2017-07-26 14:59:00

Changamoto ya ulinzi na usalama Mashariki ya Kati na Palestina


Jumuiya ya Kimataifa haina budi kufanya maamuzi magumu kuhusu hali ya Wapalestina pamoja na changamoto zinazoendelea kujitokeza huko Mashariki ya Kati; hasa kwa kutafuta suluhu ya kudumu ya mgogoro kati ya Israeli na Palestina, unaotishia: usalama, amani na mafungamano ya kijamii huko Mashariki ya Kati. Ujumbe wa Vatican unaendelea kukazia umuhimu wa kuwa na Nchi mbili zinazojitegemea yaani, Nchi ya Israeli na Nchi ya Palestina, ili kukata mzizi wa fitina ambao umekuwa ni chanzo cha ghasia na uvunjifu wa amani. Juhudi hizi zinapaswa kwenda sanjari na utambuzi wa mipaka ya nchi hizi mbili kimataifa, ili iweze kuheshimiwa na kuthaminiwa na wote.

Ili kuweza kufikia hatua hii, kuna haja kwa Israeli na Palestina kushusha jazba za kisiasa kwa kudhibiti vurugu na ghasia zinazoendelea kupamba moto kwa wakati huu! Huu ni mchango uliotolewa  Monsinyo Simon Kassas, Afisa kutoka Ofisi ya Uwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, wakati wa kuchangia majadiliano ya wazi kuhusu hali tete huko Mashariki ya Kati na tatizo la Wapalestina, tema iliyowasilishwa na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China.

Baba Mtakatifu Francisko tangu mwaka 2014 amekuwa mstari wa mbele kuwahamasisha viongozi wakuu wa Israeli na Palestina kujikita katika kuombea amani, kwa kukuza na kudumisha utamaduni wa majadiliano, ili kuimarisha uhai wa binadamu na kuondokana na utamaduni wa kifo! Anahimiza mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana na wala sio sera na mikakati inayopania kuwagawa na kuwatenga watu kwa sababu mbali mbali! Ujenzi wa Mataifa mawili yaani Israeli na Palestina, unawataka Wapalestina waliogawanyika kuonesha utashi wa kisiasa wa kutaka kusimamia ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Palestina.

Monsinyo Simon Kassas katika hotuba yake, Jumanne, tarehe 25 Julai 2017 anakumbusha kwamba,  Yerusalemu ni Mji Mtakatifu kwa Wayahudi, Wakristo na Waislam. Ni mji wenye historia tete inayohitaji kujadiliwa na kutolewa maamuzi kwa hekima na busara zaidi. Lengo liwe ni kuhakikisha kwamba, kunakuwepo na uhuru wa kuabudu, uhuru wa kidini jambo msingi katika kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu. Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuwahimiza viongozi wa Israeli na Palestina kuwa na kiasi na kuanza kujikita zaidi katika majadiliano, ili hatimaye upatanisho na amani, viweze kutawala kati ya watu wa Mataifa.

Monsinyo Simon Kassas anasikitika kusema kwamba, vita, ghasia, nyanyaso na mipasuko ya kijamii huko Mashariki ya Kati imelata maafa makubwa kwa wananchi wa Siria, Yemen na Iraq ambako hali ni ngumu sana inayohitaji suluhu ya kisiasa, kwa kuzingatia Makubaliano yaliyofikiwa mjini Geneva tarehe 30 Juni 2012. Watu wapatiwe makazi ya kudumu; wakimbizi na wahamiaji wawezeshwe kurejeshwa nchini mwao kwa amani na hivyo kuanza mchakato wa haki, amani, upatanisho na msamaha!

Viongozi wa kisiasa wasimame kidete kupambana na mazingira yanayozalisha makundi ya kigaidi sanjari na kuanza mchakato wa ujenzi wa mshikamano na mafungamano ya wananchi wote wa Siria. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusaidia mchakato wote huu, ili kwamba, utawala wa sheria, uhuru wa kidini na kuabudu; usawa na heshima kwa raia wote vinakuzwa na kudumishwa. Mchakato wa amani unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza badala ya kukimbilia mtutu wa bunduki. Utawala bora, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi ni mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga kwa ajili ya kupata suluhu ya changamoto zilizoko huko Mashari ya Kati.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.