Mitandao ya kijamii:

RSS:

Radio Vatican

Sauti ya Papa na Kanisa katika majadiliano na ulimwengu

Lugha:

Kanisa Barani Afrika \ Elimu

Umuhimu wa elimu katika kupambana na: ujinga, umaskini na maradhi!

Don Lorenzo Milani alikazia sana umuhimu wa elimu kuwa ni chombo makini cha kupambana na baa la njaa,umaskini na njaa duniani. - AP

12/07/2017 09:31

Padre Lorenzo Milani, Mkuu wa nyumba ya kitawa ya Barbiana katika maisha yake alijiwekea utamaduni wa kukimbilia mara kwa mara katika kiti cha huruma ya Mungu ili kuomba toba na msamaha wa dhambi zake kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya huruma ya Mungu na Mama mpendelevu kwa watoto wanaokimbilia huruma na tunza yake ya kimama! Hivi ndivyo anavyosema Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video kwa washiriki wa onesho la vitabu lililoandaliwa na Jimbo kuu la Milano kuanzia tarehe 19 - 23 Aprili 2017. Huyu ni Padre ambaye alisadaka maisha yake kwa ajili ya kuandika vitabu, akaitupa mkono dunia akiwa na umri wa miaka 44 na sasa imetimia miaka 50 ya ushuhuda wa nguvu!

Baba Mtakatifu anasema ni kiongozi ambaye alibahatika kuwa ni mwalimu na mlezi wa vijana; tunu msingi alizorithishwa kutoka katika familia yake ambayo haikuwa na imani na wakati mwingine, ilikuwa ni kikwazo kikubwa kwa Mapadre. Ni tabia ambayo aliibeba katika maisha yake, kiasi kwamba, hata wakati mwingine alikuwa ni mgumu na wengi walishindwa kumwelewa hata baada ya toba na wongofu wake wa ndani kunako mwaka 1943, wakati anatekeleza dhamana na wajibu wake wa kichungaji kama Padre. Haya ni mambo yanayoweza kujionesha katika maandiko yake mintarafu mfumo wa elimu, upendeleo kwa maskini pamoja na kusimama kidete kulinda na kudumisha uhuru wa dhamiri.

Baba Mtakatifu anawaalika waamini kulipenda na kulithamini Kanisa hata kama limejeruhiwa vibaya. Lakini elimu inayotolewa na Kanisa inawasaidia watu kuwa na upeo mpana kuhusu uhalisia wa maisha kwa kufungua akili na nyoyo zao, kiasi kwamba, wanaweza kuwa ni jasiri kukabiliana na ukweli wa maisha. Shuleni watu wanajifunza kwanza kabisa mambo msingi na baadaye wanajielekeza kwa mambo msingi kwani shule ni mahali ambapo mtu anajifunza kujifunza na baada ya kujifunza kujifunza anaendelea kujifunza zaidi kwani elimu haina mwisho.

Huu ni ushuhuda wa wema na upendo kwa wanafunzi wake aliotamani kuwapatia utu na chachu ya upendo kwa Kristo na Injili yake; kwa Kanisa na Jamii, huku akitamani na kuota kwamba, shule iwe ni hospitali wazi katika uwanja wa vita ili kuwaokoa na kuwasaidia maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Lengo ni kuwapatia wanafunzi: ujuzi, kufahamu na kuzungumza kwa weledi, tayari kusimama kidete kulinda na kutetea haki zao msingi. Haya ni mambo ambayo Padre Lorenzo alipenda kuyatumia hata wakati wa mahubiri yake na maadhimisho ya Sakramenti mbali mbali za Kanisa.

Utajiri, urithi na amana ya Don Milani imebisha hodi, Jimbo Katoliki la Njombe, Tanzania, hususan katika kijiji cha Nyakipambo, ambako kunako mwaka 2008 Padre Liberatus Mwenda alianzisha Chuo cha Ufundi Stadi, ili kuwajengea uwezo vijana waliokuwa wanatoka katika familia maskini, ili kuweza kupambana na changamoto za maisha na hatimaye, kujitegemea kwani mtaji wa maskini ni nguvu zake mwenyewe! Huduma hii ya elimu kwa sasa imevaliwa njuga na Padre Method Mwihava anayetumia fursa hii ya elimu kuwasaidia hata watoto yatima, ili kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Kumbu kumbu ya miaka 50 tangu alipofariki dunia Don Milani, matunda yake yanazidi kuenea kwa kwa wafadhili na wahisani mbali mbali kuendelea kuwekeza katika sekta ya elimu, chombo madhubuti katika ukombozi wa mwanadamu: kiroho na kimwili.

Vijana wa Nyakipambo wanayo matumaini makubwa kutokana na msaada wa elimu ya ufundi wanaoipata Chuoni hapo. Wako makini kushiriki katika mchakato wa maboresho ya maisha ya familia zao; wanashiriki pia katika ustawi na maendeleo ya jamii yao! Don Milani alikazia umuhimu wa elimu kuwa ni chombo makini cha kupambana na baa la njaa, umaskini, ujinga na ubaguzi unaofanywa kutokana na baadhi ya watu kuwa na maamuzi mbele! Elimu makini ni chachu ya umoja, upendo na mshikamano kati ya watu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.

12/07/2017 09:31