2017-08-01 11:07:00

Maboresho ya huduma ya maji safi na salama nchini Tanzania


Taarifa kutoka Umoja wa Mataifa zinaonesha kwamba walau kuna zaidi ya watu bilioni 2.1 hawana fursa ya kupata maji safi na salama majumbani mwao na kwamba, watu zaidi ya bilioni 4.5 hawana mfumo bora wa majitaka, hali inayohatarisha watu wengi kukumbwa na magonjwa yanayotokana na ukosefu wa matumizi ya maji safi na salama. Maboresho ya maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya watu ni muhimu sana katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030 ili kupunguza magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi na salama, kwani hii pia ni sehemu ya haki msingi za binadamu. Bwana Anthony Lake, Mkurugenzi mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF anasema, maji safi na salama; usafi sanjari na huduma bora za afya ni mambo msingi sana kwa ajili ya kuwajengea watoto matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu wa Tanzania Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la upatikanaji wa maji safi na salama katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania, ikiwemo wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ilitengewa sh. bilioni 2.72 kwa ajili ya ujenzi wa miradi ya maji. Amesema mkakati huo unatekelezwa kupitia Kampeni ya Rais Dkt. John Magufuli ya kumtua mama ndoo, na kwamba wananchi katika maeneo yote nchini Tanzania watapata huduma ya maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 kutoka kwenye makazi yao.

Waziri Mkuu aliyasema hayo Jumapili, Julai 30, 2017 alipozungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa Halmashauri za Rungwe na Busokelo katika mikutano ya hadhara aliyoifanya Kandete na Tandale katika wilaya ya Rungwe, mkoani Mbeya. Alisema mkoa wa Mbeya umetengewa sh. bilioni 10.383 kwa ajili ya utekelezaji miradi mbalimbali ya maji, ambapo kati yake sh. bilioni 2.72 zinatarajiwa kutumika katika utekelezaji wa miradi ya maji kwenye wilaya ya Rungwe.

Waziri Mkuu alitaja mradi mwingine unaotekelezwa wilayani Rungwe ni pamoja na mradi wa maji wa Masoko wenye thamani ya sh. bilioni 5.3, utakaohudumia jumla ya vijiji 15.“Mradi huu ni miongoni mwa miradi inayojengwa chini ya Programu ya Maendeleo ya Sekta ya Maji kwa fedha za ndani.”  Alisema mradi huo utakapokamilika utawanufaisha wananchi wapatao 19,624 katika vijiji vya Bulongwe, Ngaseke, Igembe, Ntandabala, Lupando, Bujesi, Lufumbi, Nsyasa, Ikama, Itagata, Busisya, Mbaka, Isabula, Lwifa na Nsanga.

Pia Waziri Mkuualisema wananchi lazima wazingatie sheria ya Mazingira inayozuia kufanya shughuli za kibinadamu pamoja na kujenga kwenye maeneo yote ya vyanzo vya maji ndani ya mita 60 ili kuliepusha Taifa kugeuka jangwa. Kufuatia hali hiyo Waziri Mkuu aliwaagiza watendaji kuwachukua hatua watu wote watakaokutwa wakiendesha shughuli mbalimbali kama za kilimo, ujenzi wa makazi na uchungaji wa mifugo ndani ya vyanzo vya maji kwa kuwa zinasababisha ukame. “Hatuwezi kuruhusu Taifa likaangamia kwa ajili ya watu wachache wanaoharibu mazingira kwa kuendesha shughuli za kibinadamu ndani ya vyanzo vya maji. Ni marufuku kufanya shughuli za kibinadamu ndani ya mita 60 kutoka katika vyanzo vya maji, atakayekutwa atachukuliwa hatua za kisheria.”

Awali Mbunge wa Jimbo la Busokelo Mheshimiwa Fredy Mwakibete na Mbunge wa Rungwe Mheshimiwa Saul Amon walimueleza Waziri Mkuu kwamba upatikanaji wa huduma ya maji na salama ni miongoni mwa changamoto zinazoyakabili majimbo yao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.