2017-07-13 13:45:00

Baba Mtakatifu Francisko "awafagilia sana" Makatekista kwa utume wao!


Makatekista ni kati ya mihimili mikuu ya Uinjilishaji tangu mwanzo kabisa wa Kanisa, kwani hawa wamebebeshwa jukumu la kuwaandaa wakatekumeni kupokea: imani ya Kanisa inayofumbatwa katika Fumbo la Utatu Mtakatifu; kwa kuwaandaa kuzifahamu na hatimaye kuadhimisha vyema Sakramenti za Kanisa; kwa kumwilisha Amri za Mungu kama dira na mwongozo wa maisha ya Kikristo yanayofumbatwa katika sala. Ili kweli Makatekista waweze kutekeleza dhamana na wajibu wao katika maisha na utume wa Kanisa hawana budi kufundwa: kiakili, kitaalimungu, kimaadili, kiutu na kichungaji.

Ni watu wanaohimizwa na Mama Kanisa kutangaza na kushuhudia imani yao kwa njia ya maisha yenye mvuto na mashiko, kwa kutambua kwamba, hii ni kazi endelevu inayohitaji ustahimilivu, kwani ni chanzo cha uvuvio! Makatekista wanahimizwa kutekeleza wajibu huu kwa majitoleo, ujasiri, bidii, uaminifu mkubwa na utakatifu wa maisha chachu muhimu sana katika ujenzi wa Fumbo la Mwili wa Kristo, yaani Kanisa! Kuanzia tarehe 11 Julai hadi tarehe 14 Julai 2017, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Kanisa Katoliki Argentina, UCA, kinaendesha kongamano la kimataifa kuhusu Katekesi, huko Buenos Aires.

Kongamano limeandaliwa na Taasisi ya Katekesi nchini Argentina, ISCA na linaongozwa na kauli mbiu “Heri wale wanaoamini”. Askofu mkuu Luis Francisco Ladaria, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa na Monsinyo Josè Arenas, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya kuhamasisha Uinjilishaji mpya ni kati ya wawezeshaji wakuu wanaoshiriki katika kongamano hili. Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe aliomwandikia Askofu mkuu Ramon Afredo Dus, Mwenyekiti wa Tume ya Katekesi na Utume wa Biblia, Baraza la Maaskofu Katoliki Argentina anapenda kukazia mambo makuu mawili: Ubunifu na safari ya pamoja kama mambo msingi yanayompatia Katekista utambulisho wake katika maisha na utume wa Kanisa.

Mtakatifu Francisko alikazia kwa namna ya pekee kabisa, katekesi inayomwilishwa katika ushuhuda wa imani tendaji, pale wanaowatembelea wagonjwa; wanapowasaidia watoto wadogo; wanapowanywesha na kuwapatia chakula maskini; hapa watambue kwamba, wanatekeleza sehemu kubwa sana ya kazi ya Uinjilishaji wenye mvuto na mashiko. Ikumbukwe kwamba, Ukatekista si kazi bali ni wito wa huduma katika Kanisa unaomsukuma kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu, kwa kuwafundisha Mafumbo ya Kanisa na kwamba, utangazaji wa awali ni msingi wa mambo yote. Utangazaji na ushuhuda huu hauna budi kuwasindikiza watu katika safari ya maisha yao ya kiroho. Ni watu wanaoweza kusaidia kuimarisha ibada na upendo mambo msingi yanayoweza kusaidia kuunda mazingira ya zawadi ya imani, ili kwamba, maneno na matendo yao yanaonesha ushuhuda wa kuwa ni wafuasi wa Kristo Yesu.

Baba Mtakatifu Francisko anawataka Makatekista kutembea pamoja na Kristo Yesu, kwa kumwachia nafasi ili aweze kuwagusa kwa jicho lake lenye upendo unaopenyeza katika sakafu ya maisha ya waamini wake, ili hatimaye, waweze kuwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya huruma na upendo wa Mungu kwa jirani zao, wanapomhubiri Kristo Yesu. Yesu daima alikuwa ni mtu wa sala iliyomwilishwa katika matendo ya huruma na upendo kwa kuwatibu na kuwaganga wagonjwa; kwa kuwalisha na kuwanywesha wale wote waliokuwa na njaa na kiu ya Mungu. Aliwaponya na kuwaokoa watu kutoka katika lindi la dhambi na aibu, kiini na chimbuko la katekesi ya Mafumbo ya Kanisa inayojikita katika Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.

Baba Mtakatifu Francisko anakaza kusema, Katekesi ni utangazaji na ushuhuda wa Neno na daima kiini chake ni Neno, lakini inahitaji mazingira yenye mvuto, utumiaji wa ishara zilizo wazi, ili kumwezesha mwamini kukua na kukomaa katika maisha; kwa kusikiliza kwa makini na kuitikia. Katekista anapaswa kuwa ni mtu mwenye kipaji cha ubunifu, anayeweza kutumia njia mbali mbali za mawasiliano ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima.

Kristo ana uwezo wa kuzima kiu ya furaha ya maisha hapa duniani. Huu ni utafiti unaopania kumfahamu Kristo Yesu kama utimilifu wa uzuri na wema wote duniani anayewawezesha kumtangaza na kumshuhudia, jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Makatekista wanasoma alama za nyakati, ili kuwashirikisha watu huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao na wala hakuna sababu msingi ya kuogopa kwani Kristo mwenyewe anawatangulia katika maisha na utume wao na kwamba, yuko kati ya watu wa nyakati hizi, anawasubiri kwa hamu kubwa. Mwishoni, Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza Makatekista wanaofanya hija na familia ya Mungu katika maeneo yao! Anawataka wawe wajumbe jasiri, walinzi wa wema na uzuri unaong’ara na kuangaza katika maisha; daima wakiwa ni wafuasi wamissionari. Yesu mwema awabariki na Bikira Maria, mwalimu wa imani awalinde kwa tunza yake ya kimama!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.