2017-07-03 14:25:00

Papa Francisko: Jumuiya ya Kimataifa ishikamane ili kutokomeza njaa!


Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe uliosomwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumatatu tarehe 3 Julai 2017 wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 40 wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO ameonesha masikitiko yake kwamba, hakuweza kuhudhuria katika mkutano huu kama yalivyo mapokeo tangu kuanzishwa kwa FAO, lakini anawakilishwa kikamilifu na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican. Ni matumaini yake kwamba, wajumbe wa mkutano huu wataweza kushirikisha majibu muafaka kuhusu sekta ya kilimo na chakula, ili kuzima kiu ya matumaini ya mamilioni ya watu duniani.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, Vatican inaendelea kufuatilia kwa ukaribu sana shughuli za Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato mzima unaopania kufutilia mbali baa la njaa na utapiamlo wa kutisha duniani. Haitoshi kuonesha utashi mwema wa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula kila siku, lakini inapaswa kufahamika kwamba, chakula ni sehemu ya haki msingi za binadamu, kumbe, watu hawana budi kupata chakula. Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo Mwaka 2030 unaendelea kusua sua kutokana na ukosefu wa utamaduni wa mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa unaopaswa kumwilishwa katika hali halisi ya maisha ya watu, lakini kwa bahati mbaya, Jumuiya ya Kimataifa inajikuta ikiwa imefungwa zaidi na takwimu au hamu ya kutaka kupata tija kabla ya kumwilisha dhana ya ushirikiano na mshikamano kwa ajili ya ustawi na mafao ya wengi! Kuna haja kwa kila nchi kuhakikisha kwamba, inaongeza kiwango chake za uzalishaji wa chakula, kwa kujikita katika maboresho ya sekta ya kilimo na hali ya maisha ya wakulima vijijini.

Kuna haja anasema Baba Mtakatifu Francisko, kuwa na sera na mbinu mkakati makini utakaosaidia maboresho ya shughuli za uzalishaji na ugavi wa mazao ya kilimo, kwa kutambua kwamba, binadamu anapaswa kukombolewa kutoka katika lindi la umaskini na baa la njaa, changamoto inayohitaji umoja na mshikamano wa dhati kutoka kwa familia nzima ya binadamu, ili kuwasaidia wale wanaoogelea katika majanga haya maisha! Mahali ambapo baa la njaa bado linaendelea kuwatesa watu, kiwango cha maendeleo kitakuwa duni na kwamba, athari za mabadiliko ya tabianchi yanaweza kusababisha hatari kubwa ya kukosa kuwa na uhakika wa usalama wa chakula. Katika mazingira kama haya, kuna haja kwa FAO na Mashirika ya Kimataifa kuingilia kati ili kuonesha mshikamano ili kupata ufumbuzi wa changamoto hii. Ikumbukwe kwamba, rasilimali na utajiri wote wa dunia ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kuwahudumia watu wote, kwa kujikita katika mshikamano kama kipimo cha ushirikiano wa kimataifa.

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, baa la njaa linaendelea kutishia maisha ya watu wengi duniani na kwamba, hakuna sababu ya kukata tamaa kwani baa la njaa na utapiamlo ni dalili za ukosefu wa maendeleo na kielelezo cha hali ya juu kabisa cha ubinafsi. Vita, vitendo vya kigaidi, changamoto ya wakimbizi na wahamiaji ni mambo ambayo yanaendelea kukwamisha ushirikiano wa kimataifa, dhana inayotekelezwa kwa sera zilizotungwa kwa makusudi mazima. Lakini, ifahamike kwamba, kuna watu wanaolazimika kuzikimbia nchi zao kutokana na sababu mbali mbali, kwa matumaini ya kupata usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Misaada ya maendeleo kwa nchi maskini duniani inazidi kupungua siku hadi siku na athari za mtikisiko wa uchumi kitaifa na kimataifa zinaonekana wazi kabisa!

Baba Mtakatifu Francisko kwa namna ya pekee kabisa, anapenda kuihamasisha Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mshikamano sanjari na kutekeleza dhamana na wajibu waliojitwalia katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu. Baba Mtakatifu anapenda kuunga mkono mkakati wa FAO unaopania kupeleka mbegu katika maeneo ambayo yameathirika sana kwa ukame na vita, kama kielelezo cha maisha na utume wa Kanisa wa kutembea bega kwa bega na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hii ndiyo changamoto inayotolewa kwa Jumuiya ya Kimataifa ya kuhakikisha kwamba, wadau mbali mbali wanachangia katika utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030. Usalama wa chakula duniani unapaswa kupewa msukumo wa pekee kabisa kwa kuonesha mshikamano ili kuwapatia chakula na lishe watu wanaoteseka kwa baa la njaa na utapiamlo! Hii ni changamoto pevu kwa FAO na kwa Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake. Hata Mama Kanisa anasema Baba Mtakatifu anataka kulivalia njuga baa la njaa na utapimlo.

Mwishoni, Baba Mtakatifu anasema kwamba, ni matumaini yake kuwa wajumbe wa mkutano mkuu wa FAO wataweza kutoa ari na mwamko mpya katika shughuli za FAO pamoja na kutoa majibu muafaka kwa watu wanaoitegemea FAO kwa kiasi kikubwa, si tu kwa masuala ya teknolojia ili kuongeza rasilimali na hatimaye kuboresha ugavi wa matunda yanayopatikana, bali kuwajengea mshikamano wa kidugu unaowahakikishia matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi. Baba Mtakatifu anawapatia wajumbe wote baraka zake za kitume ili kwamba, Mwenyezi Mungu aweze kuwakirimia nguvu wanayohitaji kwa ajili ya kusukuma mbele maendeleo endelevu ya familia ya binadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.