2017-08-01 15:00:00

Uchaguzi mkuu Kenya kwa Mwaka 2017: Ombeeni amani na maendeleo!


Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawaalika watu wa Mungu nchini humo, kuhakikisha kwamba, wanashiriki kikamilifu katika utekelezaji wa haki yao ya kikatiba na kidemokrasia kwa kupiga kura ili kuwachagua viongozi watakawaongoza na kuwapatia dira na mwelekeo sahihi wa maisha katika mchakato mzima wa maendeleo endelevu ya binadamu! Maaskofu wanawataka wananchi wa Kenya kuhakikisha kwamba, uchaguzi unakuwa: huru, wa haki, amani na kweli. Hili kuweza kufanikisha azma hii, kuna haja kwa wananchi wote kuunda mazingira ya amani yanayoonesha uzalendo kwa nchi ya Kenya. Maaskofu wanasema, wananchi waongozwe na kauli mbiu “Tafuteni amani na maendeleo endelevu” (Rej. Yer. 29:7).

Maaskofu wanapenda kuwapongeza wagombea uchaguzi pamoja na wapambe wao ambao kwa siku za hivi karibuni wameendesha kampeni za kistaarabu na kuwataka kuendelea na msimamo huu, ili kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya kitaifa. Maaskofu wanawataka vijana kutojihusisha hata kidogo na ghasia, badala yake, wawe ni mashuhuda na vyombo vya utamaduni wa amani, ili kuendeleza tunu hii muhimu katika ustawi na maisha ya wananchi wote wa Kenya.

Maaskofu wanawahimiza kwa mara nyingine tena, wadau wote kuhakikisha kwamba, uchaguzi mkuu unafumbatwa katika: uhuru, haki, amani na ukweli. Maaskofu wanakaza kusema, watashirikiana kwa karibu sana na watazamaji wa uchaguzi mkuu, ili kuhakikisha kwamba, mambo yote yanakwenda kama yalivyopangwa! Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linathamini sana mchango wa tasnia ya habari katika kuhabarisha na kwamba, vyombo hivi vitekeleza dhamana na wajibu wake kwa kuwajengea watu mazingira ya amani, ili kukuza na kudumisha utamaduni wa haki, amani na upatanisho nchini Kenya.

Vyombo vya ulinzi na usalama, vitekeleze dhamana na wajibu wake barabara, ili kufanikisha mchakato mzima wa uchaguzi mkuu. Mahakama, ihakikishe kwamba, haki inatendeka, kwa wao kutekeleza dhamana na wajibu wao kwa kuzingatia weledi, uadilifu, uwajibikaji na nidhamu kazini bila woga wala vitisho! Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya linawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuanzia tarehe 30 Julai hadi tarehe 7 Agosti, 2017 kusali Novena kwa ajili ya kuombea mafanikio ya mchakato mzima wa uchaguzi mkuu nchini humo. Wanamwomba Mwenyezi Mungu kuwasimamia waja wake, ili amani iweze kutawala miongoni mwa wananchi wote wa Kenya!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.