2017-07-20 15:03:00

Zambia Miaka 125 ya huruma na upendo: Sasa ni muda wa ushuhuda!


Askofu mkuu Julio Murat, Balozi wa Vatican nchini Zambia, ndiye aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu kama kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 125 ya Imani Katoliki nchini humo kwa kuongozwa na kauli mbiu “Kanisa Katoliki nchini Zambia, miaka 125 ya upendo na huruma ya Mungu”. Ameitaka Familia ya Mungu nchini Zambia kuhakikisha kwamba, inajitahidi kuwa kweli ni shuhuda na chombo makini cha uwepo endelevu wa Kristo miongoni mwa watu wake. Hii ni changamoto kwa waamini kuhakikisha kwamba, wanamwilisha ndani mwao tunu msingi za maisha ya Kikristo, kwa kuiga na kuendeleza ujasiri wa kujitosa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Waamini wawe ni watangazaji wa Habari Njema ya Wokovu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko na kwa njia hii, watu wengine wataweza kuguswa na kuvutwa na uzuri pamoja na utakatifu wa imani ya Kanisa Katoliki. Kilele cha maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 125 ya Imani Katoliki nchini Zambia, kilikuwa ni hapo tarehe 15 Julai 2017. Askofu mkuu Murat amesoma salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Maadhimisho ya Jubilei ni kipindi cha kumshukuru Mungu kwa neema na baraka anazowakirimia waja wake.

Hiki ni kipindi cha kufanya toba na kuomba msamaha kwa mapungufu yote yaliyojitokeza katika kipindi hiki cha miaka 125 ya upendo na msamaha wa Mungu miongoni mwa wananchi wa Zambia. Huu ni wakati wa kuomba neema na baraka ili kusonga mbele kama mashuhuda wa tunu msingi za Kiinjili ndani na nje ya Zambia, kama kielelezo cha ukomavu wa imani.

Katika mahubiri yake, Askofu mkuu Telesphore George Mpundu, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Zambia amekazia kwa namna pekee umuhimu wa sadaka na majitoleo ya wamissionari wa kwanza, ambao wengi wao walifariki dunia wakiwa na umri mdogo sana kutokana na magonjwa pamoja na mazingira magumu. Dhamana ya kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo ndani na nje ya Zambia kwa sasa iko mikononi mwa waamini wenyewe wanaohamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba,  wanawashirikisha wengine furaha ya Injili ya Kristo ili iweze kuzaa matunda ya toba, wongofu wa ndani na utakatifu wa maisha!

Askofu mkuu Mpundu anakaza kusema, miaka 125 si haba, Kanisa nchini Zambia linapaswa kucharuka zaidi katika ari na maisha ya kimissionari. Waamini wahakikishe kwamba, wanajifunga kibwebwe kutangaza na kushuhudia imani yao kwa Kristo na Kanisa lake kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko. Waamini wajisadake kwa kuhakikisha kwamba, wanatumia vyema karama na mapaji waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya Kanisa zima.

Askofu mkuu Mpundu amehimiza waamini nchini Zambia kuhakikisha kwamba, wanajitegemea na kulitegemeza Kanisa kwa rasilimali watu, vitu na fedha, ili liweze kutekeleza dhamana yake ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, ili kupambana kufa na kupona na magonjwa, umaskini na ujinga. Haya ni maeneo ambayo Kanisa Katoliki nchini Zambia limeyavalia njuga katika kipindi cha miaka 125 iliyopita.

Kwa upande wake, Kardinali Berhaneyesus D. Souraphiel, Mwenyekiti wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika Mashariki na kati, AMECEA, ameungana na familia ya Mungu nchini Zambia kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa na shukrani kwa zawadi ya imani ambayo wamekirimiwa na Mwenyezi Mungu katika kipindi cha miaka 125. Huu ni muda muafaka wa kuweka sera na mikakati ya shughuli za kichungaji kwa miaka ijayo, kama sehemu ya utekelezaji wa mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

AMECEA inawashukuru na kuwapongeza watoto wa familia ya Mungu kutoka Zambia waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa AMECEA kwa kuanzia na Hayati Kardinali Medardo Mazombwe, Kardinali Adam Kozlowiecki aliyekuwa Mwenyekiti wa kwanza wa AMECEA kuanzia mwaka 1961 hadi mwaka 1964. Wengine waliokumbukwa ni pamoja na Askofu Dennis De Jong. Makatibu wakuu ni pamoja na  Padre Killian Flynn na Padre Peter Lwaminda. Wote hawa ni matunda ya upendo na huruma ya Mungu inayojikita katika mchakato wa uinjilishaji nchini Zambia. Maisha na utume wa Kanisa umewagusa watu wengi nchini Zambia.

AMECEA inaikumbusha familia ya Mungu nchini Zambia kwamba: furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya wanadamu wa nyakati hizi, hasa ya maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii yote ni furaha na matumaini; uchungu na fadhaa ya wafuasi wa Kristo pia, kama walivyosema Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.