2017-07-05 16:43:00

Mapadre: Wito na maisha yenu yamehifadhiwa kwenye chombo cha udongo!


Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni akiwa Jimbo kuu la Genova, Kaskazini mwa Italia alipata nafasi ya kukukutana na: wakleri, watawa na majandokasisi kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Lorenzo. Baba Mtakatifu alifafanua kwa kina na mapana juu ya vigezo vinavyopaswa kutumiwa na wakleri katika kutekeleza dhamana, majukumu na utume wao katika ulimwengu mamboleo, unaoonekana kuwapeleka mchaka mchaka! Aliwataka kukazaia: Umoja na udugu wa maisha na utume wa Kipadre unaorutubishwa kwa njia mikutano, hija za maisha ya kiroho, mafungo pamoja na ujirani mwema, lakini Baba Mtakatifu alikazia zaidi huduma makini na mshikamano na maskini! Amewataka watawa kuhakikisha kwamba, wanaishi kwa uaminifu karama na utume wao, kama sehemu ya utekelezaji wa sera na mikakati ya kichungaji majimboni mwao!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 ya tangu Mapadre wa kwanza walipopewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kutokana na uzito wa tukio hili, Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania linaadhimisha Mwaka wa Padre ambao utafikia kilele chake huko Jimbo kuu la Dodoma, tarehe 15 Agosti 2017. Hiki kitakuwa ni kipindi cha semina na makongamano kwa watu wa Mungu nchini Tanzania mintarafu maisha, wito na utume wa kipadre. Kwa kutambua changamoto zilizoko mbele ya Mapadre wengi katika maisha na utume wao, tungependa kukushirikisha tena vigezo msingi katika maisha, utume na wito wa Kipadre kama vilivyopembuliwa na Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni, hasa ukizingatia kwamba, Mwezi Julai, Majimbo na Mashirika mengi nchini Tanzania, ni kipindi cha Mashemasi wa Mpito kupewa Daraja Takatifu ya Upadre.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Yesu alikuwa karibu pamoja na watu; akatambua matatizo, changamoto na fursa zao na kuzipatia majibu muafaka. Daima alijitahidi kuanza na kuhitimisha matukio makubwa katika maisha yake kwa njia ya sala. Wakleri na watawa wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa utulivu bila haraka kwani haraka haraka haina baraka. Wawe ni watu wa kusoma alama za nyakati na kamwe wasiwe ni watumwa wa muda. Wajitahidi kuadhimisha mafumbo ya Kanisa kwa ibada na uchaji na kamwe si kama wafanyakazi wa mshahara. Maisha na wito wa kipadre na kitawa daima ni mapambano endelevu yanayopaswa kusimikwa katika sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu; katika huduma makini na shirikishi!

Yesu katika maisha yake alikutana na wagonjwa, maskini, waliopagawa na wadhambi. Mapadre wajitahidi kukutana na Kristo Yesu katika Fumbo la Ekaristi Takatifu na Mwenyezi Mungu katika sala na waamini katika huduma. Mapadre na watawa wajenge sanaa ya kusikiliza kwa makini shida na mahangaiko ya watu! Wajitahidi kukutana na Kristo mfufuka miongoni mwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wajenge moyo wa saburi na uvumilivu, daima wakijikita katika kipaji cha ubunifu, sadaka na utayari, vinginevyo, watachoka na kuwachosha waamini wao. Wawe na jicho la huruma na mapendo kwa wale wanaotaka huduma yao; hao ndio pia wanaowasindikiza katika maisha na utume wao kwa sala, sadaka na majitoleo yao ya kila siku!

Baba Mtakatifu anawaonya mapadre na watawa kuhusu tabia ya kujitafuta wenyewe; kutafuta ”ujiko” na umaarufu usiokuwa na tija wala mashiko; hizi ni dalili za utupu katika maisha yao, hatari sana. Mapadre na watawa wawe ni watu wa sala, tafakari makini ya Neno la Mungu; hata katika mchoko waoneshe uvumilivu, ari na moyo mkuu, kwani hizi ni cheche za utakatifu wa maisha. Wawe ni madaraja ya kukutana na watu; kielelezo cha Ibada ya kuabudu Ekaristi Takatifu; wahudumu wa familia ya Mungu wanaoweza kusikiliza kwa makini; wanaowaheshimu na kuwathamini jirani zao, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa kwa furaha na uaminifu mkubwa!

Taarifa iliyotolewa na Padre Aidan Mubezi, Katibu Jimbo kuu la Dar es Salaam inaonesha kwamba,  tarehe 7 Julai 2017, majira ya Saa 3:00 kwenye Viwanja vya Kituo cha Msimbazi, Jimbo kuu la Dar Es Salaam, Askofu Msaidizi Eusebius Alfred Nzigilwa atatoa Daraja Takatifu ya Upadre kwa Mashemasi 6 wa Jimbo na Mashemasi 3 kutoka katika Mashirika ya Kitawa. Mapadre watarajiwa ni kama ifuatavyo:

Shemasi Alfonce Ntakwezile.

Shemasi Danipaso Bitegeko.

Shemasi Francis Malele.

Shemasi Frank Mtavangu.

Shemasi Simoni Shija.

Mashemasi kutoka katika Mashirika ya Kitawa ni kama ifuatavyo:

Shemasi Conrad Mutayoba, OFM.

Shemasi Patrick Aidan Ngamesha, Shirika la Yesu (Jesuists).

Shemasi Christopher Amoni Mapunda, Shirika la Yesu (Jesuits).

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican inawatakia heri na baraka tele katika maandalizi ya kupokea Daraja Takatifu ya Upadre. Daima wakumbuke tu kwamba, hii ni zawadi kubwa sana ambayo imehifadhiwa kwenye chombo cha udongo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.