2017-07-21 16:07:00

Mhandisi aliyejenga Hospitali ya Itigi, kupewa Daraja ya Upadre!


Askofu Douglas Regattieri wa Jimbo Katoliki la Cesena-Sarsina, lililoko nchini Italia, Jumamosi jioni, tarehe 22 Julai 2017 anatoa Daraja ya Upadre kwa Shemasi Aleandro Manzi, C.PP.S. wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Kanda ya Italia, kwenye Parokia ya Mwili na Damu Azizi ya Yesu, wakati huu, Shirika linapofanya kongamano la kimataifa kuhusu changamoto za maisha ya kijumuiya. Tayari ujumbe kutoka Tanzania unaongozwa na Padre Cesco Peter Msaga, Mkuu wa Kanda ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Tanzania umewasili nchini Italia kutia nguvu tukio hili la kihistoria ambalo linapata chimbuko lake katika ushuhuda wa huduma ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!

Jumapili, tarehe 23 Julai 2017 Alessandro Manzi mwenye umri wa miaka 47 ataadhimisha Misa yake ya shukrani kwenye Parokia ya Sant’Egidio, Jimbo Katoliki la Cesena-Sarsina. Kwa siku za hivi karibuni watu wengi wameendelea kupigwa na butwaa kuona watu walioshindikana katika mashindano ya ulimbwende duniani, watu waliotandaza kabumbu katika timu kubwa za kimataifa, wakibwaga manyanga na kuingia katika maisha ya kitawa, tayari kumtumikia Mungu na jirani zao. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Lawi mtoza ushuru, alipoangaliwa na Yesu kwa jicho la upendo na huruma, akaacha yote na kumfuasa. 

Ndivyo ilivyokuwa kwa Shemasi Alessandro Manzi, mwandisi aliyebobea alipoacha yote na kwenda kujichimbia kwenye huduma ya ujenzi wa Hospitali ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Mayoni, Singida, nchini Tanzania, wakati wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo Duniani. Akaguswa na mahangaiko ya wagonjwa kutoka sehemu mbali mbali za Tanzania, akakikiliza kilio cha damu kilichoacha chapa ya kudumu katika historia ya maisha yake. Kunako mwaka 2006 akateuliwa na Kituo cha Radio Maria kuwa ni mratibu mkuu wa shughuli za Radio Maria Barani Afrika.

Huko akaendelea kujisadaka bila ya kujibakiza na kushuhudia Radio Maria ikipanuka na kuendelea kudumisha mchakato wa uinjilishaji sehemu mbali mbali za Bara la Afrika. Tarehe 15 Agosti 2009 Alessandro Manzi, “akabwaga manyanga” na kuamua kurejea kwenye nyumba ya Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu, Tanzania. Mbegu ya wito wa kitawa ikaendelea kukua na kupaliliwa na Padre Dino Gioia, moja wa waasisi wa Shirika la Wamissionari wa Damu Azizi ya Yesu nchini Tanzania. Mwaka 2011 akarejea nchini Italia na kuanza masomo na majiundo ya kitawa na kikasisi.

Tarehe 2 Mei 2015 akapokelewa Shirikani rasmi na tarehe 6 Januari 2017 akapewa Daraja ya Ushemasi wa mpito pamoja na Shemasi Dominic Mavula mikononi mwa Askofu Edward Mapunda wa Jimbo Katoliki Singida. Ibada hii inadhuhuriwa pia na Padre Dominic Mavula, C.PP.S aliyepadrishwa, hivi karibuni na Askofu msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, katika Parokia ya Mandera, Jimbo Katoliki la Morogoro. Matendo makuu ya Mungu kwa waja wake! Padre mteule Manzi  katika kauli mbiu yake anasema, “Mimi ninakwenda pale Bwana anaponituma, sina uhakika, lakini nina mwamini Yeye”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

 








All the contents on this site are copyrighted ©.