2017-07-21 07:32:00

Huruma ya Mungu inafumbata historia nzima ya wokovu!


Desturi ya kibinadamu inatusukuma kumtenga au kumfukuza yule anayekuwa kinyume chako au mpinzani wako. Dominika ya leo tunawekewa wazo ambalo ni la kimapinduzi, yaani uvumilivu kwa wale ambao tunadhania kuwa ni waovu au wabaya au wapinzani. Hii ndiyo namna ya utendaji wa Mungu wetu, Yeye ni mvumilivu, haukumu kama binadamu na daima anatoa nafasi ya mabadiliko. Hii ndiyo huruma yake ambayo inaufunua upendo wake mkuu kwa wanadamu. Huruma yake ni ya milele na kwake Yeye si furaha anapomuona mwanadamu ameangukia dhambini. Leo tunafundishwa kuwa uvumilivu na moyo wa msamaha hutoa nafasi kwa mwenzako kujirudi na kutubu makosa yake, kurudisha tena uhusiano mwema kati yenu na hivyo kudumisha mshikamano wa kidugu.

Somo la Injili linaionesha hekima hiyo ya Mungu katika namna ya ajabu. Mwenyezi Mungu anawavumilia walio wema kuishi na kukua pamoja na walio waovu. Pengine tunaweza kuona ni jambo la hatari kwani hawa walio wema wanaweza kuathiriwa na kuvutika katika uovu. Lakini la hasha! Huo ni wasaa kwa hawa wema kutumika kama kielelezo cha maisha mazuri kwa waovu na kuwa sababu au msukumo wa wongofu wao. Wakati mwingine hukumu ya kuwatenga wanaoonekana waovu huweza kuathiri baadhi ya walio wema kutegemeana na unasaba au mahusiano yao. Lakini zaidi tunafunuliwa upendo wa Mungu kwa mwanadamu ambaye amemuumba katika ukamilifu. Mwanadamu anapokengeuka ni huzuni kwa Mwenyezi Mungu. Hali ya dhambi inamchafua haiba yake njema na hivyo Mwenyezi Mungu anajisikia kupasika kuwa na uvumilivu na kumtoa katika uovu wake.

Kwa namna ya nyingine tunaweza pia kutafakari uwepo wa ngano bora na magugu katika nafsi ya mtu mmoja. Tunaweza kumchukulia mtu mmoja kama shamba ambalo ndani mwake kunaonekana uwepo wa wema na ubaya. Mwenyezi Mungu anatuacha tuendelee kukua huku tumechangamana na udhaifu wetu ili kutoa fursa ya kujitambua na kujitakasa na hatimaye, kubakia safi kama Yeye mwenyewe anavyotaka tuwe. Yeye bado anayo matumaini makubwa ya wema kutawala juu ya uovu unaoweza kuambatana na sisi na zaidi tunaweza kuichukulia hali hiyo kama njia ya kuuonesha utukufu wa wema juu ya uovu. Anapotaka kuyaacha magugu kukua na ngano ni tahadhari ya kuepuka kuyaondoa hata yale yaliyo mema katika nafsi ya mtu. Mwisho wa yote tutapata fursa ya kugundua vema ni kipi kilicho chema na kukitunza na kipi kilicho uovu na kuking’oa na hivyo kubakiwa na mtu aliyetakasika.

Mwenyezi Mungu hatendi kama wanadamu. Yeye ni mwingi wa fadhili na amejaa rehema. Fursa anayompatia mwanadamu ni udhihirisho wa ukuu wa upendo na huruma yake. Kamwe mwanadamu asibweteke na kudhani kwamba Mungu hawezi kumwadhibu. Hekima ya Sulemani inatuambia: “Kwa kuwa iwapo wanadamu hawasadiki ya kuwa umekamilika katika uweza wako, Wewe wadhihirisha nguvu zako; waifadhaisha jeuri yao”. Ni onyo kwetu kutokuiacha mbachao kwa msala upitao. Tusibweteke na kudhani kwamba kwa kuwa Mungu ni mwenye huruma na amejaa upendo basi tuendelee tu kuponda raha na “kula bata” hadi kuku waone wivu. Huu ni wito wa kuhangaikia wokovu wetu; wito wa kugeuka na kuijongea huruma ya Mungu. Nafasi anayotupatia ni adhimu kwa ajili manufaa yetu kiroho.

Ingawa Mungu ni mwenye huruma lakini pia uhukumu kwa haki. Hekima ya Sulemani inamtambulisha Mungu katika haiba hiyo tukiambiwa: “Hakuna Mungu mwingine yeyote ila Wewe, unayewaangalia watu wote, hata umwonyeshe huyo ya kuwa hukuhukumu bila haki”. Mwisho wa maisha yetu hapa duniani “atawatuma malaika zake; nao watakusanya kutoka katika ufalme wake machukizo yote, na hao watendao maasi, na kuwatupa katika tanuru ya moto; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno. Ndipo wenye haki watakapong’aa kama jua katika ufalme wa Baba yao”. Uvumilivu wa Mwenyezi Mungu wa kutokuwaangamiza waovu ni fursa kwao kuijongea huruma ya Mungu kwani “Bwana yu mwema, amekuwa tayari kusamehe, na mwingi wa fadhili kwa watu wote wamwitao”.

Mtume Paulo anaweka mbele yetu msaada mahsusi wa kutufanya tuweze kujivika hali hiyo ya kimungu. Huyu ni Roho Mtakatifu kwani “hutusaidia katika udhaifu wetu, kwa maana hatujui kuomba jinsi itupasavyo”. Utendaji wowote wa kibinadamu ambao hausukumwi na Roho Mtakatifu ni wa visasi na vinyongo kwa wale wanaoonekana kukosea. Hapa tutatenda mithili ya watumwa wa mwenye shamba ambao baada ya kuona ngano njema zinamea pamoja na magugu wanamwambia Bwana wao: “Wataka twende tuyakusanye?” Ndivyo hekima ya kibinadamu inatusukuma katika kuchuchumilia ukamilifu tu na kutupilia mbali kilicho dhaifu. Kristo ni mfano kwetu wa huruma ya Mungu kama anavyotabiriwa na Nabii Isaya kwamba “mwanzi uliovunjika hakuuponda na wala utambi utoao moshi hakuuzima”.

Ni changamoto kwa jamii yetu ya leo ambayo haiko tayari kukumbatia kinachoonekana kuwa dhaifu na chenye mapungufu. Sayansi na teknolojia ambavyo ni matunda ya weledi wa kibinadamu katika kuufanya ulimwengu huu kuwa mzuri zaidi havitoi nafuu yoyote kwa vilivyo dhaifu zaidi ya kuvisukumizia pembezoni kabisa. Jamii imetawaliwa na utamaduni wa kuvifanya  kuwa takataka vile ambavyo havina faida. Ni vigumu kuviacha viendelee kukua na pengine kuboreka zaidi kadiri muda unavyosogea. Matukio ya utoaji wa mimba na kifo laini “eutanasia” yanathibitisha mwelekeo huo wa kibinadamu ambao haupo tayari kuvumilia na kuviacha vilivyo dhaifu kuendelea kukua pamoja na vyenye nguvu.

Changamoto ya pili ni ile hali ya kuishi kana kwamba Mungu hatofuatilia matendo yetu. Wanadamu wengi, hasa rika la vijana na hasa katika jamii iliyo juu kiuchumi hawana nafasi yoyote kwa Mungu. Mtindo wao wa maisha hauoneshi kugutushwa na huruma na uvumilivu wa Mungu. Wengi huamini katika uwepo wa Mungu lakini hupungukiwa na hekima ya kuutambua ukuu wake, nafasi yake na huruma yake kwao. Ni jambo la kumshukuru Mungu kwa uvumilivu wake lakini ni wakati wa kugutuka na kuchangamkia ufadhili wake huu. Anachopanda Mungu ndani ya viumbe vyote ni kilicho chema na kikamilifu, utii wetu kwake, ukubali wetu wa ukuu wake na kujifungamanisha naye wakati wote ni fursa kwetu ya kujisafisha na uovu unaotunyemelea na kutuchafua. Tusijidanganye kuwa wenyewe tunaweza. Roho wa Mungu ndiye anatuwezesha katika udhaifu wetu.

Mungu wetu ni mwenye huruma na ni mvumilivu. Tujitakase kwa nafasi mbalimbali anazotupatia ili kubaki kuwa ngano safi. Pia tuitumie nafasi yetu kama wale tuliojazwa na Roho Mtakatifu kuwa sababu ya nguvu, matumaini na mwanga mpya kwa wale wanaoonekana dhaifu. Tuwe wajumbe wa kuuneza upendo na huruma ya Mungu kwa kuukumbatia na kuuganga ubinadamu ulio dhaifu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.