2017-07-15 15:21:00

Jitaabisheni kulisoma, kulitafakari na kulimwilisha Neno la Mungu


Ndugu yangu,  Ninakukaribisha katika tafakari ya Neno la Mungu Dominika hii ya 15 ya Mwaka A wa Kanisa. Mama Kanisa siku ya leo anatusisitizia juu ya nafasi na umuhimu wa Neno la Mungu katika maisha ya kila mwanadamu na hasa katika maisha ya mfuasi wa Kristo. Tunaongozwa na masomo matatu toka katika Maandiko matakatifu. Somo la kwanza latoka katika kitabu cha Nabii Isaya Sura ya 55 aya ya 10 hadi ya 11, somo la pili linatoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi Sura ya 8 aya ya 18 hadi ya 23 na somo la tatu linatoka katika Injili ya Mtakatifu Mathayo Sura ya 13 aya ya 1 hadi ya 23. Kukuletea tafakari hii ni mimi Padre Walter Milandu wa Shirika la Damu Takatifu Ya Yesu.

Ndugu yangu mpendwa tafakari ya Neno la Mungu Dominika mbili zilizopitz zilitusaidia kuelewa nini maana ya kuwa mfuasi wa kweli wa Kristo. Mkristo wa kweli ni yule ampaye Mungu nafasi ya kwanza kuliko mtu au kitu chochote na ambaye yuko tayari kuuchukua msalaba wake akimfuata Yesu nyuma yake. Pia mfuasi wa kweli wa Yesu ni yule anayejifunza toka kwa Kristo akiziishi tunu na fadhila za maisha ya Yesu mwenyewe.  Zaidi sana Mkristo wa kweli ni yule ambaye hujiweka daima chini ya maongozi ya Roho Mtakatifu kama jinsi Yesu mwenyewe alivyoongozwa naye katika kutimiza mapenzi ya Baba yake. Leo hii Mama Kanisa anatupatia tena kipimo au sharti jingine la kuwa mfuasi wa Yesu Kristo. Sharti au kipimo hicho ni kuwa tayari kulipokea Neno la Mungu na kuruhusu Neno hilo lifanye kazi na kuongoza maisha ya Mkristo. Tunapolipokea Neno la Mungu katika maisha yetu Neno hilo linafanya kazi kuu mbili.

Kwanza kabisa Neno la Mungu linatupatia nafasi ya kumjua Mungu na kutambua mapenzi yake katika maisha yetu. Mungu katika historia, ameongea na mwanadamu kwa njia mbalimbali lakini kwa namna ya pekee na kwa namna iliyo bora zaidi, Mungu anaongea na mwanadamu kwa njia ya Neno lake. Athari za kutosikiliza Neno la Mungu ni kutomjua Mungu, kutomjali na kumuasi Mungu kama jinsi ilivyotokea kwa wana wa Israeli. Nabii Isaya mwanzoni mwa sura tuliyoisoma leo, anaonyesha masikitiko ya Mungu kutokana na tabia ya wana wa Israeli kutomsikiliza na hatimaye kumuasi akisema, “Sikieni enyi mbingu, tega sikio Ee nchi maana Bwana amenena, Nimewalisha watoto na kuwalea, nao wameniasi. Ng’ombe amjua bwana wake, na punda ajua kibanda cha bwana wake, Bali Israeli hajui, watu wangu hawafikiri.” Hayo ndiyo yanayotutokea hata sisi katika maisha ya kila siku tunaposhindwa kusikiliza Neno la Mungu. Na Neno hili la Mungu ndiyo Kristo mwenyewe aliyekuwepo tangu kabla ya kuumbwa ulimwengu, akafanyika mwili naye akafanya makao yake kati yetu. (Yoh 1:14. )

Mtakatifu Yeronimo alisema kuwa kutojua Maandiko Matakatifu ni kutomjua Kristo, ni kutomjua Mungu. Haitoshi kusikiliza Neno mara mojamoja tu tunapokwenda Kanisani bali tujitahidi kusoma na kulitafakari Neno hilo kila siku katika ngazi ya mtu binafsi, katika familiya na katika jumuiya zetu. Hati ya Mtaguso wa pili wa Vatican kuhusu Ufunuo wa Mungu (Dei Verbum), ililenga katika kuliweka Neno la Mungu mikononi mwa waamini ili waweze kulisoma na kulitafakari ili Neno hilo liweze kuongoza maisha yao na Yesu atawale maisha yao, kama jinsi maneno ya Zaburi ya 118 aya ya 105 yanavyosema, “Neno lako ni taa ya miguu yangu.” Baba Mtakatifu Francisko tangu mwanzoni mwa uongozi wake, anatilia daima mkazo nafasi ya Neno la Mungu katika maisha ya kila Mkristo. Leo hii mimi na wewe tujiulize, tunalipa nafasi gani Neno la Mungu katika maisha yetu ili tuweze kumjua Mungu zaidi na zaidi  

Kazi ya pili ya Neno la Mungu tunapoliacha lifanye kazi ndani yetu ni kutufanya tuzae matunda. Tukiruhusu Neno la Mungu lipenye ndani ya maisha yetu, hakika Neno hili litaleta mabadiliko makubwa katika maisha yetu. Katika kusisitiza ukweli huu, Mungu kwa kinywa cha nabii Isaya anatuambia, “Maana kama vile mvua ishukavyo, na theluji, kutoka mbinguni, wala hairudi huko, bali huinywesha ardhi, na kuizalisha na kuichipuza ikampa mtu apandaye mbegu na mtu chakula”. Mfano huu ni rahisi kuuelewa kwani sote tunafahamu ni jinsi gani mvua huleta mabadiliko katika uso wa nchi. Mvua inaponyesha, maji huleta uhai kwa kuchipusha na kuistawisha mimea na kuipa rangi ya kijani inayovutia hata kwa macho. Ustawi huu wa mimea huleta furaha kwa wanyama na hasa wanadamu kwa kujipatia chakula cha kutosha. Neno la Mungu ni kama mvua katika mioyo na maisha yetu.

Sisi sote tuliobatizwa tumepewa jukumu la kuwa wamisionari yaani kuwa mashaidi wa imani yetu na kulitangaza Neno la Mungu duniani kote na kwa watu wote ili watu wote wapate kuokoka. Mtume Paulo katika waraka wake kwa Warumi sura ya 10 aya ya 13 hadi ya 14, anatusisitizia wajibu wetu wa kulitangaza Neno la Mungu akisema, “…kila atakayeliita Jina la Bwana ataokoka. Basi watamwitaje yeye wasiyemwamini? Tena watamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena watamsikiaje pasipo mhubiri?” Ndugu yangu kabla ya kulishuhudia na kulihubiri Neno la Mungu Neno hili lazima lilishe, listawishe na kuimarisha imani na maisha yetu kama wakristo. Kila tunaposoma na kutafakari Neno la Mungu tunakutana na Kristo na ndiye anayetupa furaha ya ya kweli na inayodumu.

Baba Mtakatifu Francisko katika maneno yake yanayofungua Waraka wake wa Kitume “Evangelium gaudium” yaani ”Furaha ya Injili”, anasema, “Furaha ya Injili huijaza mioyo na maisha ya wote wanaokutana na Yesu. Wale wanaoikubali zawadi yake ya ukombozi wanawekwa huru  kuondokana na na dhambi, uchungu, utupu wa ndani na upweke.” Ni Neno la Mungu ambalo linatupa nguvu ya kumshuhudia hata pale ambapo inapotupasa kuteseka kama jinsi Mtume Paolo anavyotuasa katika somo la pili. Neno la Mungu linatupa matumaini kwamba nyuma ya Kashfa ya Msalaba kuna ushindi na utukufu.

Hata hivyo,  Yesu katika Injili tuliyoisikia leo anatukumbusha kuwa Neno la Mungu ni kama mbegu inayopandwa. Mbegu hii hufa, hutoa matunda dhaifu au hutoa matunda mengi na mazuri kadiri ya aina ya mahali inapoangukia au inapopandwa. Kadiri ya maelezo ya Yesu mwenyewe, mambo au mazingira mbalimbali yanaweza mbegu ya Neno la Mungu kukua na kuzaa matunda yanayotarajiwa kutokana na jinsi gani tunalipokea neno hili. Leo wewe na mimi tunapaswa kujiuliza, Je, mioyo yetu ni mahali gani ambapo mbegu ya Neno la Mungu huangukia? Yesu anatarajia kuwa kila aliye mfuasi wake awe udongo mzuri ili Neno lake liweze kuzaa matunda yanayojikita katika toba na wongofu wa ndani; utakatifu na unyofu wa moyo!

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.