2017-06-30 08:26:00

Ukarimu ni utambulisho wa Kikristo unaoimarisha udugu!


Ukarimu wetu kwa binadamu wenzetu ni ukarimu wetu kwa Kristo. Yeye anatuambia katika simulizi za siku za mwisho kwamba: “kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi”. Kwa fumbo la umwilisho Kristo anaungana na ubinadamu wetu. Wote tunakuwa ndugu zake. Umungu na ubinadamu vinakutana. Fumbo hilo linatufanya kuwa ndugu. Ukarimu wetu unaodhihirisha mshikamno wetu wa kindugu unasababishwa na fumbo la Kristo. Ni Yeye mwenyewe ambaye tunamhudumia katika nafsi za wahitaji walio mbele zetu. Hili ndilo fundisho tunalolipata katika Dominika hii ya leo ambapo tunaalikwa kuwatendea wote kwa ukarimu tukisukumwa na ukweli kwamba sote ni ndugu kwa sababu ya upendo mkubwa Mungu katika Kristo.

Kristo anatuambia: “Mwenye kuiona nafsi yake ataipoteza; naye mwenye kuipoteza nafsi yake kwa ajili  yangu ataiona”. Ni wito wa kufunguka na kuina nafsi yako katika maisha ya watu wengine. Fumbo zima la ukombozi wa mwanadamu lifumbatwa katika hili. Dhambi iliingia duniani kwa sababu mwanadamu aliacha kumsikiliza Mungu na kujisikiliza yeye mwenyewe. Tangu uumbaji Mungu alionesha wazi kwamba mwandamu anaweza kujiona na kuielewa vema nafsi yake katika mwanadamu mwenzake. Adamu alipewa vitu vyote lakini bado alikuwa anaonesha kupungukiwa na kutokujitambua. Mwenyezi Mungu akasema: “Si vema mtu huyu awe peke yake, nitamfanyia msaidizi wa kufanana naye” (Mw 2:18). Baada ya kuumbwa kwa Eva ndipo Adamu anaonesha kujitambua na kusema: “Sasa huyu ni mfupa katika mifupa yangu, na nyama katika nyama yangu” (Mw 2:23).

Mwanadamu alipoacha kumsikiliza Mungu kwa kujitambua katika nafsi ya mwingine ndipo ubinafsi ulipoanza naye kujifungua ndani ya nafsi yake. Hapa ndipo yanapoingia matendo maovu ambayo yanaipoteza hadhi ya kibinadamu. Mwenzangu haonekani tena kuwa ni ufunuo wa nafsi yangu bali kitu cha faida kwangu. Nitafanya chochote, nitakuwa mchoyo kwa mali zangu kwa ajili ya kuneemeka mimi tu na mambo yangu. Adamu alijitambua nafsi yake kwa sababu ya kujitoa nafsi yake na kwa kujitoa huko taswira inayomithilika na yeye ilitokea. Kwa kutolewa ubavu wake, alijimega na kwa njia hiyo akajitambua katika ukamilifu. Hili ni fundisho kwetu kwamba bila kujimega kwa ajili ya ufanisi wa wengine tunajiweka katika mazingira ya kutojitambua vyema.

Kristo ni mfano kwetu wa ukarimu wa kweli. Yeye ambaye “mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu ni kitu cha kushikamana nacho; bali alijifanya kuwa kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu” (Flp 2: 6 – 7). Anatupenda sisi kuliko hadhi yake na utukufu wake wa kimungu na anaachilia yote kwa ajili ya kunipata mimi na kwa ajili ya ufanisi wangu. Fumbo la Umwilisho na zaidi kwa namna kuu fumbo la Pasaka ni kielelezo chetu cha ukarimu wa kimungu. Ukarimu huu unawezeshwa na utayari wa kujishusha na kujivika unyenyekevu. Karama hii hii ya unyenyekevu ilioneshwa kwa ishara ya kuwaosha miguu mitume, usiku ule kabla ya kuteswa kwake na mwisho aliwaagiza kwamba wakatende hivyo hivyo, yaani wawe tayari kujitoa, kujishusha na kuukumbatia ubinadamu unaohitaji kuoshwa miguu kila leo hii.

Leo hii mfumo wa kijamii unashabikia sana haki na usawa. Wakati mwingine tunaona matamko mbalimbali ambayo yanaonesha kutia nguvu wazo hilo la usawa. Lakini tunapojiuliza usawa huo ni katika nini? Je, tunapopambanisha kulinganisha jamii moja na nyingine katika mfumo wa “win win situation” tunakuwa tunafanya sawa? Tunaweza vipi kupambanisha wasiolingana kwa namna mbalimbali na kushadidia kwamba iwe ni “win win situation?” Yote hii inapelekea kujiohoji jinsi gani binadamu tusivyo tayari kujifunua na kumpenda Kristo kuliko hali na uwezo wangu niliokuwa nao. Kila mmoja anavutika kuiboresha hali yake na kujionesha kuwa yu maridadi na bora zaidi bila kuwa tayari kujifunua na kumwona Kristo aliyeweka chapa yake kwa mtu mwingine. Ni changamoto kwa kutimiza ukarimu wetu kwa binadamu wenzetu.

Hapa nataka kuzungumzia kitu gani? Ni kusisitiza jinsi ambavyo uroho wa mali na madaraka, kiu ya kupata na kunyonya zaidi vitu vya wengine, ubinafsi unaokithiri hutufunika na kujikuta tunajipenda sisi wenyewe na kutokuwa tayari kuishi katika hali ya udugu kati yetu sisi wanadamu. Hali yangu njema haipaswi kabisa kumwezesha mwingine kutekeleza vema utume wake na kwa pamoja sote kuwa na hali njema. Kila mmoja ajihangaikie mwenyewe. Nipe changu nawe chukua chako na kila mtu aende na hamsini zake. Na tunabaki kufurahia hali hii kwani hata mifumo na taratibu za kijamii zinaratibu vema kwa kile kinafikirikika ni kutenda kwa haki na kuwa na Amani. Wakati mwingine nafika mbali zaidi hata kudhulumu vya wengine au kupindisha haki zao kwa ajili ya kulikuza jina langu. Yote haya ni kwa sababu siko tayari kuicha nafsi yangu kwa ajili ya wengine.

Ukristo wetu unatudai zaidi: si kumwacha kila mmoja na hamsini zake bali zapaswa kuwa ni hamsini zetu wote. Hata kama umemlipa mpiga debe wa daladala ujira wake lakini wapaswa kwenda mbele zaidi na kuangalia hali yake katika uhalisia na kuuboresha utu wake. Utakapoishia kulipa ujira wake kwa sababu ya kupiga debe tu unakuwa umemgeuza kuwa ni sawa na kifaa cha kutumia kwa faida binafsi na si mtu, ndugu yako ambaye anakuwa na hadhi kama yako. Namna utakavyomjali kutamtia nguvu na hata kumfanya aboreshe zaidi upigaji debe wake na matokeo yake chanya yataigusa jamii yote. Jamii yetu inahitaji watoa huduma mbalimbali lakini ni nini iliyo shukrani kwetu kwao kwa ukarimu wetu? Katika kijiji chetu tunampokeaje Mwalimu au daktari? Je, tunafurahia tu ahuduma zao na kujiridhisha kuwa wanapewa haki sababu ya mishahara waipokeayo? Je, tukutanapo nao mitaani tunazipokeaje hali zao za kawaida? Tunawapatia vipi msukumo nao kufanya maisha ya kawaida? Tukibaki katika mishahara tu nayo pia inabaki kuwa ni sawa na “win win situation”.

Hakika tendo la ukarimu linazaa. Mama mshumeni katika somo la kwanza anatenda kwa ukarimu na matunda yake anayaona. Anapata ahadi ya kuwa na mtoto katika hali za uzee wake. Nabii Elisha alimwambia: “Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana”. Yapo matunda mengi ambayo yanaweza kupatikana kwa sababu ya ukarimu wetu. Hii ni kwa sababu tendo la ukarimu linachachushwa na ukweli kwamba sote tu ndugu. Udugu wetu huo utatoa matunda ya usawa wa kweli wa kijamii, usawa ambao utajenga Amani, uelewwano, kusameheana, kushirikiana na mengineyo mengi. Usawa wa kweli wa kijamii haungalii mimi nitapata nini bali mimi, kwa kadiri ya vipawa nilivyokirimiwa na Mwenyezi Mungu, napaswa kutenda nini mahali hapa na muda huu. Na huo ndiyo ukarimu wa kikristo ambao unatutaka kuutafuta na kuustawiha ufalme wa Mungu hapa duniani. Kristo anasema: “Utafuteni kwanza ufalme wake na haki yake, na hayo yote mtazidishiwa” (Mt 6:33).

Mtume Paulo anatukumbusha kwamba kwa Ubatizo wetu tunazaliwa katika Kristo. Tunakuwa wana warithi wa Mungu. Hivyo ni wajibu wetu kuidhihirisha hiyo tunu njema iliyopandwa ndani mwetu. Namna yake ya kujitoa kwa ukarimu kwa ajili ya wokovu wetu haikupoteza hadhi yake bali ilikuwa sababu ya ukombozi wetu sisi naye kama asemavyo Mtume  Paulo “Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia jina lile lipitalo kila jina (Flp 2:9). Tuwe wajumbe wa Kristo na kuukarabati ubinadamu ulichakaa kwa ukarimu wetu wa kikristo.

Kutoka Studio za Radio Vatican ni mimi Padre Joseph Peter Mosha.








All the contents on this site are copyrighted ©.