2017-07-22 14:18:00

Mkazo wa kichungaji: Furaha ya Injili na familia; mazingira na utu!


Kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili; Umoja na mshikamano wa familia ya Mungu; huruma na upendo ni kati ya vipaumbele vinavyofanyiwa kazi na Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, aliyechaguliwa hivi karibuni. Katika mahojiano maalum na Radio Vatican anakazia umuhimu wa kujikita katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, kwa kutoa nafasi ya kuokoa maisha pale inapowezekana kwa msaada wa maendeleo ya sayansi na tiba ya binadamu.Kamwe, watu wasimezwe sana na ubinafsi na uchoyo unaohatarisha hata mafungamano ya kijamii kama ilivyojitokeza kwa kesi ya mtoto Charlie Gard, ambaye anasumbuliwa na ugongwa wa nadra sana duniani na kwamba, Uingereza tayari imekwishamkatia tamaa ya maisha na wala haitaki kutoa nafasi kwa watu wengine kujaribu kuokoa maisha yake kwa sababu za ukiritimba usiokuwa na mashiko wala mvuto!

Kardinali Gualtiero Bassetti anasema, Baba Mtakatifu Francisko katika utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro amelizawadia Kanisa nyaraka tatu kuu za kitume yaani: Furaha ya Injili, inayowahamasisha waamini kutoka kifua mbele ili kutangaza na kushuhudia Furaha ya Injili kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto unaosimikwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha imani tendaji! Huu ni mchakato wa uinjilishaji unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili.

Umoja, upendo na mshikamano kati ya familia ya Mungu nchini Italia, Kanisa, Mwenyezi Mungu na kazi ya uumbaji ni mambo yanayofafanuliwa kwa kina na mapana na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa kitume, “Laudato si” yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”. Huu ni umoja unaofumbatwa katika majadiliano ya kina: katika ukweli na uwazi; kwa njia ya urika wa Maaskofu kati yao pamoja na familia nzima ya Mungu nchini Italia, ili kujenga na kudumisha Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa. Huu ni mwaliko wa kujiweka chini ya ulinzi na maongozi ya Roho Mtakatifu katika hali ya unyenyekevu, ili aweze kuliongoza Kanisa kadiri anavyotaka!

Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye  mapenzi mema kujenga na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia katika Waraka wake wa kitume, “Furaha ya upendo ndani ya familia”. Huu ni waraka unaojikita katika tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, umuhimu wake, changamoto na fursa zilizopo katika mchakato wa maboresho ya maisha ya ndoa na familia. Hapa pia kuna haja ya kugusia kazi kama kielelezo cha utimilifu wa utu na heshima ya binadamu; changamoto za ukosefu wa fursa za ajira hasa miongoni mwa vijana pamoja na changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ambao wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa kama binadamu.

Kanisa Katoliki nchini Italia, hivi karibuni limekuwa na fursa ya kupitia tena na tena maisha ya viongozi mashuhuri kama Mtumishi wa Mungu Giorgio La Pira, ambaye, Kanisa linakumbuka miaka 40 tangu alipofariki dunia na mchango wake katika kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kwa kuthamini utu na heshima ya binadamu kama sehemu ya mchakato endelevu wa kukutana na Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu! Kristo anaye endelea kujisadaka katika maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu. Ni mtumishi wa Mungu ambaye alicheza vyema katika uwanja wa kisiasa kama Meya wa Jiji la Firenze.

Viongozi wengine wa Kanisa ni Padre Primo Mazzolari pamoja na Padre Lorenzo Milani; watu ambao walikuwa na karama na tabia tofauti kati yao, lakini wakaunganishwa na kushikamanishwa na kifungo cha upendo kwa ajili ya maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii! Kwao huduma ya elimu makini ulikuwa ni funguo wa maisha bora kwa vijana wengi waliokuwa wanatoka katika familia maskini zaidi nchini Italia! Watoto wa maskini wakiwezeshwa kwa njia ya elimu bora, wanaweza kuupatia umaskini na ujinga kisogo na kuanza kucharuka katika maendeleo endelevu: kiroho na kimwili!

Kardinali Gualtiero Bassetti anasema anaunga mkono jitihada za Baba Mtakatifu za kuwataka Maaskofu kudumisha uhusiano na mafungamano ya karibu zaidi na mapadre wao, kwa kutambua kwamba, wao ni wasaidizi wao wa karibu! Waoneshe ubaba na udugu katika maisha na utume wao. Wawajali na kuwahudumia mapadre na majandokasisi ambao wanajiandaa kwa ajili ya kujisadaka kwa Mungu na jirani. Maaskofu wajenge na kudumisha maisha ya kijumuiya na mapadre wao, wakitoa mfano bora wa kuigwa ili kuondokana na upweke unaoweza kuwapekenya huko kwenye Makao makuu ya Jimbo. Kuwa askofu maana yake ni kujisadaka maisha yako yote kwa ajili ya huduma ya upendo kwa Kristo na Kanisa. Kardinali Gualtiero Bassetti anakumbuka kwa heshima kubwa tarehe 8 Septemba 1994 alipowekwa wakfu kuwa Askofu mikononi mwa Kardinali Silvano Piovanelli.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.