2017-07-12 15:05:00

Msilichakachue Neno la Mungu likashindwa kuzaa matunda yanayokusudiwa


Kila jambo na kila kitu hapa ulimwenguni kina makusudi yake. Vyote vilivyomo ni matokeo ya kazi adhimu ya uumbaji wa Mwenyezi Mungu na kwa hakika tunaweza kutamka kama Mzaburi tukisema: “Nchi imejaa fadhili za Bwana” (Zab 33:5). Kwa neno lake Bwana Mungu vitu vyote vimefanyika. Neno lake lina nguvu na neno lake ni kweli. Anapotamka basi huwa hivyo alivyotamka. Kwa namna nyingine ahadi ya Mungu inatimilizika. Yeye aliye chanzo cha kila kilicho chema hubaki daima katika kunuia mema na hivyo neno lake kwetu sisi viumbe vyake hutamkwa mahsusi kabisa kwa ajili ya ustawi wetu kwa sababu anayajua mahitaji yetu.

Nabii Isaya analifananisha neno la Mungu na mvua au theluji ishukayo kutoka Mbinguni na kuinyweshea ardhi na kuirutubisha. Mwenyezi Mungu anasema: “Neno langu halitarudi bure, bali litatimiza mapenzi yangu, nalo litafanikiwa katika mambo yale niliyolituma”. Ahadi yake Mwenyezi Mungu si ya kuwahadaa au kuwapumbaza watu bali hubaki mwaminifu katika neno lake. Neno la Mungu haliwezi kurudi nyuma au kubadilika. Waisraeli ambao wapo utumwani Babeli wanapatiwa uhakika wa kurudi makwao kwa sababu Mungu ameahidi hivyo. Hapa ni muhimu kukumbuka kwamba tabia ya udongo na mazingira ya udongo unaonyeshewa nayo huchangia utoaji wa matunda. Pamoja na uwezekano wa kuwa na hali hizi tofauti wazo kubwa bado linabaki kwamba nia ya Mwenyezi Mungu ni neno lake kuzaa matunda kwa ajili ya ufanisi na ukamilifu wa viumbe vyake vyote.

Katika Injili ya Dominika hii Kristo anatupatia jambo muhimu la kutafakari. Pamoja na kwamba neno la Mungu ni hakika litazaa lakini yapo mazingira ambayo huyawekea vikwazo. Mfano wa mpanzi unatuelekeza katika neno la Mungu linalopandwa ndani ya nafsi ya kila mmoja wetu na lenye tumaini la kuzaa matunda mema. Namna hii ya kuyaona matunda ya neno la Mungu kwa mwitikio tofauti inafafanua juu ya hulka mahsusi ya kibinadamu na upendo wa Mungu kwetu. Pamoja na kwamba nia ya Mwenyezi Mungu ni kutoa matunda kadiri anavyonuia, Mungu wetu ni mwaminifu sana na anaheshimu hadhi ya kila kiumbe chake. Amemuumba mwanadamu huru kuweza kuchagua cha kufanya, kuweza kumtii Yeye au kutomtii. Yeye haleti Neno lake kama shuruti bali anategemea ushirikiano wa mwanadamu anayelipokea.

Mbegu za mpanzi zinaangukia katika barabara na ndege wakaja mara moja kuzinyakua. Neno la Mungu linatuambia kwamba: “Kila mtu alisikiapo neno la ufalme asielewe nalo, huja yule mwovu, akalinyakua lililopandwa moyoni mwake”. Hali ya barabara ina tabia ya ugumu na daima wengi hupita juu yake. Mioyo iliyo mithili ya barabara ni ile ambayo haina nafasi hata kidogo kwa ajili ya Mungu, ni aina ya wanadamu ambao hawafikiri chochote kilicho chema na kinachotoka kwa Mungu. Mioyo yao imejazwa na uovu na hukosa msingi wa kulipokea Neno la Mungu.

Mbegu zinazoangukia penye miamba tunaambiwa kuwa ni “huyo alishikaye lile neno, akalipokea mara kwa furaha; lakini hana mizizi ndani yake, bali hudumu kwa muda; ikitukia dhiki au udhia kwa ajili ya lile neno, mara huchukizwa”. Huu ni ushabiki wa kidini katika mambo ambayo yanafurahisha nafsi yangu, katika mambo ambayo yanatimiza matakwa ya hamu ya moyo wangu. Maeneo haya huwapata wengi wenye mielekeo ya dini kama vile ushirikina. Mungu anabaki kuwa na nafasi moyoni mwangu pale ninapopata muujiza. Hivyo nafasi ya Mungu ni kutoa tu, upande wangu sihitaji kumtambua sana na wala sina muda wa kuitafakari hulka yake na ukuu wake.

Mbegu zinazoangukia katika miiba tunaambiwa kuwa ni “yeye alishikaye neno; na shughuli za dunia, na udanganyifu wa mali hulisonga lile neno likawa halizai”. Hapa wanawakilishwa wale ambao bado wanatamani kutambulika kama Wakristo lakini bado wanavutika na mali zao, madaraka yao na umaarufu wao wa kidunia. Mambo yao yanapoangaziwa na neno la Mungu hupingwa mara moja. Kamwe neno la Mungu lisiupunguze ujiko wao bali liendelee kuutetea. Mazingira kama haya hutumika hata kuwahadaa wahubiri na watumishi wa Mungu na hivyo kuwanyima fursa ya kurekebisha mienendo mibovu ya hawa wenye mali.

Aina hizo zote tatu za udongo hapo juu ni matunda ya kazi ya shetani. Tangu mwanzo dhambi ilipoingia ulimwenguni shetani amempofusha mwanadamu asiweze tena kuiona nafasi ya Mungu na wingi wa fadhili zake kwake. Shetani amemkuza mwanadamu kifikra na kujifikiri kuwa yupo sawa na Mungu. Hivyo neno la Mungu halipati tena nafasi. Mwenyezi Mungu anaponuia mema kwa ajili ya ulimwengu huu binadamu hugeuza kwa ajili ya faida yake binafsi. Dhambi ya mwanadamu haimdhuru tu mwanadamu bali viumbe wote kwa ujumla. Mtume Paulo anatuambia kwamba: “Kwa maana twajua ya kuwa viumbe vyote pia vinaugua pamoja, navyo vina utungu pamoja hata sasa”.

Machafuko, vita, uhasama, uahribifu wa mazingira na dhuluma nyingi dhidi ya viumbe leo hii ni matokeo ya binadamu anayeligeuzia kisogo neno la Mungu na kutaka kutenda atakavyo yeye. Mwanadamu anapingana na ukweli kwamba Mungu ameviweka viumbe vyote katika mlingano sawia na vyote kutegemezana na hivyo sababu ya kujiona kuwa yupo sana na Mungu anafanya anavyotaka yeye kwa faida yake ya kibinadamu na kwa ubinafsi wake. Hivyo si ajabu kusikia ndoa za kishoga zinahalalishwa, uporaji wa maliasili za wanyonge unafumbiwa macho, uchafuzi wa mazingira hasa kwa hasara ya wasio na uwezo kujikinga, mfano wa wanadamu fukara ua viumbe wengine katika mazingira yao unafumbiwa macho hata na wale wenye kujiita mababa wa Dunia.

Mbegu zinazoangukia katika udongo mzuri tunaambiwa kuwa “ndiye alisikiaye neno, na kuelewa nalo; yeye ndiye azaaye matunda, huyu mia, na huyu sitini; na huyu thelathini”. Huyu ndiye yule ambaye analipatia nafasi neno la Mungu kutoa matunda yake na kuendelea kuufanya ulimwengu huu kuwa bora zaidi. Hawa ndiyo wana wa Mungu ambao Mtume Paulo anawataja kama tumaini kwa viumbe wote kwani matunda yake yatawaweka wote kuwa huru. Sisi wabatizwa tumepewa hadhi mpya na kufanyika udongo huu mzuri wa kuzaa matunda mema. Hivyo ni changamoto kwetu kuyathibitisha matunda haya kwa kazi njema mbele ya viumbe vyote, kazi njema ambazo zitauimarisha uwiano kati ya viumbe vyote. Tukumbuke daima kwamba ulimwengu wote na vyote vilivyomo ni kazi ya Bwana. Yeye daima hunuia mema juu ya kazi ya mikono yake. Maelekezo ya Mungu kwetu si kutunyang’anya nafasi yetu juu ya kazi ya uumbaji bali ni maongozi ya kuleta uwiano mzuri. Tumshitukie shetani anayetuadaa na anayetaka kuharibu kazi hii njema ya uumbaji kwa kuzuia neno la Mungu lisimee ndani mwetu.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.