2017-07-25 14:08:00

Paulo VI: Miaka 49 ya "Humanae Vitae": Waraka wa Maisha ya Binadamu


Mwenyeheri Paulo VI hapo tarehe 25 Julai 1968 alichapisha Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu”. Ni waraka wa kinabii unaobainisha dhamana na wajibu wa wanandoa wanaoushiriki katika kazi ya uumbaji, ili kuendeleza zawadi ya maisha kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Ni dhamana ambayo inapaswa kujikita katika maisha na furaha ya wanandoa katika maisha na utume wao ndani ya familia. Papa Paulo VI alikuwa na upeo mpana na uwezo wa kuona mbali, akagundua changamoto na vikwazo vinavyowakabili wanandoa; akabainisha wajibu wa Kanisa kama Mama na Mwalimu.

Mwenyeheri Paulo VI katika Waraka huu wa kitume, alipembua kanuni maadili na Mafundisho ya Mama Kanisa kuhusu mwono na maisha ya mwanadamu tangu pale anapotungwa mimba hadi pale mauti ya kawaida yanapomfika kadiri ya mpango wa Mungu. Akakazia kwa namna ya pekee, wajibu wa wazazi katika kushiriki kazi ya uumbaji, kulea na kutetea zawadi ya maisha, kwa kuheshimu mpango wa uzazi kwa njia ya asili. Kwa njia hii, wanandoa wanaweza kuwa kweli waaminifu katika tendo la ndoa na mbele ya Mwenyezi Mungu, kwa kukataa kishawishi cha kukumbatia utamaduni wa kifo, unaofumbatwa katika vitendo vya utoaji na uzuiaji mimba.

Kanisa linakazia umuhimu wa waamini kuambata kanuni maadili na utu wema; mambo yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao kama kielelezo cha imani inayomwilishwa katika matendo. Kanisa linapenda kuwaona waamini wake wakiwa makini kushuhudia Injili Familia inayoambata Injili ya Uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Waraka  wa “Maisha ya binadamu” unapaswa sasa kusomwa pia kwa mwanga wa “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya Injili ndani ya familia” ambao umechapishwa hivi karibuni na Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa: Injili ya Familia, Injili ya Uhai, Utu na heshima ya binadamu. Papa Francisko anapembua kuhusu wito wa familia; umuhimu wa upendo ndani ya familia; upendo unaozaa upendo kwa kujenga madaraja ya watu kukutana na kusaidiana; kwa kuenzi na kudumisha udugu na mshikamano. Anakazia umuhimu wa malezi na majiundo makini kwa watoto, bila kusahau changamoto zinazowakabili wanandoa.

Mwenyeheri Paulo VI aliona changamoto hizi, akazivalia njuga, kiasi cha kubaki peke yake akikabiliwa na kinzani kutoka ndani na nje ya Kanisa. Aliwataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kutambua na kuheshimu Injili ya Uhai kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Huu ni mwaliko wa kukata katu katu kukumbatia utamaduni wa kifo unaojielekeza hata wakati mwingine wa kutaka kupata mtoto kwa gharama yoyote ile. Matokeo yake ni baadhi ya wanawake kugeuzwa kuwa ni maabara ya kuzalisha watoto kwa njia ya chupa! Hapa kuna hatari ya watoto kugeuzwa kama bidhaa inayoweza kupatikana sokoni ikiwa kama mtu ana jeuri ya “vijisenti” vyake, au “vijisenti vya mboga”.

Lakini ikumbukwe kwamba, mtoto ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu, ni matunda ya upendo kati ya bwana na bibi katika kifungo cha ndoa, kadiri ya Mafundisho ya Kanisa. Upendo katika maisha ya ndoa na familia unajikita katika uhuru, wajibu na utashi kamili. Hapa si mambo ya mtu kujisikia tu! Waraka huu haukupokelewa kwa mikono miwili, hali ambayo hata Mwenyeheri Paulo VI alitambua fika kwamba, angekumbana nayo, lakini akasimama kidete kutangaza Injili ya Uhai inayojikita katika utu na heshima ya binadamu kadiri ya mpango wa Mungu.

Papa Paulo VI alionesha dhamana na wajibu wa Kanisa katika kulinda, kutetea sanjari na kuendeleza maisha ya mwanadamu bila kuogopa. Binadamu anapaswa kupewa heshima na kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo ya binadamu na kamwe asigeuzwe kuwa ni kichokoo cha tamaa za kibinadamu. Ndoa iwe ni kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa mwanadamu unaowajibisha na unaopania kuendeleza kazi ya uumbaji kadiri ya mpango wa Mungu! Waraka wa Kitume: “Humanae vitae” yaani “Maisha ya binadamu” unapaswa kusomwa pia katika mwanga wa Waraka wa Mtakatifu Yohane Paulo II: Injili ya uhai sanjari na Waraka wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Furaha ya Injili ndani ya familia”. Hizi ni nyaraka zinazoshibana na kukamilishana katika kutangaza Injili ya uhai inayofumbatwa katika tunu msingi za Injili ya familia, kwa ajili ya kumsaidia mwanadamu kushiriki kikamilifu katika mpango wa kazi ya uumbaji!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.