2017-08-01 14:37:00

Injili ya amani inasimikwa katika: haki, upendo, utu na maendeleo!


Amani ni msingi wa wema, heshima na maendeleo endelevu ya binadamu; ni paji na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomshirikisha na kumwajibisha binadamu. Amani ni tunda la upendo linalopaswa kuboreshwa kwa njia ya malezi ya dhamiri nyofu; ukweli na uhuru; usalama wa raia na mali zao; kwa kulinda na kuheshimu utu wa binadamu, ustawi na maendeleo ya wengi. Kwa ufupi, amani ni kazi ya haki na matunda ya upendo! Amani inatishiwa sana na mashindano ya silaha duniani; utengenezaji na biashara ya silaha pamoja na mchakato wa ulimbikizaji wa silaha duniani! Ni wajibu wa Jumuiya ya Kimataifa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani!

Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia anasema, imegota miaka mia moja tangu Papa Benedikto XV, tarehe 1 Agosti 1917 alipochapisha Waraka wake wa kitume kwa wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa akilaani vikali Vita Kuu ya Kwanza ya Dunia kwa kukazia kwamba, haya yalikuwa ni maafa “yasiyokuwa na mashiko”. Ni waraka ambao ulilitikisa Kanisa, lakini Papa Benedikto XV akasimama imara kulaani vita iliyokuwa ni chanzo kikuu cha maafa, mateso na mahangaiko ya binadamu! Mapigano haya kila siku yaliendelea kusababisha maafa kwa watu wasiokuwa na hatia. Hata baada ya miaka mia moja, bado Kanisa linakaza kusema, vita ni majanga yasiyokuwa na mashiko, kuna umuhimu wa kuzingatia kanuni maadili na sera makini za kisiasa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi

Papa Benedikto XV aliitaka Jumuiya ya Kimataifa kujizatiti katika ujenzi wa amani dumifu, inayofumbatwa katika ukweli, haki, upendo na uhuru kamili. Aliwataka wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kusitisha mapigano na kuanza kujikita katika nguvu ya kimaadili; dhana ambayo ilijikita katika ushuhuda wa kinabii. Kwa wakati ule yaliyonekana kuwa ni maneno yasiyokuwa na nguvu! Lakini, baada ya miaka 100, maneno haya bado yanagusa akili na nyoyo za watu dhidi ya vita na madhara yake. Badala ya kuwekeza katika utengenezaji na ulimbikizaji wa silaha duniani, rasilimali hii ingeweza kuwekezwa zaidi kwa ajili ya maendeleo ya wengi.

Baba Mtakatifu Francisko bado anaendelea kuitaka Jumuiya ya Kimataifa kusaidia kuokoa maisha ya wahamiaji na wakimbizi wanaokufa maji kila siku kwenye tumbo la Bahari ya Mediterrania kwa kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi! Papa Benedikto XV kwa Waraka wake ule, alikuwa anaanza kuandika taalimungu mpya mintarafu amani, kwani ujumbe wa Kristo Yesu unafumbatwa katika Injili ya amani. Huu ndio mwendelezo uliovaliwa njuga na Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa Kitume “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani”, aliouandika kunako mwaka 1963: akikazia kwa namna ya pekee kabisa: ukweli, haki, upendo na uhuru.

Tangu Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, Kanisa limeendelea kuandika na kushuhudia Injili ya amani inayofumbatwa kwa namna ya pekee kabisa katika tunu msingi za Kiinjili yaaani: haki, upendo, utu na heshima ya binadamu. Hii ni misingi inayopambana na vitendo vyote vya kigaidi, vita na machafuko ya aina mbali mbali ambayo kimsingi ni kashfa kubwa kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Jumuiya ya Kimataifa anasema Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia haina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha amani dhidi ya ubinafsi, uchoyo na uchu wa utajiri wa haraka haraka unaonuka damu ya watu wasiokuwa na hatia! Kutafuta amani na kuidumisha ni kitendo cha kishujaa na ushupavu wa hali ya juu kabisa.

Ni dhamana inayopaswa kutekelezwa na kumwilishwa katika maisha ya kila siku. Nguvu ya imani, itawale zaidi kuliko silaha zinazosababisha maafa kwa watu na mali zao; nguvu ya majadiliano katika ukweli na uwazi, ipewe kipaumbele cha kwanza, kuliko kupimana nguvu kwani katika vita hakuna mtu anayeweza kujigamba kwamba, ameshinda! Nguvu ya kimaadili ipewe nafasi ya kwanza badala ya utawala wa mabavu! Hiki ni kipindi muafaka cha kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha amani duniani, kwa ujasiri na ushupavu; kwa kukazia umuhimu wa amani kama kikolezo kikuu cha maendeleo endelevu ya binadamu, ili kuondokana na vita inayosababisha maafa kwa watu wasiokuwa na hatia!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.