2017-07-31 09:37:00

Watawa iweni mashuhuda wa kinabii na wajenzi wa mshikamano!


Changamoto kubwa inayowakabili watawa katika ulimwengu mamboleo ni ushuhuda wa kinabii, unaofumbatwa kwa kujiaminisha katika ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu inayorutubishwa kwa: maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Lengo ni kuwaonjesha uwepo endelevu wa Mungu katika historia ya mwanadamu! Hii inatokana na ukweli kwamba, tabia ya ukanimungu inataka kumwondoa Mwenyezi Mungu katika maisha ya mwanadamu! Kumbe, ushuhuda wa kinabii ni muhimu sana kwa watawa wa nyakati hizi.

Changamoto ya pili ni kwa watawa kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano wa dhati, unaovunjilia mbali ubinafsi, uchoyo, udini, ukabila na mifumo yote ya kibaguzi, inayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa utu na heshima ya binadamu! Ushuhuda wa mshikamano kati ya watawa wanaotoka katika nchi, tamaduni na mazingira tofauti ni muhimu sana kama kielelezo cha ushuhuda wa Injili ya mshikamano iliyotangazwa na kushuhudiwa na Kristo Yesu!

Hii ni sehemu ya mahubiri yaliyotolewa na Mheshimiwa Padre Mario Aldegani, Mkuu wa Shirika la “Giuseppini del Murialdo” wakati wa Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa la Msalaba Mtakatifu, Makao Makuu ya Shirika la Masista wa Mateso wa Mtakatifu Paulo wa Msalaba, mjini Roma, wakati watawa sita wa Shirika hili walipokuwa wanaweka nadhiri zao za daima, Jumamosi, tarehe 29 Julai 2017. Padre Mario Aldegani alisema, hii ilikuwa ni siku kubwa iliyosheheni furaha kwa familia ya Masista wa Mateso wa Mtakatifu Paulo wa Msalaba walipokuwa wanamwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa ajili ya sadaka na maisha ya watawa sita, ambao wamejiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kwa kuweka nadhiri za daima, tayari kushiriki katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu, wakiwasaidia watu wa Mungu kuigundua hazina iliyofichika yaani: Ufalme wa Mungu na Kristo mwenyewe aliye njia, ukweli na uzima.

Dhamana na kiini cha furaha ya watawa hawa ni uaminifu wao kwa Mwenyezi Mungu, kwani wanaitwa kumfuasa na kufanana zaidi na Kristo katika maisha na utume wao. Wameitwa na kuchaguliwa na Kristo Mwenyewe si kwa mastahili au uweza wao binafsi, bali ni kutokana na upendo wa dhati ambao Kristo Yesu amewaonesha. Watambue udhaifu wao wa kibinadamu kwani zawadi na wito huu wa maisha ya kitawa, umehifadhiwa katika chombo cha udongo! Lakini, kwa neema na upendo wa Mungu, wameteuliwa kati ya vijana wengi walioanza safari ya maisha na wito wa kitawa katika Shirika hili. Hapa, hakuna “uchawi” bali ni upendo wa Kristo unaodhihirishwa ndani mwao.

Kwa vile wamependwa zaidi, wanapaswa kuumwilisha upendo huu kama kielelezo cha shukrani na sadaka ya maisha kwa kukumbuka daima kwamba, wito ni zawadi, ni neema na baraka kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Ufalme wa Mungu. Watawa hawa wameteuliwa kama lulu yenye thamani kubwa; wao ni sawa na hazina iliyofichika; sasa wamewekwa wakfu kuwa ni manabii wa Mungu kwa njia ya ushuhuda wa furaha ya Injili, uaminifu na udumifu, kielelezo makini cha uwepo wa Mungu kati pamoja na watu wake. Watawa walioweka nadhiri zao za daima, wawe ni mashuhuda na vyombo vya huruma ya Mungu kwa watu wa Mataifa, wao pia wakijitahidi kujiweka chini ya huruma na tunza ya Mwenyezi Mungu kwa kutambua pia kwamba, kweli wamependwa zaidi.

Nadhiri za daima, ni njia tu ya kushuhudia maisha yanayofumbatwa katika imani, matumaini na mapendo kwa watu wa nyakati hizi waliochoka na kukata tamaa ya maisha! Nadhiri za usafi wa moyo, ufukara na utii, zinaweza kumwilishwa na watu mbali mbali kwa malengo na nia tofauti, kumbe, hii si habari tena! Jambo la msingi ni ushuhuda wa ukweli wa maisha yao ya kitawa yanayojikita katika unabii na ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu kati pamoja na watu wake. Watawa wawe ni mashuhuda wanaojiaminisha mbele ya Mungu, kielelezo cha shukrani, furaha na sadaka inayotolewa kwa ajili ya huduma ya ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Watawa wawe ni vyombo na mashuhuda wa mshikamano wa umoja, upendo na udugu; kwa kuishi kweli za Kiinjili, kiasi na unyenyekevu! Watawa waoneshe kwa ukamilifu kwamba, kweli inalipa kuishi katika Jumuiya, kwani Jumuiya ni Fumbo la maisha, linalomwilishwa kila siku ya maisha!

Sr. Maria D’Alessandro, Mama Mkuu wa Shirika la Masista wa Mateso wa Mtakatifu Paulo wa Msalaba ndiye aliyepokea Nadhiri za daima kutokana na mamlaka aliyokabidhiwa na Mama Kanisa. Watawa wameonesha nia yao thabiti ya kutaka kufuata Injili ya Mateso ya Kristo kwa uaminifu zaidi mintarafu Sheria za Shirika lao, ili hatimaye, waweze kupata utimilifu wa maisha kwa njia ya huduma kwa Mungu na jirani. Kwa kutegemea na kujiaminisha mbele ya huruma na neema ya Mwenyezi Mungu katika maisha yao, watawa hawa wanapania kujisadaka kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu; kwa kujiweka wakfu maisha yao yote, ili kutangaza na kushuhudia kwa njia ya maisha na matendo yao Fumbo la Mateso ya Kristo Yesu. Watawa hawa wameombewa ili hiyo kazi njema iliyoanzishwa na Mwenyezi Mungu ndani mwao, aweze, Yeye mwenyewe kuikamilisha.

Watawa walioweka nadhiri zao za daima ni:

  1. Sr. Beatrice Antony Shayo kutoka Tanzania
  2. Sr. Linda Anyango Osiro kutoka Kenya
  3. Sr. Francisca Mutheu Muange kutoka Kenya
  4. Sr. Carine Amannakou kutoka DRC
  5. Sr. Gertrude Ogechi Keke kutoka Nigeria
  6. Sr. Teresa Uchechi Isiagu kutoka Nigeria.

Maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu tangu mwanzo yalipambwa kwa utamadunisho na ishara mbali mbali zilizoonesha, kuwa kweli watawa hawa sita ni sawa na wale wanawali sita waliokuwa na busara ambao walichukua taa na akiba ya mafuta, wakawa tayari kumsubiri Bwana harusi. Kwa maandamano ya watawa wenye taa zilizokuwa zinawaka, walionesha utayari wao wa “kufunga pingu za maisha” na Kristo Yesu kwa njia ya Nadhiri za daima, tayari kuwahudumia watu wa Mungu kwa njia ya Shirika la Masista wa Mateso wa Mtakatifu Paulo wa Msalaba. Wakati wa kuimba, Utukufu kwa Mungu juu na amani duniani; Kanisa zima lililipuka kwa shangwe na vigelegele, kwa kuserebuka na kunyata nyaah!

Neno la Mungu ambalo ni taa inayoangazia miguu na maisha ya watawa. Hili ni Neno la Mungu linalorutubisha imani, matumaini na mapendo kwa Mungu na jirani! Neno hili lililetwa Altareni kwa shangwe, mwaliko kwa watawa kufanana zaidi na Kristo, Neno wa Mungu aliyefanyika mwili, kwake Yeye Bikira Maria akawa mwanadamu ili kwa njia ya Mateso, Kifo na Ufufuko wake, aweze kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.