2017-07-06 15:39:00

Kanisa Mahalia Jimbo la Musoma, Tanzania


Askofu Michael Msonganzila katika Barua yake ya kichungaji Upendo kwa Utume anapotafakari maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji Tanzania Bara, Miaka 100 ya Upadre Tanzania na Miaka 60 ya Jimbo la Musoma, leo anaangalia kwa namna ya pekee  kuhusu ukuaji wa Kanisa Mahalia nchini Tanzania: Mapadre wa kwanza wazalendo Tanzania na hali ya Kanisa Mahalia Jimbo la Musoma.

Nilieleza wakati wa maadhimisho ya Sinodi yetu ya Jimbo kuwa kanisa mahalia huwa na sifa kuu tatu; kujiongoza, kujieneza na kujitegemea. Kanisa mahalia hujiongoza kwa kuwa na uongozi wake wa Askofu, Mapadre, Watawa na Walei katika nafasi zao halisi. Hujieneza kwa kushika hatamu za uinjilishaji wa kina na kwa kuwa na roho ya utume. Hatimaye, Kanisa mahalia hujitegemea kwa kutambua mahitaji yake na kuwa tayari, kwa kushirikishana majaliwa ya hali na mali, kuendesha shughuli za kichungaji na kijamii. Sifa hizi tatu hubaki kama kipimo cha ukuaji wa kanisa mahalia.

Kanisa la Tanzania lilipata mapadre wa kwanza wazalendo mwaka 1917 ikiwa ni baada ya miaka arobaini na tisa tangu ujio wa wamisionari Bagamoyo. Upatikanaji wa mapadre hawa ulikuwa ni hatua muhimu sana katika ukuaji na ukomavu wa kanisa Tanzania. Tunapoyaangalia mazingira ya jumuiya changa ya wakristo wa wakati huo na kufikiri juu ya changamoto zilizowakabili katika kuuitikia wito wa upadre, hatukosi kuwasifu na kuvutiwa na upendo mkubwa waliokuwa nao kwa utume katika kuupokea wito wa Upadre.

Upadre ni zawadi ya upendo na ni tunda la upendo. Ni zawadi ya upendo wa Mungu mwenyewe kwa wanadamu na tena zawadi anayowajalia kwa uhuru wake na bila mastahili yao. Upendo huu mkubwa wa kimungu huhitaji jibu la upendo toka kwa mwanadamu katika kuitika kama Nabii Isaya “Mimi hapa nitume mimi…” (Isa. 6:8). Ndiyo maana tunapomshukuru Mungu kwa zawadi hii kubwa ya upendo, kwa dhati kabisa tunayataja kwa shukrani na heshima kubwa majina ya mapadre hao wa kwanza: Pd. Angelo Mwirabure, Pd. Celestine Kipanda, Pd. Wilbard Mupapi na Pd. Oscar Kyakaraba. Tunawashukuru wao, familia zao wale wote waliohusika katika malezi yao hadi kufikia daraja Takatifu.

Kanisa Mahalia Jimbo la Musoma

Upadrisho wa watangulizi hao wanne ulitia chachu mpya katika ukuaji wa Kanisa la Tanzania. Kutokana na uwepo wa wamisionari wengi kutoka Ulaya ilikuwa rahisi kuuhusisha upadre na watu kutoka Ulaya pekee. Kwa kupatikana mapadre hawa wazalendo ni dhahiri dhana mpya ilianza kujengeka kuwa “inawezekana mtanzania kuwa padre”. Huu ulikuwa mwanzo wa vijana wengi kuuitikia wito wa upadre na kujitoa kwa huduma ya kanisa.

Katika Jimbo letu la Musoma, Padre wa kwanza mzalendo alikuwa ni Msgr. Laurence James Magesa, mzaliwa wa Parokia ya Nyegina. Huyu alipadrishwa tarehe 24 Januari 1954. Wakati huu Musoma ilikuwa ni Prifektura ya Kitume kabla haijafanywa Jimbo kamili mwaka 1957. Alifariki tarehe 2 Novemba 2007 baada ya kuhudumu katika upadre kwa miaka 53. Hadi tunapoadhimisha miaka hii 60 ya Jimbo la Musoma, wamekwisha padrishwa mapadre sitini na watano (65) katika Jimbo letu. Tunawakumbuka na kuwaombea mapadre waliokwishaitwa kwa Baba ili wajaliwe kuona kwa uhalisia yale mafumbo matakatifu waliyoadhimisha kwa ishara wakiwa hapa duniani. Tuwakumbuke pia na kuwaombea kwa namna ya pekee watangulizi wangu marehemu maaskofu John Rudin (1957 - 1979), Anthony Mayala (1979 - 1987) na Justin Samba (1989 -2006).

Idadi ya mapadre katika Jimbo letu bado ni ndogo. Hii inafanya mwaliko wa Kristo “Mwombeni Bwana wa mavuno apeleke watendakazi katika mavuno yake” (Mt. 9:37) kuwa wa maana sana kwetu. Kama familia moja nawaalika tuendelee kusali kwa ajili ya kuwaombea mapadre na pia kwa ajili ya kuombea miito hasa katika mwaka huu wa Jubilei. Hatuwezi kuacha kuelekeza fikra zetu za shukrani kwa mapadre wamisionari ambao wanaendelea kuitikia mahitaji ya Jimbo letu na kuja kufanya kazi pamoja nasi. Tunawaalika waendelee pamoja nasi kuijenga familia ya Mungu jimboni Musoma, familia iliyo tayari wakati wote kuishuhudia Imani kwa Matendo yao mema na yenye kumrudishia Mungu sifa na utukufu.

Na Askofu Michael Msonganzila,

Jimbo Katoliki la Musoma, Tanzania.

 


 







All the contents on this site are copyrighted ©.