2017-07-10 09:55:00

Ujumbe wa Maadhimisho ya Jumapili ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2017


Mabaharia wanao mchango mkubwa sana katika ustawi wa jamii, maendeleo na mafao ya wengi duniani, lakini kwa bahati mbaya ni watu wanaotekeleza dhamana na wajibu wao katika mazingira magumu na hatarishi sana. Maadhinisho ya Jumapili ya Utume wa Bahari, ambayo imeadhimishwa na Mama Kanisa Jumapili, tarehe 9 Julai 2017 imekuwa ni siku ya kumshukuru Mungu na kutambua mchango unaotolewa na Mabaharia wapatao milioni 1.5, wengi wao wakiwa ni wale wanaotoka katika Nchi changa zaidi duniani. Juhudi, bidii na maarifa yao, yanawawezesha watu wengi kufurahia maisha, kwa kusafiri salama pamoja na kusafirisha mizigo ambayo kimsingi ni sawa na asilimia 90% ya mizigo yote inayosafirishwa duniani!

Mabaharia wanao mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi duniani, lakini changamoto, shida na magumu wanayokabiliana nayo ni mengi sana, kiasi cha kutishia usalama wa maisha, utu na heshima yao kama binadamu. Hii ni sehemu ya ujumbe wa maadhimisho ya Siku ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2017, ulioandikwa na Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu anayefafanua kwa kina na mapana baaadhi ya changamoto wanazokabiliana nazo Mabaharia sehemu mbali mbali za dunia!

Licha ya maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii ambayo imewawezesha Mabaharia kuweza kuwasiliana mara kwa mara na familia zao, lakini bado familia zinakabiliwa na changamoto kubwa katika malezi na makuzi ya watoto. Kwa bahati mbaya akina mama wanajikuta wakiwa pweke kwa muda mrefu hali inayowalazimu kujifunga kibwebwe katika kuhudumia familia peke yao. Kumbe, hapa wafanyakazi katika sekta ya utume wa bahari wanapaswa kuwa na jicho la upendeleo kwa familia za mabaharia, kwa kuwajengea umoja ili waweze kusaidiana na kufarijiana katika safari yao ya maisha.

Maboresho ya njia za mawasiliano yasaidie kujenga umoja na mshikamano na familia pamoja na wale wanaofanya nao kazi kwani kuna hatari kwa mabaharia kujikuta wakitoa kipaumbele cha kwanza kwa familia zao na kuwasahau wale wanaofanya nao kazi kila siku! Hii ni hatari kubwa inayojengwa na mitandao ya kijamii, kwa kuunganika na watu wengi katika ombwe, lakini wanatengwa wale ambao wako karibu sana  katika uhalisia wa maisha. Jambo la msingi ni kujenga na kudumisha utu na mawasiliano ya kibinadamu miongoni mwa mabaharia ili kuvunjilia mbali upweke hasi unaoweza kuwatumbukiza watu hata wakatamani kutema zawadi ya uhai; hali ya kutengwa na kukosa maana na thamani ya maisha na hatimaye, msononoko hatari sana kwa maisha ya binadamu kwani tafiri nyingi zinaonesha kwamba, haya ndiyo mambo msingi yanayopelekea mabaharia wengi kujinyonga!

Vitendo na mashambulizi ya kigaidi yamepekea sheria za usalama bandarini kupitiwa upya na kuimarishwa, kiasi kwamba, mabaharia katika baadhi ya mataifa hawaruhusiwi kutoka kwenye vyombo vyao vya usafiri, lengo likiwa ni kuimarisha ulinzi na usalama kwa watu na mali zao, lakini kwa bahati mbaya mazingira kama haya yanawatenga watu, hata wakati mwingine kutokana na utaifa, rangi, dini na mahali wanakotoka, hali ambayo inakwenda kinyume kabisa cha haki msingi za binadamu! Mabaharia wanapaswa kupewa huduma msingi za afya, ustawi na maendeleo yao kadiri ya sheria za kimataifa.

Kardinali Peter Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu anakaza kusema, tangu mwaka 2013, Jumuiya ya Kimataifa imeanza kutekeleza mambo msingi ya kiutu na haki ya nguvu kazi kwa mabaharia, lakini bado wengi wao wanadanganywa kima cha mishahara yao, wananyonywa na hatimaye, kudhalilishwa utu na heshima yao kama binadamu mahali pa kazi; wanashutumiwa na wakati mwingine kusukiwa ajali baharini na huko wanaachwa wakiteseka katika magereza ya nchi za kigeni. Mabaharia wana haki ya kupata msaada wa hali na mali, lakini pia viongozi wa bandari wanapaswa kuwa makini ili kuhakikisha kwamba mabaharia hawanyanyaswi na pale wanapotendewa kinyume cha sheria, basi haki itendeke kwa kuwafikisha wahusika katika vyombo vya sheria.

Katika miaka ya hivi karibuni vitendo vya kiharamia vimepungua kwa kiasi kikubwa baharini kutokana na Jumuiya ya Kimataifa kuimarisha ulinzi na usalama baharini, lakini bado mabaharia wanatishiwa na mashambulizi ya silaha na utekwaji nyara katika baadhi ya maeneo ya kijiografia. Hii ni changamoto kwa mabaharia pamoja vyombo vya usalama baharini kuhakikisha kwamba, wanasimama kidete kulinda na kuimarisha ulinzi na usalama wa mabaharia, mizigo na vyombo vya usafirishaji wanavyotumia.

Kardinali Peter Turkson, anapenda kuhitimisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2017 kwa kujielekeza katika sekta ya uvuvi na wavuvi wenyewe, watakaokuwa wanapewa kipaumbele cha pekee katika Kongamano la XXIV Kimataifa, litakalofanyika mwezi Oktoba, 2017 huko Kaohsiung, nchini Taiwan. Wavuvi ni watu wanaotumia pia muda wao mrefu wakiwa majini  na kwamba, ni kundi la wafanyakazi linalotekeleza dhamana na wajibu wake katika mazingira magumu na hatarishi sana. Hili ni eneo ambalo limekumbwa kwa kiasi kikubwa na biashara haramu ya binadamu, kazi za suluba na shuruti; vitendo vya uvunjaji wa sheria pamoja na uvuvi haramu ambao ni tishio kubwa kwa usalama wa maisha ya wavuvi wenyewe pamoja na walaji wake.

Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu ya Binadamu linasema, litatumia kongamano hili kuragibisha masuala nyeti na muhimu katika maisha ya wavuvi duniani; litapenda kuimarisha mtandao wa wavuvi ili kukuza na kudumisha ushirikiano miongoni mwa Utume wa Bahari kwa Mataifa mbali mbali duniani. Utakuwa ni muda muafaka wa kushirikishana na kubadilishana rasilimali, uzoefu na mang’amuzi katika sekta ya uvuvi duniani, ili kuboresha tija na ufanisi katika sekta hii muhimu sana katika ukuaji wa uchumi na maendeleo ya wengi. Kongamano hili linatarajiwa kuhudhuriwa na wataalamu na mabingwa wa masuala ya uvuvi, wahudumu na watu wanaojitolea katika Utume wa Bahari, kwani hata wavuvi nao ni sehemu ya Utume wa Bahari. Kardinali Peter Turkson anahitimisha ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Utume wa Bahari kwa Mwaka 2017 kwa maombezi ya Bikira Maria, Nyota ya Bahari, ili aweze kusimamia na kuwalinda mabaharia, wavuvi pamoja na familia zao, hadi pale watakapofika kwenya bandari salama ya maisha ya uzima wa milele.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.