2017-07-01 16:17:00

Mapambano dhidi ya baa la njaa duniani!


Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, kuanzia tarehe 3 hadi 8 Julai litakuwa linaadhimisha mkutano wake wa 40 unaozishirikisha nchi 194 na wajumbe zaidi ya 600 wanatarajiwa kuhudhuria. Kati ya wawezeshaji wakuu kwenye mkutano huu wa FAO ni pamoja na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Bwana Paolo Gentiloni, Waziri Mkuu wa Italia pamoja na viongozi wengine wa Jumuiya ya Kimataifa. Hii itakuwa ni fursa kwa viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa kutafakari kwa kina na mapana changamoto endelevu kuhusu masuala ya usalama wa chakula duniani; athari za mabadiliko ya tabianchi; changamoto katika sekta ya kilimo pamoja na mchakato wa utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030.

Wajumbe wa mkutano watapembua na hatimaye, kuridhia mpango mkakati wa FAO kwa Mwaka 2018 – 2019. Jumuiya ya Kimataifa inataka kulivalia njuga tatizo la ukame ambalo kwa miaka ya hivi karibuni limekuwa ni janga kubwa kwa watu wengi Barani Afrika. Baa la njaa linakuzwa pia kutokana na vita, kinzani, ghasia na migogoro ya kijamii inayoendelea huko: Mashariki ya Kati na Afrika ya Kaskazini. Jumuiya ya Kimataifa inataka kupambana kikamilifu na baa la njaa duniani, ili hatimaye, kuitokomeza kabisa kwa kuwekeza katika usalama wa chakula sanjari na kuwajengea wakulima wadogo wadogo uwezo. Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji nalo ni changamoto kubwa katika kukabiliana na uhakika wa usalama wa chakula na lishe duniani!

Katika maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa Mwaka 2016 yaliyoongozwa na kauli mbiu “Hali ya hewa inabadilika. Hata chakula na kilimo”  Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake aliomwandikia Professa Josè Graziano da Silva, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa, FAO, kwa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka 2016 aliuliza swali la msingi kuhusu mambo yaliyosababisha mabadiliko makubwa ya tabianchi na athari zake katika masuala ya kilimo na chakula duniani! Je, ni watu kiasi gani wanaojihusisha na shughuli za kilimo, ufugaji na uvuvi duniani wanaoathirika kutokana na mabadiliko ya tabianchi? Mwishoni, Baba Mtakatifu anatoa ushauri wa mambo msingi yanayopaswa kufanyika ili kudhibiti athari za mabadiliko ya tabianchi duniani yanayoendelea kusababisha majanga makubwa kwa watu na mali zao.

Baba Mtakatifu anasema kwamba, shughuli za binadamu kwa kiasi kikubwa zimechangia uharibifu wa mazingira na matokeo yake ni athari kubwa za mabadiliko ya tabianchi changamoto na mwaliko wa kutumia vyema tafiti za kisayansi na kitamaduni katika kukabiliana vyema na athari za mabadiliko ya tabianchi kwa kusimama kidete kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote. Kanuni maadili na sera bora sanjari na mabadiliko makubwa ya mtindo wa maisha ni mambo msingi katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira. Sera na mikakati inayobainishwa na Jumuiya ya Kimataifa inapaswa kutekelezwa kikamilifu kitaifa na kimataifa kwa kujikita katika udugu unaojenga msingi wa mshikamano wa kimataifa.

Baba Mtakatifu anakaza kusema, wakulima, wafugaji na wavuvi ni watu wanaokabiliwa na changamoto kubwa za mabadiliko ya tabianchi, hali ambayo inachangia pia mabadiliko hata katika mtindo wa maisha yao, kiasi cha kujiona kwamba, wamesahaulika na kutelekezwa na Serikali pamoja na taasisi husika. Inasikitisha kuona kwamba, ongezeko la idadi ya watu duniani linachochea tamaa ya watu kutaka kujipatia faida kubwa kwa makampuni makubwa pamoja na watu binafsi kufanya mabadiliko makubwa katika mazao na misimu yake hata wakati mwingine kwenda kinyume kabisa cha asili ya mazao haya.

Ubora wa mazao yanayozalishwa kwenye maabara una faida na hasara zake, kumbe kuna haja ya kulinda, kutunza na kuendeleza sera ya utunzaji bora wa mazingira, ili kweli chakula kinachozalishwa kiweze kutosheleza mahitaji ya ongezeko la idadi ya watu duniani badala ya maendeleo ya teknolojia ya sasa katika masuala ya chakula na kilimo kuendelea kusababisha watu zaidi ya millioni 800 kuteseka kwa baa la njaa duniani. Takwimu zinaonesha kwamba, kuna idadi kubwa ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kwamba, idadi hii inatarajiwa kuongezeka maradufu, changamoto kwa watu wote kushikamana ili kulinda, kutetea na kudumisha utu na haki msingi za binadamu.

Ili kufikia lengo hili, kuna haja ya kuwa na ugavi sawa wa chakula duniani na kuhakikisha kwamba, chakula kinachozalishwa ni kwa ajili ya matumizi ya binadamu na wala si vinginevyo pamoja na kudhibiti uharibifu wa chakula wakati kuna mamillioni ya watu wanaokufa kwa baa la njaa duniani. Baba Mtakatifu anawataka wadau mbali mbali katika sekta ya chakula na kilimo kuhakikisha kwamba, wanashirikiana ili kujenga mfumo mpya wa Jumuiya ya Kimataifa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi, jambo ambalo linawezekana kabisa!

Hapa jambo la msingi ni kuhakikisha kwamba, Jumuiya ya Kimataifa inajizatiti kwa ajili ya kutosheleza mahitaji ya binadamu: kiroho na kimwili. Watu wana haki ya kupata lishe bora na ya kutosha kadiri ya mahitaji yao. Mkutano wa Marrakesh kuhusu mabadiliko ya tabianchi ilikuwa ni fursa ya kujifunga kibwebwe kutekeleza dhamana hii kwa ajili ya mahitaji ya binadamu wote sanjari na kuendelea kutekeleza Itifaki ya makubaliano ya mkutano wa mabadiliko ya tabianchi huko Paris, Ufaransa kwa kujikita katika ujasiri unaopania kuleta mwelekeo mpya wa utekelezaji wa sera za kiuchumi kielelezo makini cha utawala bora wa kitaifa na kimataifa. Baba Mtakatifu Francisko mwishoni anasema, hii ndiyo tafakari yake ambayo anapenda kuwashirikisha viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wakati huu wa maadhimisho ya Siku ya Chakula Duniani kwa mwaka 2016, huku akiwa anawakumbatia moyoni mwake, waathirika wa mabadiliko ya tabianchi ambao wengi wao wanatoka katika nchi maskini sana duniani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S.

Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican.








All the contents on this site are copyrighted ©.