2017-07-29 10:28:00

Siku ya Maskini Duniani 2017: Ushuhuda umwilishwe katika matendo!


Baba Mtakatifu Francisko anaanza kuandika ujumbe wake kwa Siku ya Kwanza  ya Maskini Duniani inayoadhimishwa Jumapili ya 33 ya Kipindi cha Mwaka wa Kanisa na itakuwa ni tarehe 19 Novemba 2017 kwa kusema, “Watoto wadogo, tusipende kwa neno, wala kwa ulimi, bali kwa tendo na kweli”. Kauli mbiu ya maadhimisho haya ambayo kimsingi ni matunda ya Jubilei ya Mwaka Mtakatifu wa Huruma ya Mungu ni “Tusipende kwa neno bali kwa tendo”. Hii ni amri ambayo Kristo Yesu amewaachia wafuasi wake kuitekeleza kwa vitendo kwa kuiga mfano wa Yesu mwenyewe sanjari na kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amewapenda kwanza kiasi hata cha kutoa uhai wake kwa ajili ya wokovu wa dunia.

 

Baba Mtakatifu anasema, upendo wa namna hii unahitaji jibu makini, kwani umemiminwa bila madai yoyote na uko tayari kuwasha moyo kwa mwamini yoyote licha ya dhambi na mapungufu ya kibinadamu. Hili linawezekana ikiwa kama neema ya Mungu na upendo wenye huruma unapokelewa moyoni na kusaidia kuongoza utashi na vionjo vya upendo kwa Mungu na jirani! Huruma ya Mungu inabubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu kiasi cha kuweza kupenya katika maisha ili kuibua huruma na matendo ya huruma kwa ajili ya wahitaji zaidi! Baba Mtakatifu anaendelea kusema, Kanisa daima limekuwa likisikiliza na kujibu kilio cha maskini na wahitaji kama inavyoshuhudiwa kwenye Kitabu cha Matendo ya Mitume, kwa kuwachagua Mashemasi saba walioshuhudiwa kuwa wema, wenye kujawa na Roho na hekima, ili waweze kutoa huduma kwa maskini, hii ni alama ya kwanza ya huduma kwa maskini kutokana na utambuzi kwamba, maisha ya Kikristo yanafumbatwa katika udugu na mshikamano. Yesu mwenyewe aliwapatia maskini kipaumbele cha kwanza katika Heri za Mlimani kwa kusema, “Heri maskini, maana hao watairithi nchi. Jumuiya ya kwanza ya Wakristo iliuza mali na vitu vyao na kuwagawia watu kadiri ya mahitaji yao!

Mwinjili Luka anatoa kipaumbele cha kwanza katika Injili yake matendo ya huruma, changamoto kwa waamini hata katika nyakati hizi kuwa ni mashuhuda wa huruma ya Mungu.  Mtume Yakobo anaonya tabia ya kuwapendelea matajiri kwa kuwavunjia heshima na kuwabeza maskini, lakini hawa ndio matajiri wa imani na warithi wa ufalme wa Mungu! Anakumbusha kwamba, imani bila matendo imekufa! Baba Mtakatifu anakiri kwamba, kuna wakati katika historia ya Kanisa, waamini walimezwa na malimwengu, lakini Roho Mtakatifu akawasaidia kukumbatia mambo msingi, kiasi cha kuibua waamini ambao walijisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa maskini. Wakaandika historia ya Ukristo kwa unyenyekevu na kiasi; kwa ukarimu na upendo; wakawahudumia ndugu zao maskini kwa ari na moyo mkuu.

Mtakatifu Francisko wa Assisi ni kati ya mifano bora ya kuigwa katika huduma ya ukarimu na upendo kwa maskini, hakuridhika kuukumbatia umaskini na kutoa sadaka kwa wakoma, bali aliamua kwenda kuishi pamoja nao kule Gubbio na huko akamwongokea Mungu na kuonja huruma yake iliyomletea mageuzi makubwa katika maisha yake; mageuzi yaliyojikita katika upendo, mtindo wa maisha ya Wakristo! Baba Mtakatifu anawaalika waamini kujenga utamaduni wa kukutana na kushirikishana na maskini huruma na upendo wao, hali ambayo inapaswa kuwa ni mtindo wa maisha ya Kikristo. Hija ya maisha ya mwamini katika sala, toba na wongofu wa ndani inafumbatwa katika huduma makini kwa maskini kama njia ya kukutana na uso kwa uso na Fumbo la Mwili wa Kristo, unaonyanyasika kutokana na umaskini, kama wakati ule wa kupokea Fumbo la Ekaristi Takatifu.

Baba Mtakatifu anawaambia waamini ikiwa kama kweli wanataka kukutana vizuri na Kristo Yesu katika maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, kuna haja ya kuguswa na umaskini wa Fumbo la Mwili wa Kristo, ili kwamba, Mkate uliomegwa wakati wa maadhimisho ya Liturujia ya Kanisa unamwilishwa katika huduma makini kwa maskini na wanyonge zaidi. Waamini wawe na ujasiri wa kumwabudu Kristo Yesu kati ya maskini, wanyonge na wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii wakiteseka kwa joto na baridi kali! Waamini wanahamasishwa na Mama Kanisa kujenga mshikamano wa upendo na maskini kwa kuwatembelea, kuwapenda na kuwathamini ili kuvunjilia mbali mzunguko wa upweke katika maisha. Huu ni mwaliko wa kutoka katika mazoea ili kuonja na kuthamini fadhila ya umaskini kutoka katika undani wake.

Baba Mtakatifu Francisko anakumbusha kwamba, kwa wafuasi wa Yesu, ufukara ni wito na njia ya kumfuasa Yesu fukara, ili kuambata heri na Ufalme wa Mungu. Ufukara unaonesha moyo wa unyenyekevu, unaomwezesha mtu kujipokea na kujikubali jinsi alivyo: kwa karama na mapungufu yake ili kuvuka kishawishi cha kujisikia kuwa ni miungu wadogo. Ufukara humwezesha mwamini kushinda kishawishi, tamaa na uchu wa mali, fedha na madaraka kama nyenzo msingi za kufikia furaha ya kweli. Ufukara humwezesha mwamini kuwa huru kutekeleza dhamana na majukumu yake binafsi na katika jumuiya licha ya mapungufu yake ya kibinadamu kwa kumtumainia Mwenyezi Mungu anayemwinua kwa neema. Ufukara umwezesha mwamini kutumia vyema mali ya dunia, kwa kushuhudia upendo. Mtakatifu Francisko wa Assisi ni mfano bora wa kuigwa katika ufukara, kwani alibahatika kumwona na kumhudumia Kristo Yesu kati ya maskini. Ili kuleta mageuzi ya maendeleo endelevu katika jamii kuna haja ya kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wanaoishi katika miji na kwamba waamini kamwe wasipoteze maana ya ufukara wa Kiinjili, unaoacha chapa ya kudumu katika maisha yao!

Kuna mambo mengi yanayochangia kuenea kwa umaskini duniani unaoendelea kujionesha katika nyuso za watu mbali mbali wanaoteseka na kunyanyaswa kutokana na vita, ghasia na machafuko ya kijamii; wanafungwa bila kuhukumiwa! Ni watu wanaonyimwa uhuru na utu wao; wanateseka kwa ujinga, magonjwa, ukosefu wa fursa za ajira, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; wanalazimika kukimbia na kuishi uhamishoni; ni watu wanaoteseka na umaskini wa hali na mali; wanalazimika kukimbia nchi zao. Umaskini unajionesha katika sura ya watu wanaoteseka na kunyanyaswa utu na heshima yao kutokana na utawala dhalimu na uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka. Umaskini ni matokeo ya ukosefu wa haki jamii; mmong’onyoko wa tunu msingi za kimaadili; chuki na uhasama pamoja na hali ya kutowajali wengine.

Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema kwamba, katika mazingira kama haya, kundi la watu wachache ndani ya jamii ambalo linahodhi kiasi kikubwa cha utajiri wa dunia hii, ni kashfa ya mwaka, kwani kuna mamilioni ya watu wanaoogelea katika dimbwi la umaskini! Katika hali kama hii, matokeo yake ni ukosefu wa fursa za ajira, upendeleo; inafisha ushiriki wa jamii na kutoa nafasi kwa wenye ujuzi na weledi, mambo yanayodhofisha ari na moyo wa wafanyakazi, changamoto ya kuwa na mwelekeo mpya wa maisha ya kijamii: kwa kuwapokea na kuwahudumia maskini; kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano wa kitamaduni, kidini na kitaifa kwa kuganga na kuponya madonda ya maisha ya mwanadamu bila kutegemea kurejeshewa fadhila!

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Kanisa linawajibika kimaadili kuwasaidia na kuwahudumia maskini, ndiyo maana baada ya kufunga rasmi maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya huruma ya Mungu, ameanzisha Siku ya Maskini Duniani, ili Jumuiya za Kikristo sehemu mbali mbali za dunia, ziweze kuwa alama wazi ya upendo wa Kristo kwa maskini na wahitaji. Siku hii ni muhimu sana ili kuonesha upendeleo wa Yesu kwa maskini, mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuwasikiliza, kuwahudumia na kuwaonesha maskini upendo na mshikamano, kwa kutambua kwamba, hata wao wameumbwa na wanapendwa na Baba wa mbinguni.

Siku ya Maskini Duniani, iwe ni fursa ya kushikamana kwa kujenga na kudumisha utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana, kama alama ya: urafiki, umoja na udugu unaovunjilia mbali kuta za utengano kwa sababu mbali mbali. Maadhimisho haya yakamilishwe kwa namna ya pekee Kanisa linapoadhimisha Siku kuu ya Yesu Kristo Mfalme wa Ulimwengu. Huu ni ufalme wa kweli na wa uzima; ufalme wa utakatifu na wa neema; ufalme wa haki, mapendo na amani. Ufalme wa Kristo unafumbatwa kwa namna ya pekee katika Fumbo la Msalaba ushuhuda wa utimilifu wa upendo wa Mungu, chemchem ya maisha mapya wakati wa Pasaka.

Siku ya Maskini Duniani iwe ni nafasi ya kuwaonjesha huruma na upendo maskini na wahitaji; ni siku ya kuwakaribisha na kuwakirimia wageni inayowasaidia waamini kumwilisha imani yao katika matendo; watu wawe tayari kupokea msaada na kujitahidi kuishi kwa kuzingatia mambo msingi ya maisha, daima tayari kujiachilia kwa huruma ya Mungu. Iwe ni Siku ya kumwilisha Sala ya Baba Yetu Uliye Mbinguni, ambayo kimsingi ni sala ya maskini, tayari kusikiliza na kujibu kilio cha maskini wanaohitaji mambo msingi katika maisha. Sala ya Baba Yetu inawawajibisha waamini kupokea na kugawana hata kile kidogo kilichopo, tayari kuvunjilia mbali ubinafsi, kwa kutoa nafasi ya kushirikisha furaha ya ukarimu. Siku ya Maskini Duniani iwe ni fursa makini ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; nafasi ya kutambua kwamba, maskini wanawasaidia waamini wenzao kutambua ukweli na tunu msingi za Kiinjili. Baba Mtakatifu anahitimisha ujumbe wake kwa Siku ya Kwanza ya Maskini Duniani kwa Mwaka 2017 kwa kusema, maskini si tatizo bali ni rasilimali na amana inayowasaidia waamini kupokea na kuishi misingi ya Injili!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.