2017-07-25 10:43:00

Papa Francisko anawaalika watu kuungana naye kumwombea Mtoto Charlie


Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kusali kwa ajili ya kumwombea mtoto Charlie Gard, mwenye umri wa miezi kumi na moja, ambaye anasumbuliwa na ugonjwa hadimu sana ambao tayari umekwisha sababisha madhara makubwa kwenye misuli yake, hali ambayo inafunga tena dirisha la matumaini ya kuweza kupata tiba ya majaribio iliyokuwa itolewe na madaktari bingwa wa watoto nchini Marekani. Baba Mtakatifu anawaombea wazazi wa mtoto Charlie Gard katika kipindi hiki kigumu cha mahangaiko ya ndani.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuungana pamoja naye kwa ajili ya kumwombea mtoto Charlie Gard na wazazi wake faraja na upendo kutoka kwa Mwenyezi Mungu, mweza wa yote! Haya yamesemwa na Dr. Greg Burke, Msemaji mkuu wa Vatican ambaye anafafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko tangu mwanzo wa kesi hii, amekuwa akiifuatilia kwa karibu sana kiasi cha kuonesha uwezekano wa Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuongozwa na Vatican kuweza kutoa tiba ya majaribio, lakini wazo hili likashindikana kutokana na urasimu wa kisheria.

Kwa upande wake, Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, linapenda kuungana na familia ya mtoto Charlie Gard katika kipindi hiki kigumu cha historia na maisha yao, ili kuwaonjesha huruma, upendo na faraja. Wanawapongeza wazazi wa mtoto Charlie Gard waliosimama kidete kuhakikisha kwamba, mtoto wao anapata tiba muafaka, ili kuokoa maisha yake. Huu ni mfano bora wa kuigwa na watu wote wenye mapenzi mema kwa kusimama kidete kulinda, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo.

Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, kwamba, familia hii itaweza kupata msaada wa hali na mali, ili kuweza kudumisha amani na utulivu wa ndani baada ya malumbano ya kisheria mahakamani. Uamuzi wa kumwachia Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na faraja, maisha ya mtoto wao Charlie Gard mikononi mwake, kwa machozi ya uchungu na upendo mkuu ni kitendo ambacho kumewagusa watu wengi, akiwemo Baba Mtakatifu Francisko. Maisha ya mtoto Charlie Gard yataendelea kurutubishwa hadi pale Mwenyezi Mungu atakapoamua kumwita mja wake, ili aweze kupumzisha katika usingizi wa amani, miongoni mwa wateule wake!

Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales linasema, huu ni wakati muafaka kabisa wa kuwakumbuka na kuwaombea wale wote waliohusika katika mchakato wa kufanya maamuzi machungu juu ya hatima ya maisha ya mtoto Charlie Gard! Ni watu ambao daima walitaka kutenda kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya mgonjwa mwenyewe. Katika kipindi chote hiki: weledi, upendo na huduma makini kwa Charlie Gard zimeoneshwa na kushuhudiwa kwenye Hospitali ya “Great Ormond Street” iliyoko Jijini London. Juhudi zao za kutaka kuokoa maisha ya mtoto Charlie Gard zinapaswa pia kupongezwa wanasema Maaskofu Katoliki Uingereza na wales. Wazazi wa mtoto Charlie Gard wanasikitika kusema kwamba, pengine mtoto wao mpendwa hataweza kuendelea kuishi zaidi ya majuma mawili kuanzia sasa kutokana na madhara makubwa aliyo nayo kwenye misuli yake! Kwa majonzi makubwa wanasema, wameamua kumwachia Mwenyezi Mungu hatima ya maisha ya mtoto wao, ili aweze sasa kupumzika kwa amani, baada ya mapambano ya kisheria mahakamani ili kutaka mtoto wao apewe fursa ya kutibiwa hata nje ya Uingereza kutoweka taratibu kama mshumaa unaowaka kwenye upepo mkali!

Katika kipindi hiki kigumu katika historia na maisha yao kama wana familia, wanapenda kwa namna ya pekee kabisa, kuonesha ukaribu wao kwa mtoto wao mgonjwa hadi ile dakika ya mwisho, atakapoitupa mkono dunia, kadiri ya mapenzi ya Mungu! Wataka kusimama kidete, kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai, dhidi ya utamaduni wa kifo! Bwana Chris Gard na mkewe Connie Yates, wamekubali kuupokea mpango wa Mungu katika maisha ya mtoto wao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.