na Shirika la Utalii Duniani, “UNWTO” linalokazia kwa namna ya pekee utalii wa kiutamaduni, kilimo na mazingira ili kukuza na kudumisha misingi ya amani ushirikishwaji wa umma, ili kuongeza pato la taifalinalotokana na utalii. Kardinali Peter Turkson anakaza kusema kwamba, sekta ya utalii ina umuhimu mkubwa sana katika ustawi na maendeleo ya watu. Ni sekta inayowahusisha watu wengi wanaosafiri kama watalii au kama wafanyakazi. Ni sekta inayochangia katika ukuaji wa uchumi, utamaduni na kijamii.

Lakini pia, sekta ya utalii ni hatari na changamoto zake. Takwimu za Shirika la Utalii Duniani zinaonesha kwamba, katika kipindi cha Mwaka 2016 idadi ya watalii duniani iliongezeka na kufikia kiasi cha watalii milioni 1235. Sekta ya utalii inachangia walau asilimi 10% ya Pato Ghafi la Taifa na kiasi cha asilia 7% ya biadhaa zinazosafirishwa na kuuzwa nchi za nje pamoja na kuchangia upatikanaji wa fursa za ajira. Mchango wa sekta ya utalii unayotofautiana toka taifa moja hadi jingine kutokana na rasilimali zilizopo na hasa kwa zile nchi ambazo zinaendelea kuwekeza zaidi katika  maendeleo endelevu na shirikishi sanjari na utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote.

Kardinali Peter Turkson anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuiangalia sekta ya utalii kama chombo cha ukuaji wa uchumi sanjari na mapambano dhidi ya baa la umaskini duniani. Hapa kuna haja ya kuwa makini kwani, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanapozungumzia kuhusu maendeleo endelevu ya binadamu yanakuwa na mwono mpana zaidi na wala si tu katika ukuaji wa sekta ya uchumi, bali ni maendeleo endelevu yanayogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili kama yanavyofafanuliwa na Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka wake wa Kitume ”Populorum progressio” yaani ”Maendeleo ya watu”.

Haya ni maendeleo makini yanayogusa utu na heshima ya binadamu; changamoto iliyovaliwa njuga na Kanisa na kunako mwaka 1987, Umoja wa Mataifa kwa mara ya kwanza ukaanza kutumia ”Dhana ya maendeleo endelevu”; mchakato unaogusa na kufumbata medani mbali mbali za maisha ya binadamu: kiuchumi, kijami, kisiasa na kitamaduni. Kwa maneno mafupi, ni mchakato wa maendeleo unaomgusa mtu mzima: kiroho na kimwili! Kumbe, utalii endelevu, unapaswa kuwa ni utalii unaowajibika; unaojikita katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote; kwa kuheshimu utamaduni, mila na desturi za watu mahalia; kwa kusimama kidete katika kulinda na kudumisha utu na heshima binadamu pamoja na wafanyakazi, hasa maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Wakati wa likizo ni muda muafaka wa kuwajibika na wala si wakati wa kuponda mali na ”kujirusha pasi na nidhamu” bali ni wakati wa kila mtu kuthamini maisha yake binafsi na yale ya jirani zake. Utalii endelevu ni chombo makini cha maendeleo hata katika nchi zile ambazo zimekumbwa na athari za myumbo wa uchumi kitaifa na kimataifa; unakuwa ni fursa ya kukabiliana na matatizo pamoja na changamoto za maendeleo na kamwe haupaswi kuwa kuwa ni sababu ya matatizo. Utalii endelevu unapaswa kuwa ni kichocheo makini miongoni mwa watu, kinachowawezesha kujitegemea na kushiriki kikamilifu katika mchakato mzima wa maendeleo endelevu!

Kardinali Peter Turkson anakaza kusema, utalii endelevu unapaswa kusaidia kupyaisha maboresho ya mchakato wa ekolojia ya kijami inayoendeleza na kudumisha jamii husika; ekolojia ya kiuchumi inayohamasisha ukuaji wa uchumi shirikishi. Mwaka wa Kimataifa wa Utalii endelevu na maendeleo uziwezeshe serikali mbali mbali kuwa na mbinu mkakati pamoja na sera makini zitakazosaidia kuchochea utalii endelevu na maendeleo. Kanisa kwa upande wake, litaendelea kusimama kidete kulinda na kudumisha utu na heshima ya binadamu mintarafu mwanga wa Injili; kwa kuendeleza mazingira nyumba ya wote, kama sehemu ya kazi ya uumbaji inayowawajibisha binadamu.

Mambo msingi yanayopaswa kupewa msukumo wa pekee ni mshikamano, haki na upendo wa kidugu. Hizi ni kanuni zinazopaswa kuzingatiwa na wadau wote kwa kubadili mfumo wa maisha, mahusiano na mafungamano ya kijami. Kanisa linapenda kuhakikisha kwamba, utalii unachangia kwa kiasi kikubwa maendeleo endelevu ya binadamu kwa kufumbatwa katika ushirikiano, mshikamano kwa kutambua na kuthamini vivutio vya kitamaduni, kielelezo makini cha uzuri. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira kama uelewa wa udugu na heshima kwa utakatifu wa maisha ya binadamu na kazi ya uumbaji.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.