2017-07-10 09:29:00

Familia ya Mungu Barani Afrika: Dumisheni majadiliano ya kidini!


Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kuendelea kujikita zaidi na zaidi katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni katika ukweli, uwazi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Huu ni ujumbe kutoka kwa Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini aliowaandikia wajumbe wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika ya Kati, CERAC, walioanza mkutano wao tarehe 8 Julai 2017 huko Yaoundè, Cameroon na unatarajiwa kuhitimishwa, Jumatano tarehe 12 Julai 2017. Askofu Miguel Angel Ayuso Guixot, Katibu mkuu wa Baraza anashiriki katika mkutano huu.

Maaskofu pamoja na mambo mengine wanapembua kwa kina na mapana, changamoto, matatizo na fursa zilizopo katika mchakato wa majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Katika ujumbe wake, Kardinali Tauran anawaalika Maaskofu kujikita zaidi katika majadiliano ya kidini, kwa kuyapatia uzito wa pekee katika maisha na utume wa Kanisa mahalia. Bara la Afrika linaanza kuzalisha waamini wenye misimamo mikali ya kidini na kiimani, hali ambayo imepelekea kuibuka mashambulizi ya kigaidi sehemu mbali mbali za Bara la Afrika; ghasia na machafuko yenye mielekeo ya kidini.

Kikundi cha kigaidi cha Boko Haramu kinaendelea kupandikiza mbegu ya kifo, chuki na uhasama kati ya watu huko Nigeria, Chad na Cameroon. Haya ni maeneo yenye idadi kubwa ya waamini wa dini ya Kiislam, lakini hata wao wanashambuliwa na kikundi hiki cha kigaidi. Machafuko ya kisiasa na ukosefu wa utawala bora ni kati ya mambo yanayoendelea kuchangia mateso na mahangaiko ya watu, kiasi kwamba, madhara yake yanajionesha hata katika mchakato wa maendeleo ya kiuchumi miongoni mwa wananchi wengi, ambao kwa sasa wanaendelea kutumbukia katika dimbwi la umaskini wa hali ya juu kabisa. Amani na utulivu ni mambo msingi katika kukuza na kudumisha maendeleo endelevu ya binadamu!

Kardinali Tauran anakaza kusema, kuna haja ya kuboresha zaidi mahusiano kati ya Kanisa Katoliki na Makanisa pamoja na Jumuiya za Kikristo huko Gabon na Jamhuri ya Watu wa Congo. Mwelekeo huu hauna budi kujikita pia katika maboresho ya majadiliano na waamini wa dini za jadi Barani Afrika, kwani hata hawa bado idadi yao ni kubwa, kumbe, wanapaswa kuhusishwa katika majadiliano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Afrika. Katika shida na mahangaiko ya  wananchi huko Afrika ya Kati, Wakristo kwa namna ya pekee kabisa, wanahamasishwa na Mama Kanisa kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matumaini, hasa kwa wale waliokata tamaa kwa kutambua kwamba, licha ya tofauti zao msingi, lakini wote ni ndugu wamoja wanaounda familia kubwa ya binadamu Barani Afrika.

Maaskofu Barani Afrika hawana budi kujizatiti kikamilifu katika mchakato wa maendeleo endelevu ya binadamu: kiroho na kimwili; kwa kusimama kidete: kulinda, kukuza na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu. Maaskofu wawe mstari wa mbele kupigania haki, amani na mshikamano wa kitaifa, kwani majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni yanapania pamoja na mambo mengine haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kila mwanadamu anayo haki ya kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Ili kufanikisha azma hii nyeti, kuna haja ya kujenga na kudumisha umoja, udugu na mshikamano wa dhati unaosimikwa katika ukweli, kwa watu kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu; kwa kujenga upendo na ukarimu kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii; kwa kuwa na mgawanyo na matumizi sawa ya rasilimali na utajiri wa dunia, zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Familia ya Mungu Barani Afrika haina budi kushikamana kwa dhati katika kulinda na kuendelea mazingira nyumba ya wote, kwa kutoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na heshima ya binadamu, aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko anafundisha kwamba, ili kuweza kumwilisha tunu hizi msingi kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, kuna haja kwanza kabisa kuondokana na utamaduni na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine, kwa kujikita katika mchakato wa ujenzi wa madaraja ya watu kukutana, kuheshimiana na kusaidiana kama ndugu. Watu waondokane na dhana ya uadui na badala yake, udugu na urafiki vipewe msukumo wa pekee zaidi. Waamini wa Kanisa Katoliki hawana budi kujifunga kibwebwe ili kushirikiana na watu wote wenye mapenzi mema, kwa kuwajibika na kuaminiana, ili hatimaye, kuvunjilia mbali maamuzi mbele ambayo daima yamekuwa ni chanzo kikuu cha mipasuko ya kidini na kijamii sehemu mbali mbali za dunia.

Watu wajifunze kuheshimu na kuthamini tofauti msingi na kwamba, huu ni utajiri unaopaswa kukumbatiwa ili kujenga umoja katika utofauti kwa ajili ya ustawi wa wengine! Tofauti kati ya watu kisiwe ni chanzo cha vita, ghasia na mipasuko ya kijamii. Waamini wakiwa kweli ni mashuhuda na vyombo vya umoja, amani, upendo na mshikamano, hata Serikali zao zitahamasika kukuza na kudumisha: ustawi na maendeleo ya wengi; kwa kuunda mazingira bora zaidi yatakayosaidia maboresho ya fursa za kazi, ukuaji wa uchumi na ustawi wa jamii; mambo msingi katika kudumisha amani na ustawi wa watu. Kila mwananchi ajitahidi kuwa kweli ni chombo cha amani mahali alipo. Mwishoni, majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni anasema Kardinali Jean Louis Tauran, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya kidini ni changamoto inayopaswa kuvaliwa njuga na familia ya Mungu Barani Afrika kama sehemu ya ujenzi wa jamii inayosimikwa katika misingi ya haki, amani, udugu na umoja, ili kudumisha demokrasia ya kweli na utawala bora. Kila mtu anawajibika kutengeneza mazingira bora yatakayowawezesha watu kujisikia kuwa ndugu wamoja, licha ya tofauti zao, kwa kuonesha upendo na ukarimu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.