2017-07-08 17:03:00

Jifunzeni kwa makini kutoka kwa Yesu, ili muwe mashuhuda amini!


Ndugu mpendwa nakukaribisha katika tafakari ya Neno la Mungu Dominika hii ya 14  ya Mwaka A. Tuko katika kipindi cha kawaida cha mwaka wa liturjia baada ya kuadhimisha mafumbo makuu ya ukombozi wetu. Katika kipindi hiki Mama Kanisa anatusisitizia kuishi mambo muhimu  ambayo Bwana wetu Yesu Kristo aliyotufundisha kwa maneno na kwa mfano wa maisha yake. Neno la Mungu katika Dominika hii linatutafakarisha juu ya nini maana ya kuwa wafuasi wa kweli wa Kristo. Katika tafakari hii tunaongozwa na masomo matatu. Somo la kwanza linatoka katika kitabu cha Nabii Zekaria Sura ya 9, aya ya 9 mpaka ya 10. Somo la pili linatoka katika Waraka wa Mtume Paulo kwa Warumi Sura ya 8, aya 9 na ya 11 mpaka ya 13. Somo la tatu linatoka katika Injili ya Mtakatifu Mathayo Sura ya 11, aya ya 25 hadi ya 30.

Ndugu msikilizaji ni vema siku ya leo tukajiuliza, “Je, nini maana ya kuwa Mkristo au mfuasi wa Yesu Kristo?” Je, inatosha kubatizwa au kuitwa jina la kikristo? Je, inatosha kwenda kanisani kuhudhuria ibada kila Dominika au siku nyingine? Neno la Mungu linatupa jibu mara moja kwamba hayo yote ni mazuri na ya kufaa lakini hayatoshi kumfanya mtu awe mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo. Katika kutoa majibu halisi kwa maswali tuliyojiuliza Bwana wetu Yesu Kristo Dominika iliyopita alituambia kwamba mtu yeyote ambaye hayuko tayari kumpatia yeye nafasi ya kwanza katika maisha yake kuliko watu wote au kuliko kitu chochote, hakika mtu huyo hafai kuwa mfuasi wake. Zaidi sana alilisisitiza kwamba yeyote asiye tayari kuchukua msalaba wake na kumfuata nyuma yake hawezi kuwa mfuasi wake.

Kadhalika katika Dominika hii masomo yetu ya leo yanatupatia namna nyingine mbili muhimu za kuwa Wakristo wa kweli. Namna ya kwanza tunaiona katika somo la Injili pale ambapo Yesu mwenyewe anapotualika sote akisema, “…njoni mjifunze kwangu….” Ndugu yangu unayenisikiliza, hatuwezi kuwa wafuasi wa Kristo kama hatuko tayari kujifunza kutoka kwake. Kazi ya kwanza ya mitume na wafuasi wengine waliomfuata Yesu ilikuwa ni kujifunza toka kwake na ndiyo maana hawa waliitwa wanafunzi wake. Wewe na mimi tunaalikwa tumtazame yeye kwa makini ili tujifunze kutoka kwake si kwa nadharia tu bali tuweze kuiga tunu na fadhila zake katika maisha yetu ya kila siku. 

Tunapomtazama Bwana wetu Yesu Kristo, tunajifunza fadhila nyingi ambazo kama tukiziishi, basi tutafanikiwa kufanana naye. Neno la Mungu Dominika ya leo limeweka mbele yetu  fadhila au sifa mbalimbali zilizojenga maisha ya Bwana wetu Yesu Kristo. Yeye mwenyewe katika Injili tuliyoisikia anasema, “…jifunzeni kwangu maana mimi ni mpole na mnyenyekevu wa Moyo.” Yesu anatualika tuige upole na unyenyekevu wake. Fadhila hizi ni muhimu sana katika mahusiano yetu na Mungu pamoja na mahusiano kati yetu sisi kwa sisi. Katika mafundisho yake Yesu alisisitiza sana fadhila ya upole kwa wafuasi wake. Katika ile hotuba maarufu ya mlimani, Yesu anasema “Heri wenye upole; maana hao watairithi nchi. (Mathayo: 5,5). Yesu anaposema watairithi nchi anamaanisha wataurithi Ufalme wa Mbinguni. Mtu mpole ni mtu mtulivu, mstaarabu asiyependa kulipa kisasi wala kutumia nguvu dhidi ya wengine.

Mtu mnyenyekevu ni mtu asiye na majivuno, asiye na dharau kwa wengine na asiyejiona kuwa ni bora zaidi kuliko wengine. Mtu mnyenyekevu humtegemea na kumtumaini Mungu nyakati zote akitambua nguvu na udhaifu wake. Yesu hatufundishi tu kuwa wapole na wanyenyekevu bali yeye mwenyewe alitupatia mfano katika maisha yake ndiyo maana yeye ambaye ni Mungu alikubali kunyenyekea na kutii hadi mauti, naam mauti ya Msalaba (Filipi 2:8). Fadhila na tunu hizi, zilitosha kumdhihirisha Yesu kwamba ndiye yule Masiha ambaye ujio wake ulitabiriwa na manabii. Katika somo la kwanza, Nabii Zekaria anawafunulia Waisraeli sifa na fadhila za Masiha au Mfalme wanayemsubiria akisema, “Furahi sana Ee binti Sayuni, piga kelele Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako, ni mwenye haki, ni mnyenyekevu, amepanda punda…naye atawahubiria mataifa yote habari za amani.” Somo hili husomwa siku ya Dominika ya Matawi kumdhihirisha Yesu ambaye pamoja na kuwa ni Mfalme, anaingia Yerusalem kwa upole na unyenyekevu akiwa kapanda punda. 

Nao wimbo wa katikati leo hii unaotoka katika Zaburi ya 144 unatupatia baadhi ya sifa au tabia nyingine zilizopamba maisha ya Bwana wetu Yesu Kristu. “Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma, si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema, ni mwema kwa watu wote.” Ndugu yangu hizo ni baadhi ya sifa au fadhili zilizopamba maisha ya Bwana wetu Yesu Kristu amabazo kwazo tunaalikwa kufanana naye.

Namna nyingine ya kuwa wafuasi wa kweli ya Yesu Kristo ni kumpa nafasi Roho Mtakatifu katika maisha yetu na kujiweka daima chini ya maongozi yake. Yesu alikubali kuongozwa na Roho Mtakatifu tangu mwanzo hadi mwisho wa maisha yake hapa duniani. Mwanzoni mwa kazi yake hadharani ya kuutangaza Ufalme wa Mungu, Yesu aliongozwa na Roho Mt. jangwani alipofunga kwa siku arobaini akamwimarisha katika mapambano dhidi ya Shetani. Kwa maongozi ya Roho huyo Yesu alifaulu kutimiza mapenzi ya Baba yake kila siku kama jinsi yeye mwenyewe akishuhudia kwa kusema, chakula changu ni kutimiza mapenzi ya Baba. (Yohane 4:34). Roho Mtakatifu alimwimarisha daima katika kutimiza mapenzi ya Baba hata pale ilipombidi aingie kwenye mateso makali na amwage Damu yake Msalabani.

Ndugu yangu, Roho Mtakatifu ni zawadi kubwa ya Kristu Mfufuka kwetu sisi. Roho huyo tulimpokea kwa mara ya kwanza tulipobatizwa na tukaimarishwa naye kwa Sakramenti ya Kipaimara. Hatuwezi kuwa wafuasi wa kweli wa Kristu kama hatutamruhusu Roho Mtakatifu kuishi na kufanya kazi ndani yetu. Ndiyo maana Mtume Paulo katika somo la pili anatuonya juu ya Ukristo wetu akisema, “…mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristu, huyo si wake.” Kila tunapopokea Ekaristi Takatifu kwa kustahili basi tunamruhusu Roho wa Bwana kufanya kazi ndani yetu. Roho huyu anatuwezesha kutembea katika mwanga wa Kristu mfufuka na kutuwezesha kuchagua matendo ya mwanga yaletayo uzima na kuyakataa matendo ya giza yanayotuelekeza kwenye kifo. Mtakatifu Paulo katika somo la pili anatuonya akisema, “kama mkiishi kwa kufuata mambo ya mwili, mwataka kufa, bali kama mkiyafisha matendo ya mwili kwa Roho, mtaishi.”

Endapo tutamruhusu Roho Mtakatifu afanye kazi ndani yetu basi tutachagua na kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu. Lakini kama hatutamruhusu Roho wa Bwana kufanya kazi ndani yetu basi itakuwa vigumu kutekeleza mapenzi ya Mungu na tutachagua na kutenda kadiri ya tamaa na ubinafsi wetu. Matokeo yake hatutakuwa na mahusiano mazuri na Mungu pamoja na wenzetu. Tutatambua kwamba Roho Mtakatifu anaishi ndani yetu endapo matunda yake yatajidhihirisha katika maisha yetu, katika familiya na jamii inayotuzunguka. Matunda hayo ni: upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Wagal. 5: 22.

Ndugu yangu mpendwa, wewe na mimi siku ya leo tunapaswa kujiuliza maswali muhimu yafuatayo: “Je, ni kwa namna gani nafanana na Bwana wangu Yesu Kristo? Na ninafanya juhudi gani kufanana naye zaidi na zaidi?” Pia kila mmoja wetu ajiulize, “Je, nampa nafasi gani Roho Mtakatifu katika maisha yangu? Je, ninayashuhudia matunda yake katik maisha yangu na kwa wale wanaonizunguka?”

Nakutakia Dominika njema na Mungu akubariki sana. 

Na Padre Walter Milandu, C.PP.S.








All the contents on this site are copyrighted ©.