2017-07-22 14:31:00

Huduma kwa wakimbizi na wahamiaji: mafungamano ya kifamilia!


Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia, linaendelea kuunda maisha ya watu wengi duniani: kijamii, kisiasa na kiuchumi. Ili kuweza kukabiliana na changamoto kubwa kama hii, kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inakuwa ni mbinu mkakati wa kuwashirikisha wahamiaji na wakimbizi hawa katika shughuli za maisha ya jamii inayowapatia hifadhi; kwa kuzingatia: utu na heshima ya binadamu. Huu ni mwaliko wa kuondokana na tabia ya ubaguzi wanayotendewa baadhi ya wahamiaji kutokana na mahali wanakotoka au dini yao!

Haya yamesemwa hivi karibuni na Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa yaliyoko mjini Geneva kama sehemu ya mchango wa Vatican katika majadiliano ya Shirika la Kimataifa la Wahamiaji, (IOM) kuhusu: umuhimu wa kufahamu hali tete wanayokabiliana nayo wakimbizi na wahamiaji na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kudumisha utu na heshima yao! Makundi yasiyokuwa na ulinzi wa kutosha; yasiyoweza kusimamia haki zao msingi wala kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi ndiyo yanayoathirika vibaya. Licha ya mchanganuo wote huu, lakini jambo la msingi linalopaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ni utu na heshima ya binadamu. Hapa mtu mzima: kiroho na kimwili anapaswa kulindwa.

Mtazamo mzima wa safari ya wakimbizi na wahamiaji unapaswa kuangaliwa kwa dhati kabisa kwa kufanya upembuzi yakinifu kuhusu sababu zinazopelekea makundi ya watu kuzikimbia nchi zao; ili Jumuiya ya Kimataifa iweze kutoa msaada unaohitajika katika hatua mbali mbali za safari yao hadi siku ile hali itakavyoboresha na kutengeneza mazingira ya kuweza kurejea tena salama salimini katika nchi zao za asili. Kutokana na changamoto hii, Baba Mtakatifu Francisko anapenda kuialika Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, wakimbizi na wahamiaji pamoja na watu wanaotafuta hifadhi ya kisiasa; haki zao msingi, utu na heshima yao kama binadamu zinalindwa na kudumishwa na wote pasi na ubaguzi.

Baba Mtakatifu anafafanua kwamba, kuna sababu mbali mbali ambazo zinapelekea watu kukimbia au kuzihama nchi zao. Kati ya sababu msingi ni umaskini; ukosefu wa usawa; unyonyaji, ukosefu wa fursa za ajira; mifumo mbali mbali ya kibaguzi; dhuluma na nyanyaso; vita, kinzani na mipasuko ya kijamii pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi. Wakimbizi na wahamiaji mara nyingi wanajikuta wakiwa katika hali tete kiasi kwamba, haki zao msingi, utu na heshima yao kama binadamu havithaminiwi tena.

Mshikamano wa kifamilia ni jambo la msingi sana katika majadiliano kuhusu haki za wakimbizi na wahamiaji. Licha ya changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika kuwahifadhi wakimbizi na wahamiaji, lakini pia wao ni nguvu kazi inayotumiwa kuzalisha mali na huduma. Si rahisi sana mtu kuacha familia, nchi na utamaduni wake na kuamua kuzamia ughaibuni, hali inayowafanya kuwa katika mazingira magumu kwanza kabisa kama wakimbizi pamoja na familia walizoziacha nyuma yao. Kumbe, watu hawa wanapokuwa ugenini wanahitaji walau kuonjeshwa heshima, upendo na kuwajali kama binadamu, licha ya shida na magumu yanayowaandama. Katika kuunda mwelekeo mpya wa Jumuiya ya Kimataifa kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji, tunu msingi za maisha ya kifamilia zinapaswa pia kuzingatiwa na wote.

Kwa njia hii, wakimbizi na wahamiaji wanaweza kuchangia kwa kiasi kikubwa katika ustawi, mafao na maendeleo ya wengi na kwamba, dhana hii pia ni sehemu ya Malengo ya Maendeleo Endelevu ya binadamu ifikapo mwaka 2030. Ni matumaini ya ujumbe wa Vatican kwamba, wanasiasa wataonesha utashi wa kisiasa katika kutekeleza mambo msingi yanayopitishwa na mikutano ya kimataifa! Mchakato mzima wa ushirikiano unapaswa kutekelezwa kwa dhati kabisa, ili kutoa kipaumbele cha pekee kwa kanuni na haki msingi za maisha. Jumuiya ya Kimataifa haina budi kusimama kidete kuwalinda na kuwatetea wakimbizi na wahamiaji, kwani ni kwa ajili ya mafao ya Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.