2017-07-22 09:22:00

Saratani ya rushwa na ufisadi inavyoisambaratisha jamii!


Kardinali Peter Turkson amefanikiwa kuchimbua mizizi ya maeneo yanayoweza kuchochea kishawishi cha rushwa na ufisadi. Ameanza katika maisha ya kiroho, yaani kutoka katika undani wa mtu mwenyewe na kupanua wigo huu katika maisha ya kijamii, kisiasa, kitamaduni na kiuchumi sanjari na kuelezea dhamana na wajibu wa Mama Kanisa katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi, saratani inayopekenyua maisha ya mataifa mengi duniani, kiasi cha kukwamisha: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Hii ni changamoto pevu katika maisha, utume na utambulisho wa Kanisa, ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika dibaji ya kitabu kuhusu “Rushwa” kilichoandikwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu baada ya kufanya mahojiano na Bwana Vittorio V. Albert. Kardinali Turkson anasema, Kanisa halina budi kuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi; uhalifu wa magenge kitaifa na kimataifa. Ili kufanikisha mapambano haya, rushwa haina budi kushughulikiwa kama “chuma chakavu” ndani ya Kanisa kwa kujikita katika: kanuni maadili, utu wema sanjari na kuambata tunu msingi za Kiinjili. Kwa njia hii, Kanisa litaweza kuongoza mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi. 

Lakini kwanza kabisa, Kanisa halina budi kuwa safi pasi na mawaa wala makunyanzi ya rushwa na ufisadi. Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, rushwa ni mchakato unaoharibu na kuvunjilia mbali kabisa mafungamano,upendo na mshikamano wa binadamu. Rushwa inatia doa uhusiano kati ya binadamu, Mwenyezi Mungu na kazi ya uumbaji. Lakini kinyume cha rushwa ni: Uaminifu, uadilifu, utu wema, upole na unyofu wa moyo mambo yanayopania kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Rushwa inaonesha maisha ya mwanadamu asiyekuwa na  dira wala mwelekeo sahihi wa maisha, hali inayoharibu sana mafungamano ya kijamii. Matokeo yake ni kukomaa kwa ubinafsi usiokuwa na mvuto wala mashiko; tabia ya kutowajali wengine. Rushwa inaonesha ile roho ya korosho, roho ya kwa nini; roho ya kutu, roho iliyovunda na kuanza kutoa harufu mbaya. Rushwa ni kikwazo katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Rushwa inapelekea kushamiri kwa biashara haramu ya binadamu na mifumo yote ya utumwa mamboleo. Ni chanzo kikuu cha kuibuka na kusambaa kwa magenge ya kihalifu, kitaifa na kimataifa; magenge yanayochochea utamaduni wa kifo.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, ili kupambana na rushwa pamoja na ufisadi kuna haja ya kuwajengea vijana uwezo wa kiuchumi, kimaadili, kitamaduni na kiutu! Hii inatokana na ukweli kwamba, rushwa inapata chimbuko lake katika moyo wa mwanadamu! Rushwa ina tabia ya kujigeuza geuza kadiri ya mazingira na vionjo vya mtu, kumbe, hakuna anayeweza kujidai kwamba, rushwa ameipatia kisogo! Jambo la msingi ni kuwa macho na makini; kwa kukesha na kusali, ili kutokutumbukia majaribuni!

Kanisa ni mama na mwalimu wa tabia ya kimaadili na utu wema. Ni sauti ya kinabii inayotetea haki, kupinga na kukemea mambo yasiyo ya haki. Kanisa linahimiza umuhimu wa kumwilisha Injili ya huruma, upendo, mshikamano na udugu kwa watu wote. Kanisa linapenda kusimama kidete, kulinda na kuwatetea maskini, wajane, yatima na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha. Kwa namna ya pekee, Kanisa linaitwa kujenga na kuimarisha Ufalme wa Mungu hapa duniani kwa kusaidia kuunga mkono sera za kiuchumi, kisiasa na kijamii zinazokuza na kudumisha: haki, amani, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Sera na mikakati inayopania kulinda utu na heshima ya binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu; mambo ambayo yanapata mwanga wake katika Maandiko Matakatifu na Mafundisho Jamii ya Kanisa.

Kimsingi, Mafundisho Jamii ya Kanisa yanafumbatwa katika utu wa binadamu, ustawi, maendeleo endelevu na mafao ya wengi; udugu na mshikamano; ushiriki wa watu katika kupanga, kuamua na kutekeleza sera na mikakati mintarafu mustakabali wa maisha yao kwa kuzingatia kanuni auni! Ni mafundisho yanayojikita hasa katika misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi, kwa kuzingatia pia utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, kama sehemu ya mchalato wa mwendelezo wa kazi ya Uumbaji ambayo binadamu amekabidhiwa na Mwenyezi Mungu. Huu ndio mwongozo rasmi wa maisha na utume wa Kanisa katika masuala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na hata katika masuala ya kidini!

Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Kusini mwa Afrika, SACBC, inasema rushwa ni saratani inayokwamisha na kukatisha tamaa mchakato na jitihada za kusukuma mbele gurudumu la maendeleo endelevu ya binadamu. Rushwa inawajengea watu uchu wa mali na madaraka kwa njia za mkato, inachafua na kudhohofisha kabisa mafungamano ya kijamii kwa kuunda matabaka ya watu wanaothaminiwa kutokana na uwezo wao wa kifedha na wale wanaodharauliwa kwa sababu si “mali kitu”. Hapa utu na heshima ya binadamu vinapimwa si kutokana utu na heshima yake kwa vile ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu bali kwa ni kwa sababu anayo fedha na madaraka! Umefika wakati kwa wananchi wa Afrika ya Kusini kukataa katu katu rushwa kuwa ni sehemu ya vinasaba na utambulisho wao kijamii, kwani rushwa ni adui wa haki! Watu wawe na ujasiri wa kukemea na kupambana na rushwa, ili kuondoa uovu ndani ya jamii na hatimaye, kuduisha haki, amani, upendo na mshikamano. Huu ni ujasiri wa kutaka kukuza na kudumisha kanuni maadili, miiko ya kazi na utu wema; kwa kukuza sheria, nidhamu na misingi ya utawala bora.

Rushwa ina madhara makubwa katika maisha ya wananchi kwani inapunguza umaarufu wa viongozi kama inavyoendelea kujitokeza nchini Afrika ya Kusini, kiasi kwamba, wananchi wamekosa imani kwa Rais Jacob Zuma na wanataka aachilie ngazi kutokana na shutuma za rushwa na ufisadi wa mali ya umma zinazomwandama kwa sasa, ingawa anakingiwa kifua na Chama cha A.N.C. Rushwa inapelekea wananchi kujenga hasira dhidi ya serikali yao na haya ndiyo yanayoendelea kujitokeza Afrika ya Kusini kwa maandamano yasiyo koma. Rushwa inashusha kiwango cha maadili, hali ya kuaminiana, inapotosha utu na heshima ya binadamu inakuza na kudumisha ubinafsi, uchu wa fedha, tamaa ya mali na madaraka!

Tume ya haki na amani ya Baraza la Maaskofu Kusini mwa Afrika inasema, kwa hakika rushwa imekuwepo katika maisha ya wananchi wa Afrika ya Kusini, lakini ni jambo lisilofumbiwa macho kusema kwamba, rushwa imeongezeka maradufu wakati wa uongozi na utawala wa Rais Jacob Zuma. Huu ni utawala ambao umeshikamana sana na wafanyabiashara maarufu na matokeo yake ni ufisadi kupiga hodi Ikulu ya Afrika ya Kusini. Rais Zuma amefanya ukarabati mkubwa wa makazi yake ambayo yameligharimu taifa kiasi kikubwa cha fedha, hizi ni dalili za Saratani ambayo inaendelea kuwapekenyua wananchi wa Afrika ya Kusini pasi na huruma hata kidogo.

Vituo vya huduma ya elimu na afya, vimegeuzwa kuwa ni mahali pa watu kuombea rushwa. Umefika wakati kwa wafanyakazi wa Umma nchini Afrika ya Kusini, kufanya uamuzi wa busara na wa haki kwa kung’atuka kutoka madarakani, wale wote wanaohusishwa na tuhuma za rushwa nchini Afrika ya Kusini! Tume ya Haki na Amani ya Baraza la Maaskofu Kusini mwa Afrika inakiomba Chama cha A.N.C wakati wa mchakato wa uchaguzi mkuu kunako mwaka 2019 kuhakikisha kwamba, kinasimamisha mgombea urais safi na jasiri, atakayethubutu “kufukua makaburi” ya rushwa na ufisadi wakati wa utawala na uongozi wa Rais Jacob Zuma, ili haki iweze kushika mkondo wake! Rushwa itaweza kupewa kisogo kwa wananchi kujikita katika kanuni maadili na utu wema; kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; kwa kurekebisha sheria, kanuni na mianya inayoshabikia na kukoleza rushwa katika uongozi na huduma mbali mbali. Kiwango cha taaluma na uwajibikaji kipewe msukumo wa pekee kabisa! Wananchi wamechoshwa na maumivu ya Saratani ya rushwa nchini Afrika ya Kusini.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.