2017-07-21 16:52:00

Kanisa mwezi Novemba 2017 kuwasilisha mpango mkakati kwa wahamiaji


Askofu mkuu Ivan Jurkovič, Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Ofisi za Umoja wa Mataifa na Mashirika ya Kimataifa yaliyoko mjini Geneva kama sehemu ya mchango wa Vatican katika majadiliano ya Shirika la Kimataifa la Wahamiaji, (IOM) kuhusu wahamiaji: ushirikishwaji kama sehemu ya kukabiliana na changamoto ya wimbi kubwa la wahamiaji na wakimbizi duniani anasema, mwelekeo huu una umuhimu wake wa pekee katika utu na heshima ya wakimbizi na wahamiaji duniani.

Hawa ni watu ambao wanakataliwa, wanadhulumiwa na kunyanyaswa utu na heshima yao, ingawa sehemu nyingine za dunia ni watu wanaopokelewa kwa mikono miwili kabisa kutokana na machango wao katika ustawi na ukuaji wa uchumi! Wahamiaji wanakabiliwa na changamoto mbali mbali katika maisha yao. Ni watu wanaotaka kuboresha maisha yao: kiuchumi, kijamii na kisiasa pia. Wao ni sehemu ya sura mpya ya mchakato wa wimbi kubwa la utandawazi duniani; ni watu wenye: matumaini, ujasiri na ushupavu kiasi kwamba, wanaweza kutumika kama mashuhuda na vyombo ya amani kwa kutangaza na kushuhudia kwamba, binadamu wote wanaunda familia moja kubwa ya binadamu.

Tafiti na pembuzi yakinifu zinaonesha athari na mapungufu yanayojitokeza katika maisha ya wakimbizi na wahamiaji kutoka katika nchi zao za asili, wanapokuwa njiani na hatimaye, katika nchi zinazowapatia hifadhi. Athari na faida hizi zinajionesha katika maisha yao kama watu binafsi, familia na nchi mbali mbali wanakotoka, wanakopitia na hatimaye, mahali wanakopatiwa hifadhi na huduma. Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, kumekuwepo na kampeni chafu katika vyombo vya mawasiliano ya kijamii vinavyotishia ulinzi na usalama kwa raia na mali zao kutokana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji hali ambayo imewafanya wananchi kutowapokea na matokeo yake ni kuwazuia kuingia katika miji yao, kwa hofu ya kupoteza utambulisho na utamaduni wao!

Askofu mkuu Ivan Jurkovič, katika kukabiliana na changamoto hii anafafanua kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anakazia wajibu wa mshikamano kwa kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kuna haja ya kuwasaidia na kuwahudumia maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kujenga na kudumisha madaraja ya kuwakutanisha watu, ili hatimaye, kuweza kujenga ulimwengu bora zaidi unaofumbatwa katika haki na udugu.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, huu ni mchakato wa kutambua na kuthamini utajiri mkubwa unaofumbatwa katika tamaduni za watu hawa na kwamba, hakuna mpango wa kutawala wala kufifisha tamaduni za nchi zinazowapatia hifadhi. Huu si mpango wa kuonesha ubora wa tamaduni fulani hali ambayo ingeweza kusababisha utengano na ubaguzi, kiasi cha kutengeneza makazi duni ya watu. Katika mchakato huu, wakimbizi na wahamiaji wanapaswa kuonesha ushirikiano na mshikamano na watu pamoja na tamaduni zinazowapatia hifadhi ya maisha; kwa kuheshimu na kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi hisani. Hizi nchi ambazo zinatoa hifadhi, zinapaswa pia kuzingatia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia, kwa kujielekeza katika mchakato wa kuwashirikisha wahamiaji na wakimbizi katika maisha ya kawaida ya nchi hisani, kwa kuunganishwa na familia zao, nguzo msingi wa mafungamano ya kijamii.

Askofu mkuu Ivan Jurkovič, anakazia umuhimu wa kuendeleza mchakato huu wenye mwelekeo wa pande mbili zinazowajibikiana kikamilifu, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu kama kiini na kikolezo cha maendeleo endelevu ya binadamu. Viongozi Mahalia hawana budi kukuza na kudumisha sera na mipango itakayodumisha utamaduni wa kuwashirikisha watu; maboresho na utajiri wa pamoja na amani kama mambo msingi yanayopaswa kuvaliwa njuga na wahusika wote. Wahamiaji watambue kwamba, wanao wajibu wa kuzingati, kuheshimu na kutekeleza sheria, kanuni na desturi na tamaduni  za watu mahalia.

Mwishoni, Askofu mkuu Ivan Jurkovič anasema kwamba, mwezi Novemba, 2017 wakati wa mkutano mkuu wa Shirika la Kimataifa la Wahamiaji, Vatican pamoja na Mashirika yake ya Misaada Kimataifa kama vile, Caritas Internationalis, Order of Malta, Tume ya Kanisa Katoliki kwa ajili ya Wahamiaji Kimataifa, Mfuko wa Ukweli katika upendo “Caritas in Veritate” watakuwa na mkutano utakaowasilisha mbinu mkakati wa mazoea mema na mapendekezo muhimu katika mchakato wa maboresho ya kuwashirikisha wahamiaji katika maisha ya watu wanaowapatia hifadhi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.