2017-06-30 07:30:00

Mataifa yaachane na tofauti zao; yatokomeze silaha za maangamizi


Viongozi wa Bolivia, siku ya Jumatano tarehe 28 Juni 2017, wamewasilisha hoja katika Jumuiya ya kimataifa kuzuia utengenezaji wa silaha za maangamizi. Askofu mkuu Bernadirto Auza, Mwakilishi wa Kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa, akichangia hoja hiyo, anaelezea jinsi gani utengenezaji na usafirishaji wa silaha za maangamizi unaendelea kuwa changamoto, kwani hata baada ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kukubaliana kwa pamoja kusitisha utengenezaji wa silaha hizo, leo ni miezi sita tangu makubaliano hayo na bado inaonekana hakuna kilichobadilika.

Baba Mtakatifu Francisko anasema ni kituko cha kujipinga kuzungumzia amani, wakati silaha zinazidi kutengenezwa na kuuzwa kwenye jamii zenye kinzani na ghasia, kukubaliana hakuna tena kutengeneza silaha wakati biashara ya silaha inaonekana kuzidi kushamiri. Askofu mkuu Bernadirto Auza anasema, kanuni za uwazi, mshikamano na utekelezaji ni kanuni zinazopaswa kuzingatiwa na mataifa yote duniani, kwa yale ambayo yanakubaliwa na Jumuiya ya kimataifa.

Ujumbe wa Vatican unasisitiza umuhimu wa kusaidiana kimataifa katika kutekeleza makubaliano ya kuzuia utengenezaji na usambazaji wa silaha za maangamizi. Katika hili, nia njema na bidii makini viwekwe kuhakikisha sheria za kimataifa na Katiba ya Umoja wa Mataifa vinazingatiwa na kutekelezwa na Jumuiya ya kimataifa, katika mataifa yote. Nguvu ya pamoja na nia njema katika uwazi na ukweli ndivyo vitakavyofanikisha hilo.

Silaha ni hatari sana kwani zinaharibu vibaya mwanadamu na mali zake sehemu mbali mbali duniani, anasema Askofu mkuu Auza. Kwa mwendo wa namna hii amani haiwezi kupatikana duniani, wala malengo ya maendeleo endelevu ya hayataweza kufikiwa, nayo Jumuiya ya mwanadamu itazidi kuzama kwenye wimbi la machafuko na mateso makubwa. Hivyo ni muhimu sana mataifa yaachane na tofauti zao, yatafute suluhu kwa njia ya majadiliano, ili kusitisha vita, ili kusitisha ugaidi, ili kusitisha utengenezaji wa silaha za maangamizi.

Na Padre Celestine Nyanda.

Idhaa ya Kiswahili, Radio Vatican.

 

 

 








All the contents on this site are copyrighted ©.