2017-07-12 14:08:00

Mwongozo wa Wafanyakazi katika Sekta ya Afya kuzinduliwa Septemba


Ilikuwa ni tarehe 12 Julai 2016, Askofu mkuu Zygmunt Zimowski, aliyekuwa Rais wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya wafanyakazi katika sekta ya afya alipofariki dunia. Monsinyo Jean-Marie Mupendawatu, aliyekuwa Katibu mkuu wa Baraza hili ambalo kwa sasa ni sehemu ya Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumbu kumbu hii, alipokuwa nchini Poland kwa safari ya kikazi. Akiwa huko ameshiriki pia katika hija ya maisha ya kiroho kwa kuungana na familia ya Mungu nchini Poland kwenda kwenye Madhabahu ya Bikira Maria wa Jasna Gora, yaliyoko Jimbo kuu la Czestochowa, ili kusali na kuwaaminisha watu wa Mungu chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria sanjari na wokovu wa walimwengu.

Katika mahojiano maalum na Radio Vatican, Monsinyo Mupendawatu anasema, ameungana na wagonjwa pamoja na wazee kusali Rozari Takatifu, muhtasari wa historia nzima ya huruma ya Mungu kwa binadamu; amesikiliza shuhuda za mateso na mahangaiko ya wagonjwa; akaonja: imani na matumaini yanayobubujika kutoka katika sakafu ya maisha yao, hata kama wanateseka kutokana na magonjwa mbali mbali!

Ameadhimisha kumbu kumbu ya mwaka mmoja tangu Askofu mkuu Zygmunt Zimowski alipofariki dunia! Ni kiongozi aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kulinda, kukuza na kudumisha, utu, heshima, ustawi na mafao ya wagonjwa sehemu mbali mbali za dunia. Hata katika mateso na mahangaiko yake, aliweza kuifuata Njia ya Msalaba, akayatolea mateso na mahangaiko yake kwa ajili ya malipizi ya dhambi zake binafsi na kwa ajili ya huduma ya Kanisa kwa wagonjwa. Hayati Askofu mkuu Zygmunt Zimowski ameacha urithi mkubwa kama Askofu: umuhimu wa kuwahudumia watu bila kujibakiza; ushauri wake kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro ambao pia umepelekea kuundwa kwa Baraza la huduma ya maendeleo endelevu ya binadamu pamoja jitihada za kutaka kuboresha huduma ya afya duniani, maskini wakipewa kipaumbele cha kwanza.

Mwongozo wa Wafanyakazi Katika Sekta ya Afya utakaozinduliwa rasmi, Mwezi Septemba 2017. Kimsingi unakazia umuhimu wa wafanyakazi katika sekta ya afya kuhakikisha kwamba wanatumia: akili, ujuzi, maarifa na weledi wao kwa ajili ya kuwahudumia wagonjwa; wawaoneshe huruma na upendo na kamwe wasiwageuze kuwa ni kichokoo cha majaribio ya kisayansi! Wafanyakazi hawa wawaonjeshe: huruma na upendo; wawapatie kipaumbele wanachohitaji kwa uwepo na huduma yao makini; wawaelewe na kushirikishana; wawaonjeshe wagonjwa uvumilivu na utu wema sanjari na kukuza majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa ajili ya ustawi na mafao ya mgonjwa mwenyewe! Kila mgonjwa anapaswa kuangaliwa kwa jicho la huruma na mapendo!

Monsinyo Mupendawatu anasema, sekta ya afya inakabiliwa na changamoto kubwa ya kimaadili, ukosefu wa rasilimali fedha na watu; vifaa tiba na dawa; hali ambayo inapelekea watu wengi kupoteza maisha hasa katika nchi maskini zaidi duniani. Bado kuna idadi kubwa ya watu walioathirika kwa ugonjwa wa Ukimwi, ambao bado hawajapata fursa ya kupatiwa dawa za kurefusha maisha; hawa pia ni changamoto kubwa inayohitaji mshikamano wa upendo, unaoongozwa na kanuni auni! Makampuni makubwa yanayotengeneza dawa, yanapaswa kuonesha moyo wa huruma kwa maskini badala ya kujikita katika kupata faida kubwa. Jumuiya ya Kimataifa ijenge mtandao wa umoja, mshikamano na udugu kwa ajili ya kuwasaidia watu wanaoteseka kutokana na magonjwa mbali mbali, hasa yale yasiyokuwa na tiba wala chanjo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.