2017-07-29 14:34:00

Padre Pio, mfano bora wa mchungaji mwema!


Mchungaji mwema ni yule anayejipambanua kwa kujisaka kutafuta na kuokoa kondoo waliopotea; kuwaganga kwa mafuta ya faraja wale waliovunjika na kupondeka moyo kwa kuwanyweshwa divai ya matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Ni sawa ni Baba mwenye huruma, anayesimama daima mbele ya lango la nyumba yake, akisubiri kuona dalili za Mwana mpotevu, aliyetubu na kurejea tena nyumbani, ili kuonja huruma na upendo wa Baba wa milele!

Mchungaji mwema, ni hakimu mwenye haki, ambaye hatoi hukumu yake kwa kuangalia sura, nafasi na cheo cha mtu! Hizi ni sifa ambazo Mtakatifu Padre Pio wa Pietrelcina alizionesha, akazimwilisha na kuzishuhudia katika maisha na utume wake kama Padre, lakini zaidi kama Padre muungamishaji, aliyejisadaka muda mrefu kwenye kiti cha huruma ya Mungu, ili kuwagawia watu huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Upatanisho! Haya yamesemwa hivi karibuni na Kardinali Angelo Amato, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Kuwatangaza waamini kuwa wenyeheri na watakatifu katika ibada ya maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100, tangu Padre Pio alipowasili na kuanza makazi yake kwenye Konventi ya Gargano.

Ibada hii imehudhuriwa na umati mkubwa wa familia ya Mungu kutoka ndani na nje ya Italia. Wakati wa mahubiri yake, Kardinali Angelo Amato amekazia umuhimu wa utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika mchakato wa kumwilisha “Heri za Mlimani” Muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Ni mwaliko wa kuishi kikamilifu sheria mpya ya upendo kwa Mungu na jirani; kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa uwepo wa Mungu katika maisha ya mwamini. Dhamana hii inatekelezeka kwa njia ya sala, maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, inayompatia mwamini nafasi ya kumsikiliza Mungu kutoka katika undani wa maisha yake katika hali ya ukimya, bila kusahau Tafakari ya kina ya Neno la Mungu.

Kardinali Angelo Amato anakaza kusema, yote haya aliyatekeleza kwa kuonesha utii kwa Injili ya Kristo pamoja na Sheria za Shirika lake kadiri ya wito na utume wake kama mtawa. Akatekeleza dhamana na wajibu wake barabara; akakubali kwa moyo radhi mateso na mahangaiko katika maisha yake, daima akionesha unyenyekevu na utii kwa viongozi wa Kanisa pamoja wale wa Shirika lake. Matokeo yake, ni moto mkubwa wa upendo kwa Mungu na jirani, uliowashwa na kushuhudiwa na Padre Pio. Akaonesha ukarimu wa ajabu kwa maskini, kiasi cha kuwaacha watu wengi wakiwa wamepigwa na bumbuwazi.

Daima alimwona Kristo Yesu, miongoni mwa wagonjwa na maskini na hawa akawapatia kipaumbele cha kwanza katika maisha na utume wake. Aliguswa na wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu, kiasi hata cha kutoa machozi ya furaha na shukrani kwa Mwenyezi Mungu. Miongoni mwa watawa wenzake, alikuwa ni shuhuda wa huruma, upendo na mshikamano wa dhati. Padre Pio alikuwa ni kiongozi mwenye mvuto kwa watu mbali mbali kutoka ndani na nje ya Italia. Katika maisha na utume wake, watu walionja ile sura ya Kristo Mchungaji mwema; wakaona mwanga wa matumaini katika shida na mahangaiko yao; wakapata faraja kwa kushiriki maadhimisho ya  Mafumbo mbali mbali ya Kanisa.

Sakramenti za Kanisa zikatumika kutibu na kuganga makovu ya maisha ya kiroho ya wale wote waliokuwa wanateseka; kwa hali hii, akawa ni mkate uliomegwa kwa ajili ya maskini; divai, iliyowarejeshea furaha wadhambi waliotubu na kumwongokea Mungu. Maadhimisho ya Sakramenti za Kanisa kwa Padre Pio, ilikuwa ni fursa ya kuwafunda waamini na kuwapatia malezi ya maisha ya kiroho sanjari na kuwapatia furaha ya ndani, iliyokuwa inabubujika kutoka kwa Kristo Yesu. Aliwaonesha waamini dira na mwongozo wa kufuata ili kurejea tena nyumbani kwa Baba mwenye huruma kwa kukazia toba, wongofu wa ndani na upatanisho. Kwa hakika, Padre Pio alikuwa ni Baba wa upatanisho, toba na wongofu wa ndani, mfano bora wa kuigwa katika utakatifu wa maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.